top of page

Gundua

bible-study-lesson-tips-small-group-lead
Ugunguzi.jpg

Miongozo Mbalimbali

bible-png-clipart-12.png

12. MWOKOZI ALIYEPO DAIMA

Kijana mmoja wa Kiskoti, kwa jina Petro, alipopotea katika nyika yenye majani mengi usiku mmoja uliokuwa na giza jeusi kama wino, Mungu alimwita kwa jina lake: "Petro!" Sauti ile ya mbinguni ilipoita tena, Petro alisimama katika njia yake, akaangalia chini na kugundua kwamba alikuwa umbali wa hatua moja tu kutumbukia katika shimo la machimbo ya mawe lililokuwa limeachwa.

Je! isingekuwa ni ajabu kwetu sisi kama tungeweza kumsikia Mungu akituita kwa majina yetu? Je! yasingekuwa makubwa kwetu endapo yeye angekuwa rafiki yetu aliye karibu sana nasi-endapo tungeweza kukaa pamoja naye kabisa na kuongea naye kwa muda mrefu juu ya mapambano yetu tuliyo nayo pamoja na zile ndoto zetu?

1. Kwenda Kwa Yesu Bila Kizuizi

Amini usiamini, sisi tunaweza kwenda karibu sana na Yesu sasa kuliko vile ambavyo tungeweza endapo Yeye angeishi kabisa hapa pamoja nasi akiwa ni mtu anayeonekana kwa macho. Kuwa na Yesu kimwili katika mji wetu kwa kweli lingekuwa ni jambo la ajabu, lakini hebu fikiria juu ya yale makundi makubwa sana yatakayomsonga ili yapate kumwona kwa karibu zaidi. Fikiria juu ya muda wake mwingi ambao ungetakiwa kutumika. Lingekuwa ni jambo jema kuweza kupata dakika chache za kuongea naye ana kwa ana katika kipindi chote cha maisha yetu.

Kristo anapenda kujenga uhusiano wake na kila mmoja wetu. Hii ndiyo sababu moja iliyomfanya aondoke duniani humu ili kwenda mbinguni kufanya huduma ya pekee ambayo ingemwezesha kuja karibu na kila mmoja wetu kila siku. Kwa sababu Yesu hajafungwa mahali pamoja kama alivyokuwa alipokuwa hapa duniani, yeye kwa njia ya Roho Mtakatifu sasa yuko tayari kuweza kuyaongoza maisha ya kila mtu mmoja mmoja atakaye.

Je, ni ahadi gani ya kutia moyo aliyoitoa Yesu kabla hajapaa juu kwenda mbinguni?
"NAMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE naam, mpaka mwisho wa nyakati." - (Mathayo 28:20).

Je, Kristo anafanya kazi gani kule mbinguni ambayo inafanya uwezekano uwepo kwa yeye kuwa "pamoja nanyi siku zote?"
"Basi, tuzingatie kwa makini imani tunayoungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka mbinguni; Yesu, Mwana wa Mungu. Huyu Mkuu wetu anaelewa kabisa unyonge wetu; yeye mwenyewe alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida " - (Waebrania 4:14-16).

Zingatia ahadi hizi zinazotolewa kwetu tunapokuwa na Yesu kama mwakilishi wetu kila mmoja binafsi kule mbinguni: "Alijaribiwa kama sisi kwa kila namna." "Kutuhurumia sisi katika udhaifu wetu." "Kutusaidia wakati wa shida." Tukiwa na Yesu kama Kuhani wetu Mkuu hatuendelei tena kutanga mbali na mbingu iliyo mbali sana. Kristo anaweza kutukaribisha sisi kuingia kabisa mbele zake Mungu. Si ajabu, basi, kwamba tunaombwa sana tu "kikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema"

Je, Yesu anakaa mahali gani kule mbinguni?
"Lakini Kristo alitoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi milele dhabihu ifaayo kisha akaketi UPANDE KULIA WA MUNGU" - (Waebrania 10:12).

