top of page

JE, WAFU WANAWEZA KUONGEA NASI?

hell-on-earth-large.jpg

 Huduma ya malaika watakatifu, kama ilivyoelezwa katika Maandiko, ni ukweli wenye
faraja kuu na wa thamani kwa kila mfuasi wa Kristo. Walakini fundisho la Biblia juu ya 
jambo hili limetiwa giza na kupotoshwa kwa njia ya makosa yanayotokana na theolojia
inayopendwa sana na watu wengi. Fundisho lile lisemalo kwamba mwanadamu ana roho 
isiyokufa, ambalo liliazimwa kwanza kutoka kwa falsafa ya kipagani, na hatimaye wakati
wa giza lile la UASI MKUU likaingizwa katika imani ya Kikristo, limechukua mahali pa
ile kweli, inayofundishwa kwa wazi kabisa katika Maandiko, kwamba "WAFU 
HAWAJUI NENO LO LOTE." Watu wengi sana wamekuja kuamini kwamba ni roho za
wale waliokufa "watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu."  
Walakini [imani] hiyo ni kinyume na ushuhuda wa Maandiko yanayohusu kuwako kwa
malaika mbinguni, na uhusiano wao na historia ya mwanadamu, kabla ya [kutokea] kifo
cha mwanadamu ye yote. 

 Fundisho lisemalo kwamba mtu anapokufa anaendelea kuishi, hasa imani ile isemayo 
kwamba roho za wafu zinarudi kuja kuwatumikia walio hai, limetayarisha njia kwa dini
ya siku hizi ya kuongea na mizimu (modern spiritualism). Kama wafu wanaruhusiwa
kufika mbele za Mungu na mbele ya malaika watakatifu, na kupewa uwezo wa kuwa na 
maarifa yanayozidi yale waliyokuwa nayo kwanza, kwa nini, basi, wasirudi duniani na
kugawa maarifa yao na kuwafundisha walio hai? Iwapo roho za wafu zinarukaruka juu ya 
[vichwa vya] rafiki zao waliomo duniani humu, kama wafundishavyo wanatheolojia hao
wanaopendwa sana na watu wengi, kwa nini, basi, wasiruhusiwe kuongea nao, na
kuwaonya dhidi ya maovu, ama kuwafariji katika huzuni zao? Ni kwa jinsi gani wale 
wanaoamini kwamba mtu akifa roho yake inaendelea kuishi wanaweza KUIKATAA
nuru ile inayowajia kama nuru itokayo mbinguni ambayo inaletwa na pepo [roho] hao 
wenye utukufu? Hapo ndipo ipo njia inayodhaniwa kuwa ni takatifu, ambayo Shetani
anaitumia kutekeleza MAKUSUDI yake. Malaika wale walioanguka ambao
wanatekeleza amri zake [Shetani]  wanakuja kama wajumbe wanaotoka katika 
ulimwengu wa roho.  Wakati [wenye dini ya mizimu] wanadai kwamba wanawaleta
walio hai katika mawasiliano na wafu, hapo ndipo yule mkuu wa uovu anapotumia nguvu 
yake ya uchawi juu ya mioyo [akili] yao [hao walio hai].

 Anao uwezo wa kuleta mbele ya wanadamu mfano [kivuli] wa ndugu zao waliokufa. 
Mfano huo [umbile la marehemu] unakuwa kamili; mtazamo wake huwa ni ule ule
waliouzoea kuuona, maneno yake, sauti yake, huigwa kabisa kwa namna ya kushangaza 
sana.  Wengi hufarijika kwa matumaini ya kwamba ndugu zao wapendwa wanafurahia
raha isiyo na kifani kule mbinguni, na bila kushuku hatari inayowakabili, wanatega sikio
lao "wakisikiliza roho [mapepo] zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani." [l 
Timotheo 4:l.]
 
