top of page

Je Tusitunze Sabato kwa Sababu Hatupo Chini Ya Sheria, Bali Chini Ya Neema?


Mafungu yenye nguvu ya Maandiko kwa namna ya kusikitisha sana yanatumika vibaya ili kujaribu kuweka kitu kingine mahali pa mojawapo ya Amri [Kumi] za Mungu [wasiyoipenda], yaani, inayochukiwa karibu na viongozi hao wote ambao wao wenyewe hawataki kabisa kuyatii madai ya Amri ile ya Nne [Kut. 20:8-11], na ambao wanajaribu kuwazuia watu wasiitii, kwa kawaida wao wanalishikilia sana fungu hilo la Warumi 6:14. Wakiwa na wazo la Sabato peke yake kichwani mwao, wanajitahidi sana kuitumia lugha ya fungu hilo kwa kuihusisha Amri ile ya Nne tu [ihusuyo Sabato], wanasoma kwa kusisitiza sana, wakisema, "Hamwi chini ya Sheria [Amri Kumi], bali chini ya Neema [Msamaha]." Narudia tena, amri moja peke yake ambayo fungu hilo linatumika kuipinga ni ile ya Nne [Sabato], lakini basi, yapasa ikumbukwe kwamba Sabato ni sehemu moja tu ya Sheria hiyo [Amri Kumi], na kama ukweli huo wa kusema hatuko chini ya Sheria [Amri Kumi] unatusamehe sisi tusiweze kuishika Sabato, basi, kwa hakika kabisa unatuachilia huru tusizitii amri zile nyingine tisa za Sheria hiyo [Amri Kumi].

Hebu na tuseme ya kwamba tumelitumia fungu hilo. Chukua ile Amri ya Nane, isemayo, Usiibe." Mwizi anaposhutumiwa kwa matendo yake ya udanganyifu na kuambiwa kuwa inampasa kuishi kwa kufanya kazi kwa mikono yake, wala sio kwa udanganyifu, anaweza kujibu kwa ukali, na kusema, "Hoja yenu haiungwi mkono na Maandiko, kwa kuwa hatuko chini ya Sheria [Amri Kumi], bali chini ya neema, kwa hiyo, mimi naweza kuiba mara kwa mara kama nipendavyo."

Hebu na tuseme ya kwamba mchungaji anayeitumia hoja hiyo anakwenda China kama mmishonari. Kule anawafundisha makafiri kwamba Biblia ni Neno la Mungu, na kwamba linapaswa kutiiwa, kisha kafiri yule aliye na moyo mnyofu anayeisoma mwenyewe Biblia ile anaanza kuitunza Sabato "kwa mujibu wa amri ile." Luka 23:56, KJV; Kutoka 20:8-11. Rafiki yetu anamkemea na kusema, "Hilo si sawa kabisa; hupaswi kuitunza Sabato; sisi hatuko chini ya Sheria [Amri Kumi], bali chini ya Neema [Msamaha]." Maskini yule Mchina haoni kuwa jambo hilo ni sawa; lakini kwa kuwa ni nafuu zaidi kutoitunza Sabato kuliko kuitunza, basi, anaruhusu desturi na nafuu hiyo kufidia utusitusi wa suala hilo, naye anamtii mwalimu wake huyo mpya.

Lakini siku ya pili yake, rafiki yetu mmishonari yule anapigwa na butwaa kumwona mwongofu wake mpya akiisujudia sanamu ya kutisha sana, na kufukiza uvumba mbele yake. " Nini hiyo!" [mchungaji huyo] anatamka ghafula kwa mshangao. "Je! Hivi umesahau kwamba Mungu wetu Mkuu aliyeumba vitu vyote amesema, 'Usiwe na miungu mingine ila mimi,' tena, amesema, "Usijifanyie sanamu ya kuchonga,... usivisujudie?' " (Kutoka 20:2,4-5). Kisha mtu yule mjinga atajibu, na kusema, "Mimi sijasahau; mimi nayakumbuka vizuri sana mafundisho yako; mimi siko chini ya Sheria [Amri Kumi], bali chini ya Neema [Msamaha]." Ni kwa kutumia hoja gani basi, rafiki yetu [mmishonari] ataweza kumweleza waziwazi kuwa japo maneno haya, "hamwi chini ya Sheria [Amri Kumi], bali chini ya Neema [Msamaha]," yanaundolea mbali uwajibikaji wake kwa Amri ile ya Nne, hayawezi kupunguza hata kidogo wajibu wake wa kuzishika Amri zile nyingine zote [tisa]?