Kristo aliye hai-mmoja anayetuelewa sisi-ni mwakilishi wetu kila mmoja binafsi katika kiti kile cha enzi "mkono wa kuume wa Mungu."

Ni kwa jinsi gani maisha ya Yesu yalimwandaa kuwa Kuhani wetu?
"Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake wa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa" - (Waebrania 2:17,18).

"Ndugu" yetu aliyeshiriki katika ubinadamu wetu, na ambaye "alijaribiwa" kama sisi tunavyojaribiwa, hivi sasa yeye ni Kuhani wetu Mkuu ameketi upande wa kulia wa Mungu, "Alifanywa kama" sisi, anajua yale tunayoyapitia. Amepata kuwa na njaa, kiu, majaribu, na kuchoka sana kiasi cha kuishiwa nguvu. Alijisikia kwamba alikuwa na haja ya kuhurumiwa na kueweleka.

Lakini zaidi ya hayo yote, Yesu anazo sifa za kuwa Kuhani wetu Mkuu kwa sababu yeye alikufa ili "kufanya upatanisho" kwa ajili ya dhambi zetu. Alilipa gharama yote ya dhambi zetu kwa kufa badala yetu sisi. Hii ndiyo Injili, yaani, Habari Njema kwa wanadamu wote kila mahali na kwa wakati wote.

Mmojawapo wa Wakurugenzi wa Shule yetu ya Biblia anatusimulia kisa hiki kilichompata akisema "Binti yetu mdogo kabisa alipokuwa na umri wa miaka mitatu, alijibana kidole chake katika kiti cha kukunjwa, na kuuvunjavunja mfupa wake. Tulipomkimbiza kumpeleka kwa daktari, kilio chake kikali kutokana na maumivu yake kiliturarua kweli mioyo yetu. Tena kikamgusa mtoto wetu wa miaka mitano kwa njia ya pekee. Sitaweza kusahau maneno yake aliyosema baada ya daktari kumshughulikia dada yake aliyejeruhiwa. Binti yule akalia kwa kwikwi, na kusema, 'Baba, natamani kingekuwa ni kidole changu mimi!"

Wanadamu wote waliposetwa na dhambi na kuhukumiwa kufa milele, Yesu alisema, "Baba, natamani ningekuwa mimi." Naye baba akampa Yesu kile alichotamani pale msalabani. Mwokozi wetu amepitia kila aina ya maumivu makali ambayo kwayo sisi tuliteseka - na zaidi ya hayo!

2. Injili Katika Agano La Kale

Wana wa Israeli walipopiga kambi yao chini ya Mlima Sinai, Mungu alimwagiza Musa kujenga patakatifu ambapo paliweza kusafirishwa toka mahali hata mahali kwa ajili ya ibada "kama mfano wake, ulioonyeshwa [kwako Musa] mlimani "(Kutoka 25:40). Karibu miaka 500 baadaye, Hekalu kuu la mawe la mfalme Sulemani lilijengwa ili kuchukua mahali pa hema takatifu lililokuwa likichukuliwa huku na huku. Na hekalu lile lililjengwa kwa mfano ule ule kabisa kama lilivyojengwa hema takatifu lililokuwa linachukuliwa huku na huku.

3. Huduma Ya Yesu Kwetu Imefunuliwa Katika Patakatifu

Patakatifu na huduma zake hufunua kile anachofanya Yesu sasa katika hekalu la mbinguni, na anachofanya sasa hapa duniani ili kututayarisha na kutuongoza kila mmoja wetu katika maisha yetu ya kila siku.