 Baada ya kusadiki kwamba wafu wanarudi kweli na kuongea nao, Shetani anafanya
watokee wale walioingia makaburini mwao wakiwa hawajajiweka tayari [yaani, waovu]. 
Hao hudai kwamba wanayo furaha mbinguni na ya kwamba wanakalia hata vyeo vya juu
kule, na kwa njia hiyo uongo unaenezwa kote kwamba hakuna tofauti yo yote kati ya 
wenye haki na waovu. Wageni hao wasemao uongo [mapepo] wanaowatembelea
[wanadamu] kutoka katika ulimwengu wa roho wakati mwingine wanatoa tahadhari na 
maonyo ambayo hutokea kuwa ni ya kweli. Basi, imani [ya walio hai] inapoimarishwa
hivyo, wanaanza kutoa mafundisho ambayo moja kwa moja yanaihafifisha imani [ya
watu hao] katika Maandiko. Huku  wakijionyesha kuwa wanapenda sana kuwaona 
marafiki zao waliomo duniani wakiwa na hali njema ya maisha, wanapenyeza
mafundisho ya uongo kwa hila ambayo ni ya hatari sana [kiroho]. Ukweli wa kwamba 
wanatoa baadhi ya mafundisho yaliyo ya kweli, na wakati fulani wanaweza kubashiri
matukio yatakayotokea baadaye, hufanya maneno yao wanayosema yawe na mwonekano
wa kutegemewa;  mafundisho yao ya uongo yanapokelewa kwa upesi na watu wengi 
sana, na kusadikiwa kabisa [pasipo shaka lo lote], kana kwamba [maneno hayo] yalikuwa
ni zile kweli takatifu sana za Biblia.  Sheria ya Mungu [Amri Kumi] huwekwa kando, 
Roho wa neema anadharauliwa, na damu ile ya agano inahesabiwa kuwa ni kitu kilicho
najisi. Roho hizo [mapepo] zinakana Uungu wa Kristo na hata zinamweka Muumbaji
kuwa yuko sawa nazo. Hivyo chini ya umbo hilo jipya la kuigiza Mwasi yule Mkuu 
[Shetani] bado anaendelea na pambano lake dhidi ya Mungu lililoanza kule mbinguni na
[sasa] ni karibu miaka elfu sita limeendelezwa duniani humu. 


 
 MAONYESHO YA  UWEZO WA MAPEPO


 Wengi hujaribu kueleza sababu ya maonyesho ya uwezo wa mapepo [miujiza] kwa 
kusema kwamba hiyo ni hila na kiinimacho kwa upande wa yule kijumbe. Walakini,
japokuwa ni kweli kwamba mara nyingi matokeo hayo ya kiinimacho [mazingaombwe] 
yamefanywa kwa kutumia hila na kudaiwa kuwa ni maonyesho ya kweli, pia ni kweli
kwamba kumekuwako na maonyesho yaliyotendwa yanayoonyesha uwezo usiokuwa wa
kibinadamu. Kule kugonga-gonga kwa ajabu ambako kulianzisha Imani hii ya Mizimu ya 
Kisasa (modern spiritualism) hakukutokana na udanganyifu wala hila za mwanadamu,
bali ilikuwa ni kazi ya moja kwa moja ya mapepo [malaika] wale wabaya, ambao kwa 
njia hiyo walianzisha mojawapo ya madanganyo yaliyofanikiwa sana katika
kuziangamiza roho za watu wengi. Wengi watanaswa kwa kuamini kwamba Imani hii ya
Mizimu ni udanganyifu tu wa kibinadamu; hapo watakapokutana ana kwa ana na 
maonyesho ambayo watayafikiria kuwa si kitu kingine bali ni mwujiza, ndipo
watakapodanganyika, na kushawishika kuyakubali kama ni uweza mkuu wa Mungu. 

 Watu hao wanapuuzia ushuhuda wa Maandiko kuhusu maajabu yanayofanywa na
Shetani na vibaraka wake. Ilikuwa ni kwa msaada wa Shetani wale wachawi wa Farao 
waliweza kuigiza [baadhi ya] matendo ya Mungu. Paulo anashuhudia kwamba kabla ya
marejeo ya Kristo kutakuwa na maonyesho [miujiza] yanayofanana na hayo 
yatakayofanywa kwa uwezo wa Shetani. Kuja kwake Bwana kutatanguliwa na "kutenda
kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo 
yote ya udhalimu." 2 Wathesalonike 2:9,10. Naye Mtume Yohana, akiwa anaelezea juu
ya nguvu hiyo itendayo miujiza ambayo itajitokeza katika siku za mwisho, anasema kwa 
mkazo: "Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu
ya nchi mbele ya wanadamu. Naye AWAKOSESHA wale wakaao juu ya nchi, kwa 
ISHARA zile alizopewa [alizo na uwezo kabisa wa] kuzifanya."  Ufunuo l3:l3,l4. Huo
sio udanganyifu tu unaotabiriwa hapa.  Wanadamu wanadanganywa kwa miujiza ambayo
MAWAKALA WA SHETANI [2 Wakorintho 11:13-15] wanao uwezo wa kuifanya, sio 
wanayojifanya kuifanya.
 


