Katika kusoma vijizuu na vitabu vinavyotumwa kwangu vikipinga Sabato ile ya Amri ya Nne, bila kuhitilafiana ko kote inatajwa kama Sabato ya Wayahudi. Hivyo waandishi hao wanajaribu kuilundikizia chuki au dharau juu yake [siku hiyo ya Sabato]. Kwa nini waandishi hao wasitumie lugha ya Biblia na kuiita Amri ile ya Nne kuwa ni "Sabato ya BWANA [YEHOVA], Mungu wako"? [Kutoka 20:10.]
Ni kweli kwamba Amri ile ya Sabato pamoja ni zile nyingine tisa zilitangazwa rasmi kutoka Sinai mbele ya umati ule mkubwa wa watu wale ambao kwa sehemu kubwa sana walikuwa Wayahudi. Lakini, je! hiyo ndiyo sababu yote ya kutojihusisha kwetu kabisa na Sabato hiyo? Je! hatutakuwa na heshima iwayo yote kwa manabii wale na mitume kwa sababu wote walikuwa Wayahudi? Je! tutamkataa Yesu, kwa kuwa ali"twaa asili ya mzao wa Ibrahimu"? Waebrania 2:16. Tena alitembea katikati ya watu wale kama Myahudi. Je! yule Muasisi wa wokovu wetu hakupata kusema kwamba "wokovu watoka kwa Wayahudi"? Yohana 4:22. Je! Hivi sisi tutakataa kwenda mbinguni ati kwa sababu juu ya kila mlango wa mji ule kuna jina la Myahudi na kwa sababu majina ya Wayahudi tu yameandikwa katika misingi yote ya kuta zile? Ufunuo 21:12,14. Je! sisi tunaweza kuhitimisha [hoja hii] kwa kusema kwamba manabii wote wa Biblia, mitume, Mwokozi, wokovu, na mbingu, vyote hivyo vitawahusu Wayahudi peke yao? Lo! ni mbali jinsi gani tunaweza kwenda tunapofuata mkondo mbaya wa kufikiri [mawazo potofu]!
Mathalani, chukua uzoefu wa maisha wa wanafunzi wale watatu, yaani, Petro, Yakobo na Yohana ----- wote wakiwa Wayahudi. Siku moja Kristo aliwachukua na kwenda nao juu ya Mlima ule wa Kubadilika Sura Yake [Mlima wa Mizeituni], kisha sauti ikatoka mbinguni ikisema, "Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye." Luka 9:35. Je! kwa hiyo sisi tuelewe kwamba agizo hilo lilipaswa kutiiwa na wale wanafunzi watatu tu, au zaidi sana, na taifa lote la Wayahudi tu ambalo wao walikuwa sehemu yake? Sababu hiyo ingekuwa ya maana sawa tu na hitimisho lihusulo Amri ya Sabato. Mungu aliliheshimu taifa la Wayahudi kwa kuwaita watu wake wa pekee. Akawapa kweli zake zote. Akawafunulia Masihi yule aliyeahidiwa kwa njia ya mifano na vivuli. Aliwapa maagano na kukusudia kuwa wao watakuwa nuru ya ulimwengu. Akawaweka kwenye eneo muhimu la nchi, lililokuwa lango kuu la [njia kuu ya] Mataifa. Ndiyo, walishindwa kumfuata! Lakini, je! zile kweli alizowapa Mungu zilikoma kwa sababu taifa lile lilishindwa kumfuata? Mungu bado ni Mungu. Kweli bado ni Kweli. Siku ya saba bado ni "Sabato ya BWANA, Mungu wako." Kristo alitangaza akisema: "Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu." Marko 2:27. Hakusema kwa ajili ya Myahudi, bali kwa ajili ya mwanadamu!
Kama sisi ni wanadamu, basi, Mungu aliifanya Sabato kwa ajili yetu! Sabato ilifanyika wakati wa uumbaji kwa ajili ya mwanadamu. Mwanadamu peke yake aliyekuwako wakati ule alikuwa Adamu. Katika Isaya 56:1-8 nabii huyo anazungumza juu ya siku za mwisho za kufungwa kwa historia ya dunia hii, naye anazungumza juu ya baraka itakayowajia "mgeni" aitunzaye Sabato hiyo.