Kwa kuwa patakatifu pale pa duniani palijengwa kwa mfano wa hekalu la mbinguni, basi, panaakisi patakatifu pa mbinguni ambako Kristo anahudumu sasa. Kutoka 25-40 huelezea habari za huduma ile na taratibu zake za kafara ya patakatifu pale pa jangwani kwa kinagaubaga sana. Muhtasari mfupi wa vyombo vya patakatifu huonekana katika Agano Jipya:

"Agano la kwanza lilikuwa na kawaida taratibu zake za ibada na maskani takatifu ya duniani. Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje ilitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu. Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa hema iliyoitwa Mahali Patakatifu sana. Humo mlikuwa na madhabahu ya dhambi kwa ajili ya kufukizia ubani, na sanduku la agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana, fimbo ya Aroni ilikuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano. Juu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo " - (Waebrania 9:1-5).

Hema hilo takatifu lilikuwa na vyumba viwili, yaani, Patakatifu, na Patakatifu pa Patakatifu. Ua uliwekwa mbele ya pataktifu. Katika ua ule ilisimama madhabahu ya shaba nyeupe ambayo juu yake makuhani walitoa dhabihu zao, na birika la maji walimonawa.

Dhabihu zilizotolewa juu ya madhabahu ile ya shaba nyeupe zilikuwa mfano wa Yesu, ambaye, kwa njia ya kifo chake msalabani alikuwa ndiye yule "Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! (Yohana 1:29). Mwenye dhambi aliyetubu alipokuja na dhabihu yake kwenye madhabahu ile na kuziungama dhambi zake, alipokea msamaha na utakaso. Vile vile mwenye dhambi leo anapata msamaha na utakaso kwa njia ya damu yake Yesu (1 Yohana 1:9).

Katika chumba kile cha kwanza, au Patakatifu, kile kinara cha taa saba kiliwaka daima, kikimwakilisha Yesu ambaye ni "Nuru ya ulimwengu" inayowaka daima (Yohana 8:12). Meza ya mikate iliyowekwa wakfu ilimwakilisha yeye ambaye ni "Mkate wa Uzima" ambaye daima yupo kukidhi njaa yetu ya kimwili na kiroho (Yohana 6:35). Ile madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba iliwakilisha huduma ya Yesu ya uombezi anayofanya kwa ajili yetu mbele za Mungu (Ufunuo 8:3,4).

Chumba cha pili, au Patakatifu pa Patakatifu, palikuwa na sanduku la agano lililofunikwa na dhahabu pande zote. Liliwakilisha kiti cha enzi cha Mungu. Kifuniko chake cha upatanisho, au kiti cha Rehema, kiliwakilisha uombezi wa Kristo, Kuhani wetu Mkuu, akiwaombea wanadamu wenye dhambi ambao wameivunja sheria ya Mungu ya Maadili [Amri Kuu]. zile mbao mbili za mawe ambazo juu yake Mungu aliandika Amri Kumi zilihifadhiwa chini ya kile kiti cha rehema. Makerubi wale wawili wa dhahabu wenye utukufu waliinamia kile kiti cha rehema kutoka katika kila mwisho wa lile sanduku. Nuru tukufu iliangaza katikati ya wale makerubi wawili, hiyo ikiwa ni ishara ya kuwako kwake Mungu mwenyewe.

Pazia lilipaficha pale Patakatifu ili pasionekane na watu wakati makuhani walipokuwa wakiwahudumia katika ule ua. Pazia la pili mbele ya Patakatifu pa Patakatifu lilikikinga kile chumba cha ndani kisionekane na makuhani walioingia katika chumba kile cha kwanza cha Patakatifu.

Yesu alipokufa pale msalabani, je, ni kitu gani kilitokea kwa pazia lile?
"Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini" - (Mathayo 27:51).

Patakatifu pa Patakatifu paliachwa wazi Yesu alipokufa. Baada ya kifo cha Yesu, hakuna pazia liwalo lote lote liwezalo kuwepo kati ya Mungu Mtakatifu na muumini aliye mnyofu wa moyo; Yesu, Kuhani wetu Mkuu, anatukaribisha na kutuingiza kabisa mbele za Mungu (Waebrania 10:19-22). Tunayo njia ya kukifikia chumba kile ambamo kimo kiti cha enzi cha Mungu kwa kuwa Yesu ni Kuhani wetu Mkuu aliye mkono wa kulia wa Mungu. Yesu ndiye anayetuwezesha sisi kuja mbele za Mungu - yaani, hadi ndani ya ule moyo wa upendo wa Baba. Basi "na tukaribie."