   MKUU WA GIZA 

 

 Mkuu wa giza, ambaye kwa muda mrefu sana anatumia nguvu zake za akili kufanya kazi
ya kuwadanganya watu, kwa werevu anabadilisha majaribu yake kwa wanadamu wa 
tabaka zote na kila hali. Kwa wasomi na waungwana anawaletea Imani hii ya Mizimu
katika hali yake ya kitaalam na kiungwana, naye kwa njia hiyo anafanikiwa kuwavuta 
wengi katika mtego wake. Hekima inayotolewa na Imani hii ya Mizimu ni ile iliyoelezwa
na Mtume Yakobo, ambayo "siyo ile ishukayo kutoka mbinguni, bali ni ya dunia, ya tabia
ya kibinadamu, na Shetani." Yakobo 3:15.  Walakini, jambo hilo Mlaghai huyu Mkuu 
hulificha [kwao] anapoona kuficha kutamfaa kwa makusudi yake. Yule ambaye aliweza
kuonekana amevikwa mavazi ya nuru yanayovaliwa na makerubi walioko mbinguni 
wakati ule alipomjia Kristo katika nyika ile ya majaribu, anawajia wanadamu kwa njia ya
kuvutia kabisa kama malaika wa nuru. Anaishawishi akili kwa kuleta mafundisho makuu
yanayowachangamsha sana; anayafurahisha mawazo yao kwa kuwaletea mandhari 
[matukio] za kuifurahisha mno mioyo yao;  naye anayashirikisha mapenzi ya moyoni
mwao kwa usemi wake wa ufasaha akionyesha upendo na huruma. Anayachochea 
mawazo yao yaweze kupaa juu, akiwaongoza wanadamu kujivunia sana hekima yao kiasi
cha kumdharau Yule wa Milele mioyoni mwao. Kiumbe yule mwenye nguvu nyingi
ambaye aliweza KUMCHUKUA Mkombozi wa ulimwengu huu mpaka juu kwenye 
kilele cha mlima ule mrefu sana na kuleta mbele yake falme zote za dunia pamoja na
utukufu wake, ataleta majaribu yake kwa wanadamu kwa njia ya kuzipotosha fahamu za 
wale wote ambao hawajalindwa na nguvu ya Mungu.

 Shetani anawadanganya watu LEO kama alivyomdanganya Hawa kule Edeni kwa 
kuwasifu mno, kwa kuamsha tamaa ya kujipatia maarifa yaliyokatazwa, na kwa kuamsha
tamaa nyingi ya kujikweza.  Ilikuwa ni kwa njia ya kuyapenda sana maovu haya hata 
yakasababisha anguko lake [Shetani], na kwa njia ya [maovu] hayo anakusudia kupata
ufanisi wa kuwaangamiza wanadamu. "Mtakuwa kama Mungu," anasema kwa nguvu,
"mkijua mema na mabaya."  Mwanzo 3:5. Imani ya Mizimu inafundisha "kwamba 
mwanadamu ni kiumbe cha maendeleo, hata mpaka milele ataufikia Uungu." Na tena:
"Kila mtu atajihukumu mwenyewe wala sio [mtu] mwingine [kumhukumu]." "Hukumu 
hiyo itakuwa ya haki, kwa sababu ni hukumu inayotolewa na NAFSI yenyewe... Kiti cha
enzi kiko ndani yako." Mwalimu wa Imani hii ya Mizimu alisema hivi wakati  "utambuzi 
wa kiroho" ulipoamka ndani yake: "Ndugu zangu, wote walikuwa nusu-miungu
wasioanguka." Na mwingine anasisitiza hivi: "Mtu ye yote mwenye haki na aliye 
mkamilifu huyo ni Kristo."
 
 Kwa hiyo, badala ya haki na ukamilifu wa Mungu wa milele, ambaye ndiye lengo kuu la
ibada; badala ya haki kamilifu ya Sheria yake [Amri Kumi], ambayo ndicho kipimo cha
kweli cha mafanikio ya mwanadamu, Shetani ameweka tabia ya mwanadamu mwenye 
dhambi na makosa kuwa ndilo lengo pekee la ibada, kanuni pekee ya hukumu, au kanuni
ya tabia. Hayo ndiyo maendeleo, sio kwenda juu, bali kwenda chini. 


