top of page

Gundua

bible-study-lesson-tips-small-group-lead
Ugunguzi.jpg

Miongozo Mbalimbali

bible-png-clipart-12.png

1. TWAWEZA KUMWAMINI MUNGU

Siku moja Jimi alimwuliza mtu mmoja anayekana kuwa kuna Mungu endapo alipata kujaribu sana, hata kwa dakika chache tu, kupigana na wazo lisemalo kwamba huenda Mungu yuko.

"Sawa kabisa!" mkana Mungu yule akajibu, akimwacha Jimi na mshangao. "Miaka mingi iliyopita, mimi nilikuwa karibu sana nigeuke na kuwa mtu anayemwamini Mungu. Nilipokiangalia kile kiumbe kidogo sana - lakini - kikamilifu katika kitanda chake kidogo, nilipochungulia na kuviona vidole vile vidogo fahamu za kwanza za kutambua, nilipita katika kipindi cha miezi kadhaa ambayo katika hiyo mimi nilikuwa karibu kabisa niache kuwa mkana Mungu. Kule kumwangalia mtoto yule kulikuwa kumenishawishi karibu kabisa kuwa hapana budi Mungu alikuwa yuko."

1. Kila Kitu Kilichobuniwa Kina Mbunifu Wake

Muundo wa mwili wa kibinadamu unafanya iwepo haja ya kuwako mbunifu wake. Wanasayansi wanatuambia kwamba ubongo wetu hukusanya na kukumbuka picha elfu nyingi katika mawazo yetu, huyaunganisha matatizo yetu yote na kuyatatua, hufurahia kuona uzuri, huitambua nafasi ya mtu, na kutaka kukuza yaliyo bora ndani ya kila mtu. Chaji za umeme zitokazo katika ubongo huongoza shughuli zote za misuli ya miili yetu.

Kompyuta pia zinafanya kazi kwa njia ya mikondo ya umeme. Lakini ilichukua akili ya mwanadamu katika kuitengeneza hiyo kompyuta na kuiambia la kufanya.

Si ajabu, basi, kwamba mtunzi wa Zaburi alihitimisha kwa kusema kwamba mwili wa mwanadamu unasimulia habari za Muumbaji huyo wa ajabu kwa sauti kubwa iliyo wazi:
"Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu, wewe wanijua kabisa kabisa" - (Zaburi 139:14)

Hatuna haja ya kwenda mbali ili kuyaona hayo "matendo" ya Mungu. Umbo la ubongo wetu wenye sehemu nyingi za ajabu na viungo vyetu vingine ni "matendo" ya Mungu, nayo husonda kidole chake kwa yule mbunifu stadi kabisa.

Hakuna pampu yoyote iliyotengenezwa na mwanadamu inayoweza kulinganishwa na moyo wa mwanadamu. Hakuna mtandao wo wote wa kompyuta uwezao kuwa sawa na mfumo wetu wa mishipa ya fahamu. Hakuna mfumo wo wote wa Televisheni unaofanya kazi yake vizuri kama sauti, sikio, na jicho la mwanadamu. Hakuna kiyoyozi kikuu cho chote (central air conditioning) wala mfumo wa kuipasha joto nyumba uwezao kushindana na kazi inayofanywa na pua, mapafu, na ngozi yetu. Mfumo wenye sehemu nyingi za ajabu wa mwili wa mwanadamu unadokeza kwamba mtu fulani alihusika katika kuubuni, na Mtu huyo fulani ni Mungu.

 

Mwili wa mwanadamu ni mfumo kamili wa viungo mbali mbali - vyote vikiwa vinashirikiana, vyote vikiwa vimeumbwa kikamifu. Mapafu na moyo, mishipa ya fahamu na misuli, hiyo yote hufanya kazi za ajabu mno kiasi cha kuwa vigumu kusadikika ambazo hutegemezwa juu ya kazi nyingine zilizo za ajabu mno kiasi cha kutufanya sisi tushindwe kusadiki.

Endapo ungetakiwa kuzipa nambari sarafu kumi kuanzia moja mpaka kumi, na kuziweka mfukoni mwako, na kuzitikisa-tikisa huku na huku, kisha kuzitoa mfukoni mwako na kuziweka tena mfukoni moja moja, je, kuna uwezekano gani kwamba ungefanya hivyo kwa kufuata mfuatano wa nambari zake sawa sawa? Kwa sheria ya mahesabu unayo bahati moja tu katika bilioni kumi ya kuzitoa kwa mpangilio wake kuanzia ya kwanza mpaka ile ya kumi.

 

Sasa, basi, hebu fikiria ni bahati ngapi tumbo la chakula, ubongo, moyo, ini, arteri, vena, figo, masikio, macho, na meno vingekuwa nazo vikikua vyote pamoja na kuanza kufanya kazi yao kwa dakika ile ile ya wakati mmoja.