Watu hawakuokolewa katika kizazi kimoja kwa kushika Sheria [Amri Kumi] na katika kizazi kingine kwa Neema. "Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote [kuanzia Adamu] walihesabiwa haki yenye uzima." Warumi 5:18. Hivyo tunaona kwamba njia ya pekee ambayo kwayo watu wote, kuanzia mwanzo wa uumbaji mpaka mwisho wa ulimwengu huu, wangeweza kujipatia uzima wa milele ilikuwa kwa [kutegemea] kipawa hicho kilichotolewa bure kwa njia ya Yesu Kristo.

Je, hivi neema [inayopatikana kwa njia ya imani] inaibatilisha [inaifutilia mbali] Sheria ya Mungu [Amri Kumi]? Paulo anapiga kelele na kusema, "Hasha! kinyume cha hayo twaithibitisha Sheria [Amri Kumi]." Warumi 3:31. Neema na Sheria [Amri Kumi] havipingani. Kusema kweli, hapawezi kuwapo na neema yo yote kama Sheria hiyo [Amri Kumi] haiendelei kuwafunga watu wote. Mtu yule aliyeokolewa kwa neema kweli kweli, hataweza kamwe kuwa na uadui wo wote dhidi ya Sheria hiyo [Amri Kumi]. Kuna kitu kimoja tu kinachoonekana kuwa si sawa kwa mtu ye yote anayepingana na Sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Inaonyesha kwamba mtu huyo hajaongoka [hajazaliwa mara ya pili]. Yeye bado ni mtu wa mwilini. "Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii Sheria ya Mungu [Amri Kumi], wala haiwezi kuitii." Warumi 8:7.

Kielelezo kifuatacho kinaonyesha haja ya kuwa na utii kwa upande wa yule aliyeokolewa kwa neema. Tuseme kwamba mtu Fulani ameua. Alikuwa mtu mzuri kwa siku zote zilizopita, lakini kwa tendo lake hilo moja anafungwa gerezani na kuhukumiwa kufa. Maisha yake yote mazuri aliyoishi kabla ya tukio hilo hayatafaa kitu kwake sasa, kwa sababu tendo hilo moja baya litakuwa limemwondolea uhai wake. Katika seli yake huenda akaweza kutoa ahadi kwamba kamwe hatavunja tena sheria nyingine ya nchi na kwamba ataishi maisha makamilifu ya utii kwa sheria. Lakini, je! hilo litamwokoa asinyongwe? Sivyo kabisa. Tendo moja la kuua limemgharimu maisha yake wala hawezi kuokolewa kwa matendo yake mema au kwa kushika sheria. Sheria haiwezi sasa kumpa uzima. Inaendelea tu kupiga kelele, ikisema kwamba anapaswa kukabiliwa na mauti [kifo]. Ilitungwa ili iwe sheria ya kuhifadhi maisha ya watu, lakini sasa imegeuka na kuwa sheria ya mauti kwa yule aliyeivunja. Kabla ya hapo ilikuwa ni sharia iliyokuwa na uwezo wa kumfunga [kumweka katika hali ya uwajibikaji daima]. Sasa imemfunga katika seli [chumba kidogo cha gereza] na kumhukumu kufa. Hakuna njia yo yoter inayowezekana ili kuifanya sheria ile kumwokoa mhalifu huyo sasa, isipokuwa tu kama imefutwa, lakini sheria dhidi ya mauaji haiwezi kufutwa.

Ndipo mtu yule aliyehukumiwa kufa anakata rufaa kwa Gavana [au Rais] kuomba msamaha. Na siku moja anatembea na kuingia katika seli yake mtu mmoja mwenye msamaha mkononi mwake ulioandikwa juu yake neno hili, "umeokolewa kwa neema." Je, mtu yule ameokolewa kwa sheria ile au kwa kuitunza sheria ile? La, ameokolewa kwa neema peke yake. Akiwa ameupata wokovu huo kwa neema, anakuwa huru kutoka katika hali ya kufungwa na Sheria hiyo. Lakini basi, hebu nikuulize, kwa vile mtu huyo ameokolewa kwa neema, je! anao uhuru kutoka nje na kwenda kuwaua watu wengi kwa kuwapiga risasi kama atakavyo yeye, ama sheria hiyo itakuwa imefutwa kwa sababu tu ameokolewa kwa neema? Neema hiyo inamweka huru mbali na lawama [mashtaka] ya Sheria hiyo [huko ndiko kuwa chini ya Sheria], lakini sio mbali na mamlaka ya [udhibiti wa] Sheria hiyo.

Neema sio tu kwamba inasamehe uvunjaji wa Sheria [dhambi] uliopita, bali ni uweza unaotulinda sisi tusitende dhambi [tusiivunje Sheria ile ya Amri Kumi] kwa wakati huu wa sasa.

bottom of page