 
 KWA KUTAZAMA  TUNABADILIKA


 Ni sheria ya maumbile kiakili na kiroho kwamba kwa kutazama tunabadilika. Akili 
inajirekebisha yenyewe kulingana na mambo inayoruhusiwa kuyawaza kwa muda mrefu.
Inafanana na kile ambacho imezoea kukipenda na kukiheshimu. Mtu hatapanda juu zaidi 
ya ile kanuni yake ya usafi [wa maisha] au wema au kweli.  Kama nafsi yake ndicho
kipeo chake cha juu sana, basi, hataweza kupata kitu cho chote kilicho bora zaidi kuliko
hiyo. Zaidi sana, daima atazidi kuzama chini zaidi na zaidi. Akiachwa hivyo peke yake, 
ni lazima njia yake [ya maisha] itaelekea chini tu.
 
 Kwa yule anayetimiza tamaa zake za mwili pasipo kujizuia, mpenda anasa, na
mwasherati, Imani hii ya Mizimu inaletwa kwake kwa kificho kisichokuwa cha siri sana
kama kwa msomi na mwungwana; katika mifumo yake michafu sana wanapata kitu 
kinachoafikiana na mwelekeo wao. Shetani anajifunza kila dalili ya tabia dhaifu ya
kibinadamu, anaziangalia kwa makini dhambi ambazo kila mmoja anaelekea kuzifanya, 
na kisha anahakikisha kwamba nafasi hazitakuwa chache za kutosheleza mwelekeo huo
wa dhambi. Anawajaribu watu kwa kutokuwa na kiasi katika kile ambacho chenyewe ni
halali, akiwafanya, kwa utovu wao wa kiasi, kudhoofisha nguvu zao za mwili, akili, na 
maadili. Amewaharibu na bado anaendelea kuwaharibu maelfu kwa njia ya kutimiza
tamaa zao za mwili, na kwa njia hiyo kuifanya tabia yote ya mwanadamu iwe kama ya 
mnyama. Na katika kuikamilisha kazi yake hiyo, anatangaza, kwa njia ya mapepo,
kwamba "ujuzi wa kweli unamweka mwanadamu juu ya Sheria;" kwamba "cho chote
kilichopo, ni halali;" kwamba "Mungu hahukumu;" na kwamba "dhambi ZOTE 
zinazotendwa hazina ubaya wo wote." Watu wanaposhawishika kusadiki hivyo kwamba
tamaa ndiyo sheria ya juu kuliko zote, kwamba uhuru ni ruhusa [ya kufanya watakavyo]; 
na ya kwamba mwanadamu anawajibika tu kwake mwenyewe, ni nani, basi, awezaye
kushangaa kwamba upotovu na tabia zilizoharibika zimezagaa kila upande? Watu wengi
sana kwa furaha wanayakubali mafundisho yale yanayowaacha huru kufanya sawasawa 
na hisia zao zinazotoka katika mioyo yao yenye dhambi. Kamba za kujizuia wameziweka
katika shingo ya tamaa mbaya, nguvu zao za akili na roho zimetawaliwa na mwelekeo wa 
kinyama wa miili yao, na Shetani akiwa anashangilia anawaingiza katika wavu wake
maelfu ya wale wanaojidai kwamba ni wafuasi wake Kristo. 

 Lakini hakuna haja kwa mtu ye yote kudanganyika kwa  kuyasikiliza madai ya uongo ya 
Imani hiyo ya Mizimu. Mungu ameupa ulimwengu huu nuru ya kutosha kuwawezesha
[wanadamu] kugundua mtego huo. Kama ilivyokwisha kuonyeshwa tayari, NADHARIA 
hiyo inayojenga msingi halisi wa Imani ya Mizimu inayapiga vita maneno yaliyo wazi
kabisa ya Maandiko. Biblia inatangaza kwamba wafu hawajui neno lo lote, kwamba
mawazo yao yamepotea; hawana sehemu tena katika jambo lo lote linalofanyika chini ya 
jua; hawajui cho chote kuhusu furaha au majonzi ya wale waliopendwa sana nao waliopo
hapa duniani. 