4. Ufunuo Wa Kristo Akifa Kutuokoa

Kama palivyotumika pale patakatifu pa kidunia kama mfano mdogo kabisa wa hekalu lile la mbinguni ambako Yesu anahudumu sasa kwa ajili yetu, huduma zile zilizoendeshwa katika patakatifu pale pa kidunia zilikuwa "mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni" (Waebrani 8:5). Lakini ipo tofauti dhahiri ambayo inajitokeza: mkuhani wale waliohudumu katika hekalu la duniani wenyewe walikuwa hawana uwezo wa kusamehe walikuwa hawana uwezo wa kusamehe dhambi, lakini pale msalabani Yesu "alitokea mara moja tu katika utimilifu wa nyakati zile ili aziondolee mbali dhambi kwa kujitoa dhabihu yeye mwenyewe" (Waebrania 9:26).

Kitabu kile cha Mambo ya Walawi cha Agano la Kale kinaeleza kwa undani sana huduma zile zilizoendelea kufanywa katika patakatifu pale. Taratibu zile za ibada ya dhabihu ziligawanywa katika sehemu mbili: huduma za kila siku na huduma za kila mwaka. (Mwongozo 13 unazishughulikia huduma zile za kila mwaka).

Katika zile huduma za kila siku makuhani wale waliotoa dhabihu kwa ajili ya mtu mmoja binafsi na kwa ajili ya mkutano mzima. Mtu ye yote alipotenda dhambi, alitakiwa kuleta mnyama asiye na waa lolote kama sadaka yake ya dhambi, 'a[li]weka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja kuwa sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka za kuteketezwa" (Mambo ya Walawi 4:29). Hatia ya mwenye dhambi yule ilipaswa kuhamishiwa kwa mnyama yule asiye na hatia kwa njia ya maungamo ya dhambi na kuweka mikono juu ya kichwa cha mnyama yule. Jambo hilo lilikuwa mfano wa Kristo akiwa amebeba hatia yetu pale Kalvari; yule mmoja asiye na dhambi alifanywa kuwa "dhambi kwa ajili yetu" (2 Wakorintho 5:21). yule mnyama wa dhabihu alipaswa kuuawa na damu yake kumwagwa kwa sababu ilisonda kidole chake mbele kwenye ile adhabu kuu kuliko zote ambayo kwayo Kristo aliteswa vibaya pale msalabani.

5. Kwa Nini Damu?

"Pasipo kumwaga damu hakuna msamaha" (Waebrania 9:22). Kile kilichotokea katika patakatifu pale pa Agano la Kale kilisonda kidole chake mbele kwenye tendo lile moja kuu la wokovu alilolitenda Kristo. Baada ya yeye kufa kwa ajili ya dhambi zetu, "aliiingia patakatifu pale pawili mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, baada ya kupata ule ukombozi wa milele" kwa ajili yetu (fungu la 12). Damu ya Yesu ilipomwagika pale msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, "pazia lile la hekalu [kule Yerusalemu] lilipasuka vipande viwili toka juu mpaka chini" (Mathayo 27:51). Kwa sababu ya ile kafara aliyoitoa Yesu pale msalabani, hapakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu zile za wanyama.