 
 MAWASILIANO YALIYOPIGWA MARUFUKU
 
 Zaidi ya hayo, Mungu kwa makusudi mazima amekataza mawasiliano yote na wale
wanaojidai kuwa ni roho za waliokufa.  Katika siku zile za Waebrania kulikuwa na kundi
fulani la watu waliodai, kama wanavyodai wenye imani ya mizimu leo, kwamba 
walikuwa na mawasiliano na wafu. Walakini "mapepo" hayo kama walivyoitwa wageni
wale hayakutoka katika dunia zingine, yanatangazwa na Biblia kuwa hayo ni "ROHO ZA 
MASHETANI."  (Linganisha Hesabu 25:1-3; Zaburi 106:28; l Wakorintho 10:20; 
Ufunuo 16:14.) Kazi ya kushughulika na "wenye pepo" [wachawi] ilitangazwa kuwa ni
CHUKIZO kwa Bwana, tena ilikatazwa kabisa kwa adhabu ya kifo. Mambo ya Walawi 
19:31; 20:27. Neno hilo la uchawi siku hizi linadharauliwa. Madai kwamba wanadamu
wanaweza kuongea na pepo wabaya yanaonekana kuwa ni hadithi za uongo za Zama zile 
za Giza. Lakini, Imani hii ya Mizimu [Umizimu], ambayo inawahesabu wafuasi wake
kwa mamia ya maelfu, naam, kwa mamilioni, imejipenyeza na kuingia katika mazingira
ya wanasayansi, imeyashambulia makanisa, nayo imepata washabiki katika vyombo vya 
kutunga sheria za nchi, na hata kwenye majumba ya wafalme ----- udanganyifu huu
mkubwa sana, katika umbo lake la kujificha, ni kurudi tu kwa uchawi ule uliolaaniwa na 
kupigwa marufuku hapo zamani.

 Kama pasingekuwapo na ushahidi mwingine wa tabia halisi ya Imani hii ya Mizimu, 
ingetosha kwa Mkristo kujua kwamba mapepo hayo hayatofautishi kati ya haki na
dhambi, kati ya Mitume adhimu sana na watakatifu wa Kristo na watumishi wale wa 
Shetani wafisadi mno. Kwa kuwaonyesha watu waliokuwa waovu kupindukia kuwa
wako mbinguni na kwamba wamepewa vyeo vikubwa sana huko, Shetani anaiambia
dunia hii kwamba: "Si kitu kama wewe ni mwovu kiasi gani, si kitu kama unamwamini 
au humwamini Mungu wa Biblia. Uishi upendavyo; mbinguni ni nyumbani kwako." Kwa
kweli, waalimu wale wa Imani ya Mizimu wanatangaza hivi: "Kila mmoja atendaye 
dhambi ni mwema machoni pake Bwana, naye anawafurahia; au, Mungu wa hukumu
yuko wapi?" Malaki 2:17.  Neno la Mungu lasema hivi: "Ole wao wasemao kwamba
uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya 
giza." Isaya 5:20.
 
 Mitume, kama wanavyoigizwa na roho hizo zidanganyazo [mapepo], wanafanywa
waweze kusema maneno ya kukanusha yale waliyoyaandika kwa uongozi wa Roho 
Mtakatifu walipokuwa hapa duniani. Wanakanusha kwamba Biblia haikutoka kwa
Mungu, na kwa kufanya hivyo wanaupasua msingi wa TUMAINI LA MKRISTO na  
KUIZIMA NURU inayoonyesha njia ya kwenda mbinguni. Shetani anaifanya dunia
isadiki kwamba Biblia ilikuwa ni hadithi za uongo tu, au kitabu kilichofaa kwa kizazi kile 
kichanga cha wanadamu [wa mwanzo], lakini kwa sasa kinafaa kuangaliwa kwa juu juu
tu, au kutupiliwa mbali kama kitu kilichopitwa na wakati.  Na mahali pa Neno la Mungu
anaweka MAONYESHO [MIUJIZA] YA MAPEPO. Hapa ndipo ilipo njia iliyodhibitiwa 
kabisa na yeye [Shetani]; kwa njia hii anaweza kuifanya dunia isadiki cho chote
atakacho. Kitabu kile KITAKACHOMHUKUMU yeye na wafuasi wake anakitupa 
kivulini, mahali anapotaka hasa kiwe; Mwokozi wa ulimwengu huu anamfanya aonekane
kuwa sio zaidi ya mwanadamu wa kawaida tu. Na kama vile askari wale wa Kirumi
waliolilinda kaburi lile la Yesu walivyotangaza habari za uongo ambazo makuhani na 
wazee waliweka kinywani mwao ili kukanusha ufufuo wake [Kristo], ndivyo waumini wa
maonyesho [miujiza] haya ya mapepo wanavyojaribu kufanya ionekane kwamba hakuna 
mwujiza wo wote unaoweza kuonekana katika matukio yanayohusu maisha ya Mwokozi
wetu. Baada ya kutafuta kwa njia hiyo namna ya kumweka Yesu nyuma [ili watu
wamsahau], wanawataka watu kuiangalia miujiza yao wakijitapa kwamba hiyo inaipita 
kabisa ile ya Kristo.
 


 IMANI YA MIZIMU  YABADILISHA SURA YAKE 

 

 Ni kweli kwamba Imani ya Mizimu sasa inabadilisha sura yake, na, ikiwa imeficha
baadhi ya mambo yake yasiyokubalika, inavaa VAZI LA KIKRISTO. Lakini maneno 
yake toka jukwaani na katika vitabu vyake kwa miaka mingi yamekuwa mbele ya Umma,
na katika hayo tabia yake halisi inaonekana wazi. Mafundisho haya hayawezi kukanwa 
wala kufichwa.

 Hata katika sura yake ya sasa, mbali na kuweza kustahili kuvumiliwa kama zamani, 
yamekuwa ya hatari kweli kweli, kwa sababu ni udanganyifu ulio mgumu kuutambua
kwa urahisi. Hapo zamani [imani hii] ilimshutumu Kristo na Biblia, sasa INAJIDAI 
kuvikubali vyote viwili. Walakini Biblia inatafsiriwa kwa njia ambayo inapendeza kwa
moyo ule usioongoka, ambapo KWELI ZAKE NZITO NA ZA MAANA zinafanywa
kuwa ni ubatili mtupu. Upendo unaongelewa sana kuwa ndiyo tabia kuu ya Mungu, 
lakini unadhalilishwa na kuwa hisia duni za tamaa ya mwili, bila kuweka tofauti yo yote
kati ya mema na mabaya. Haki ya Mungu, kukemea dhambi kwake, matakwa ya Sheria 
yake takatifu [Amri Kumi], vyote hivyo wao hawavioni [wanavidharau]. Watu
wanafundishwa kuiona Sheria ile ya Amri Kumi kama ni waraka uliokufa [yaani,
usiokuwa na kazi]. Hadithi za uongo zinazopendeza zinayashikilia mawazo ya watu na 
kuwafanya waikatae Biblia kama msingi wa imani yao. Kwa kweli, Kristo anakataliwa
kama zamani; lakini Shetani ameyapofusha macho ya watu hao kiasi kwamba 
udanganyifu huo hauwezi kutambulikana.
 
 Kuna wachache mno ambao wanayo dhana sahihi ya udanganyifu wa nguvu hiyo ya
Imani ya Mizimu na hatari ya kujiingiza chini ya mvuto wake. Wengi wanachezacheza 
nayo tu kwa ajili ya kutosheleza udadisi wao. Hawana imani ya kweli katika hiyo, tena
wangejazwa na hofu kuu kuwazia kujisalimisha wenyewe ili watawaliwe na mapepo hao. 
Lakini wanaukanyaga uwanja ule uliokatazwa, na Mharabu huyo mwenye nguvu nyingi
anatumia uwezo wake [wa uchawi] juu yao kinyume na matakwa yao. Hebu kwa mara
moja tu washawishike kuitoa mioyo yao upande wake [Shetani],  atawashikilia mateka. 
Haiwezekani, kwa nguvu zao, kujinasua na nguvu yake ya uchawi yenye ushawishi
aliyowatupia. Hakuna kitu cho chote kinachoweza kuwaokoa watu hao walionaswa, 
isipokuwa ni uweza wa Mungu utolewao kama jibu kwa maombi ya bidii yaliyojaa
imani.
 