Yesu alipomwaga damu yake kutoka katika msalaba ule, alikuwa anatoa sadaka ya maisha yake makamilifu ya utii kuwa badala ya kushindwa kwetu kwingi. Baba na Mwana walipotenganishwa kwa nguvu pale Kalvari, Baba aligeuka na kuangalia kwingine kwa utungu na Mwanawe alikufa kutokana na moyo wake uliopasuka. Mungu Mwana aliingia katika historia yetu na kuchukua mwilini mwake athari kamili za dhambi zetu na kuonyesha wazi jinsi utendaji wa mabaya unavyoleta maafa ya kusikitisha kweli kweli. Hapo ndipo angeweza kuwasamehe wenye dhambi bila ya kuihafifisha dhambi. Kristo alifanya "amani kwa damu yake iliyomwagika pale msalabani" (Wakolosai 1:20).

6. Ufunuo Wa Yesu Akiishi Kutuokoa

Je! ni kazi gani anayofanya Yesu siku-kwa-siku katika hekalu lile la mbinguni?
"Naye kwa sababu hii aweza kuwaokoa kabisa wale wanaokuja kwa Mungu kupitia kwake, kwa sababu YU HAI SIKU ZOTE ILI AWAOMBEE" - (Waebrania 7:25).

Yesu sasa "yu hai' ili kutoa damu yake, yaani, kafara yake, kwa ajili yetu. Sasa yeye anafanya kazi kwa bidii nyingi ili kumwokoa kila mwanadamu kutoka katika dhambi iletayo mauti. Wengine kwa kuelewa vibaya wanadhani kwamba Yesu, akiwa kama Mwombezi wetu, yuko kule mbinguni kwa madhumuni ya kumsihi sana Mungu ambaye hataki ili atusamehe sisi. Kwa kweli ni Mungu anayeikubali kwa furaha kubwa kafara ile aliyoitoa Mwanawe kwa ajili yetu.

Kama Kuhani wetu Mkuu, Kristo pia anawasihi sana wanadamu. Yeye anafanya kazi yake ili kuwasaidia wale ambao hawajali kitu ili waiangalie kwa mara ya pili ile neema yake, anawasaidia wenye dhambi ambao wanakata tamaa ili walishikilie sana tumaini lao linalopatikana katika injili, na kuwasaidia katika waumini kupata utajiri mwingi zaidi katika maombi yao. Yesu anayatengeneza maisha yetu ili yapatane na amri [Kumi] za Mungu na kutusaidia kuzikuza tabia zetu ambazo zitaweza kustahimili lile jaribio la wakati.

Mungu aliyatoa maisha yake na kufa kwa ajili ya kila mwanadamu aliyepata kuishi katika dunia hii. Na sasa, yeye akiwa Kuhani Mkuu au Mpatanishi, "yu hai siku zote" ili kuwaongoza watu wakikubali kifo chake kwa ajili ya dhambi zao. Wanadamu hawatapotea kwa kuwa wao ni wenye dhambi, bali kwa sababu wanakataa kupokea msamaha ambao Yesu anawapa.

Dhambi iliharibu uhusiano wa karibu sana ambao Adamu na Hawa walifurahia kuwa nao pamoja na Mungu. Lakini Yesu, kama Mwana-Kondoo wa Mungu, alikufa ili kuwaweka huru wanadamu wote mbali na dhambi na kuwarudishia tena urafiki ule uliopotea. Je! hivi wewe umemgundua yeye kuwa ni Kuhani wako Mkuu, Mmoja aliye hai siku zote ili apate kuudumisha uhusiano huo uwe wa karibu na wa kusisimua sana?

Kifo chake Kristo kilichotolewa kama sadaka ya dhambi ni cha pekee kabisa. Huduma yake Kristo kule mbinguni haina kifani. Ni Kristo peke yake anayemleta Mungu karibu sana kando yetu. Ni Kristo peke yake anayefanya uwezekano uwepo kwa Roho wa Mungu kuweza kukaa kabisa ndani ya mioyo yetu. Alijitoa kabisa yeye mwenyewe ili kutufanya sisi tutimike. Anastahili vile vile tujitoe wakfu kwake kama yeye alivyojitoa. Hebu na tumpokee kabisa kama Mwokozi na Bwana wa maisha yetu.

bottom of page