 
 KWA SHERIA  NA USHUHUDA

 

 Asema hivi nabii Isaya: "Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye 
pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! haiwapasi watu kutafuta
habari kwa Mungu wao?  je! waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?
Na waende kwa SHERIA na USHUHUDA; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila 
shaka kwa hao hapana asubuhi." Isaya 8:19,20.  Endapo watu wangekuwa tayari kupokea
kweli ile iliyoelezwa wazi katika Maandiko kuhusu ASILI YA MWANADAMU na 
HALI YA WAFU,  wangeona katika madai hayo na maonyesho [miujiza] ya mizimu
kutenda kwake Shetani kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo. Lakini basi, kuliko
kuachana na uhuru ule unaoafikiana na moyo usioongoka, na kuzikataa dhambi 
wazipendazo, watu wengi sana wanafumba macho yao ili wasiione nuru hii, nao wanazidi
kusonga mbele, bila kujali maonyo, wakati Shetani naye anatega mitego yake 
kuwazunguka, nao wanakuwa mateka wake. "Kwa sababu hawakukubali KUIPENDA
ILE KWELI [KUITUMIA KATIKA MAISHA YAO], wapate kuokolewa," kwa hiyo
"Mungu AWALETEA [HAIZUII] NGUVU YA UPOTEVU; wauamini UONGO." 2 
Wathesalonike 2:10,11.
 
 Wale wanaoyapinga mafundisho ya Imani ya Mizimu wanawashambulia, sio wanadamu
peke yao, bali Shetani na malaika zake. Wameingia katika pambano dhidi ya falme, na
mamlaka na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Shetani hatakubali 
kuiachia hata inchi moja ya eneo lake isipokuwa kama amerudishwa nyuma kwa uwezo
wa wajumbe wale watokao mbinguni.  Watu wa Mungu wangeweza kukabiliana naye, 
kama alivyofanya Mwokozi, kwa kutumia neno hili: "IMEANDIKWA." Shetani naye
anaweza kunukuu Maandiko kama siku zile za Kristo, naye ataweza kuyapotosha
mafundisho ili kuendeleza madanganyo yake. Wale wanaotaka kusimama katika siku hizi 
za mwisho za hatari inawapasa wao wenyewe kuuelewa ushuhuda huo wa Maandiko.
 
 Wengi watapambana na roho za mashetani zikija kwao katika umbile la ndugu zao
wapendwa [waliokufa] au marafiki zao [waliokufa] na kuwatangazia uzushi wa hatari 
mno. Wageni hao wataigusa mioyo yetu na kufanya miujiza ili kudumisha uongo wao. 
Yatupasa kuwa tayari KUWAPINGA kwa kutumia ukweli wa Biblia usemao kwamba 
WAFU HAWAJUI NENO LO LOTE na kwamba wale wanaokuja katika umbile hilo ni
ROHO ZA MASHETANI.

 

 Karibu sana mbele yetu inakuja "saa ya kujaribiwa iliyo tayari kuujia ulimwengu wote,
kuwajaribu wakaao juu ya nchi."  Ufunuo 3:10. Wale ambao imani yao haijajizatiti juu ya 
Neno la Mungu watadanganyika na kushindwa. Shetani anafanya kazi yake kwa kutumia
"madanganyo yote ya udhalimu" ili kuwatawala wana wa wanadamu, na madanganyo 
yake yatazidi kuongezeka daima. Lakini anaweza kufikia lengo lake tu kama watu
wanajitoa wenyewe kwa hiari yao kuingia katika majaribu yake. Wale wanaotafuta kwa
bidii KUIJUA KWELI na kujitahidi KUZITAKASA ROHO ZAO KWA KUTII, kwa 
njia hiyo, wakifanya kila linalowezekana [kwa upande wao] kujiandaa kwa pambano
hilo, wataipata NGOME IMARA ndani ya Mungu wa kweli. "Kwa kuwa umelishika 
NENO la subira yangu, Mimi nami NITAKULINDA" (Fungu la 10), ni ahadi ya
Mwokozi. Angeweza kutuma kila malaika kutoka mbinguni kuwalinda watu wake kuliko
kumwacha mtu mmoja anayemtumainia kushindwa na Shetani. 

 Nabii Isaya anaufunua udanganyifu wa kutisha utakaowajia waovu, ukiwafanya 
wajihesabu kuwa wako salama kutokana na hukumu za Mungu: "TUMEFANYA
AGANO NA MAUTI, TUMEPATANA NA KUZIMU;  pigo lifurikalo litakapopita,
halitatufikia sisi; kwa maana TUMEFANYA MANENO YA UONGO KUWA 
KIMBILIO LETU, TUMEJIFICHA CHINI YA MANENO YASIYO KWELI." Isaya
28:15. Katika kundi hili linaloelezwa hapa wamo wale ambao kwa kiburi chao cha 
kutotaka kutubu wanajifariji wenyewe kwa maneno yasemayo kwamba mwenye dhambi
hataweza kuhukumiwa; kwamba wanadamu wote, haidhuru wawe waovu kiasi gani,
watapandishwa kwenda mbinguni, na kuwa kama malaika wa Mungu. Lakini kwa mkazo 
zaidi wapo wale wanaofanya agano na mauti na mapatano na kuzimu, wanaozikataa
kweli ambazo Mbingu imezitoa kuwa kinga kwa wenye haki katika siku ile ya taabu, nao 
wanakubali kujificha chini ya uongo [mafundisho potofu] uliotolewa na Shetani badala
yake [ile kweli] ----- yaani, madanganyo ya uongo ya Imani ya Mizimu.
 
 Jambo la kushangaza mno lisiloneneka ni UPOFU wa watu wa kizazi hiki. Maelfu
wanalikataa Neno la Mungu kuwa halifai kusadikiwa na kwa ujasiri uliojaa shauku kuu 
wanayapokea madanganyo ya Shetani. Wenye mashaka na wenye dhihaka
wanaushutumu ushupavu wa dini wa wale wanaoishindania ile imani ya manabii na
mitume, nao wanajifurahisha wenyewe kwa kuyadhihaki maneno mazito ya Maandiko 
yamhusuyo Kristo na Mpango wake wa Wokovu, na kisasi kitakachowajia wale
wanaoikataa kweli yake. Wanajifanya kana kwamba wana huruma nyingi sana kwa watu 
hao [wa Mungu] wenye mawazo finyu, duni na ya ushirikina kwa kuyakubali madai ya
Mungu na kuyatii matakwa ya Sheria yake [Amri Kumi]. Wanaonyesha kuwa wanayo
hakika kana kwamba kweli walikuwa wamefanya agano na mauti na mapatano na 
kuzimu -----  kana kwamba walikuwa wamejenga kuzuizi kisichopitika, kisichoweza
kupenywa kati yao na hasira ya kulipiza kisasi ya Mungu. Hakuna kinachoamsha hofu 
zao. Wamejitoa kikamilifu kwa yule Mjaribu, wamejifungamanisha karibu sana naye, 
nao wamejazwa roho yake kikamilifu, hata hawana nguvu wala mwelekeo wa kujinasua
kutoka katika mtego wake. 

 Kwa muda mrefu Shetani amekuwa akijiandaa kwa jaribio lake la mwisho la 
kuudanganya ulimwengu. Msingi wa kazi yake uliwekwa kwa matumaini aliyompa
Hawa katika Edeni kwamba:  "HAKIKA HAMTAKUFA." "Siku mtakayokula matunda
ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi MTAKUWA KAMA MUNGU, mkijua mema 
na mabaya." Mwanzo 3:4,5. Kidogo kidogo ametayarisha njia ya madanganyo yake ya
kilele kwa kuanzisha IMANI YA MIZIMU. Bado hajafikia kipeo cha hila zake anazotaka 
kuzitekeleza; lakini kitafikiwa katika siku chache za mwisho zitakazobakia. Asema nabii
huyu: "Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura... Hizo ndizo ROHO ZA
MASHETANI, zifanyazo ISHARA [MIUJIZA], zitokazo na kuwaendea WAFALME 
WA ULIMWENGU WOTE kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu
Mwenyezi." Ufunuo 16:13,14. Ulimwengu wote utakumbwa na kuingizwa katika 
udanganyifu huu, isipokuwa wale WATAKAOLINDWA kwa uwezo wa Mungu kwa njia
ya IMANI YAO KATIKA NENO LAKE. Watu kwa upesi sana wanalazwa usingizi
katika tumaini la usalama  utakaowaangamiza, wataamshwa tu kwa ghadhabu ile ya 
Mungu [Mapigo Saba].
 
 Asema Bwana: "Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo
timazi; na mvua ya mawe [Ufunuo 16:17-21] itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno
ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri. Na agano lenu mliloagana na 
mauti, litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo
lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa [mtakapoangamizwa] nalo." Isaya 
28:17,18.

 

 ----- E.G. White, THE TRIUMPH OF GOD'S LOVE, uk.325-331. 

 Can the Dead Speak to Us?
 
 OR, THE GREAT CONTROVERSY, Sura ya 34, uk. 551-562.
 
 Spiritualism.
 

bottom of page