 

Hivi maelezo ya busara kabisa ni yapi kuhusu ubunifu huo wa mwili wa mwanadamu?

"Kisha Mungu akasema, 'Natumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu,'..............Hivyo Mungu Akamwuumba Mtu Kwa Mfano Wake,...... mwanamume na mwanamke aliwaumba" - (Mwanzo 1:26,27).

Mwanaume na mwanamke wa kwanza wasingeweza kuwa wametokea wenyewe tu. Biblia inathibisha kwamba Mungu alitubuni sisi kwa mfano wake. Alituwaza katika mawazo yake na kutuumba.

 

2. Kila Kitu Kilichoumbwa Kina Muumbaji Wake

Lakini ushahidi wa kuwako kwake Mungu haufungamani tu na ubunifu wa miili yetu; pia umetandaa huko mbinguni. Acha taa za mjini, angalia juu katika mbingu ya usiku. Wingu lile jeupe kama maziwa lenye nyota, tunaloliita Mkanda wa Nuru (Milky Way) ambalo kwa kweli ni kundi la mabilioni ya majua (galaxy) yanayotoa mwanga mkali wa moto sawa na ule wa jua letu ambao unaweza kuonekana hapa duniani kwa kupitia katika darubini kubwa zilizopo hapa duniani kama ile darubini iitwayo "Hubble Telescope" iliyo katika anga za juu.

Si ajabu, basi, kwamba mtunga Zaburi alihitimisha kwa kusema kwamba nyota zinamtangaza Muumbaji Mtukufu:
"Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu, anga ladhihirisha kazi ya mikono yake" (Zaburi 19:1-3).

 

Je, hivi sisi twaweza kutoa hitimisho gani la busara kwa kuangalia mpangilio huo unaotatanisha sana na ukubwa wa malimwengu yote?

"Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi" (Mwanzo 1:1).

"Yeye [Mungu] alikuwako kabla ya vitu vyote; vyote hudumu mahali pale kwa uwezo wake" (Wakolosai 1:17).

 

Viumbe vyote humshuhudia yule Mungu Mbunifu Mkuu na Muumbaji asiye na Mwisho. Katika maneno haya rahisi, "Hapo mwanzo Mungu," tunalipata jibu la siri ile ya uhai. Yuko Mungu aliyeumba kila kitu.

Wanasayansi wakuu wengi siku hizi wanamwamini Mungu. Dk. Arthur Compton, mwanafizikia mshindi wa tuzo ya Nobel, akitoa maoni yake juu ya fungu hilo la Maandiko, siku moja alisema hivi:
"Kwangu binafsi, imani huanza ninapotambua kwamba yule aliye na akili isiyo na kifani ndiye aliyeyaweka hayo malimwengu na kumwumba mwanadamu. Kwangu mimi si vigumu kuwa na imani hii, kwa maana ni dhahiri kwamba po pote pale palipo na mpango yupo Mungu mwenye akili. Malimwengu yaendayo kwa utaratibu, na kujifunua kwetu hushuhudia ukweli wa usemi huu adimu mno uliopata kunenwa - 'Hapo mwanzo Mungu'"

Biblia haijaribu kumthibitisha Mungu inatangaza kuwako kwake. Dk. Arthur Conklin, mwana biolojia, siku moja aliandika hivi: "uwezekano kwa uhai kutokea kwa ajali ni sawa na uwezekano kwa kamusi kamili kutokea kutokana na mlipuko katika kiwanda cha kuchapisha vitabu".

 

Twajua kwamba wanadamu hawawezi kutengeneza kitu cho chote bila kutumia kitu kingine. Twaweza kujenga vitu, kuvumbua vitu, kuunganisha vitu, lakini kamwe hatujapata kufanya kitu cho chote bila kuwa na kitu kingine cha kuanzia, awe ni chura mdogo kabisa ua la kawaida kabisa. Vitu vituzungukavyo pande zote hupiga kelele vikisema Mungu ndiye aliyevibuni, Mungu ndiye aliyeviumba, Mungu ndiye anayevitegemeza. Jibu pekee linaloaminika kuhusu chimbuko la malimwengu hayo, dunia hii, na wanadamu - ni Mungu.

 

3. Mungu Huingia Katika Mahusiano Na Watu Binafsi

Mungu yule aliyezibuni mbingu hizo na nyota, aliyeyaumba malimwengu hayo, anatafuta kuwa na uhusiano nasi binafsi. Alikuwa na uhusiano wake binafsi na Musa: "Bwana akasema na Musa....kama vile mtu asemavyo na rafiki yake" (Kutoka 33:11). Mungu Mwenyewe anataka kuingia katika uhusiano nawe na kuwa Rafiki yako. Yesu aliwaahidi wale wanaomfuata, akisema "Ninyi mmekuwa rafiki zangu" (Yohana 15:14).

Sisi sote tumeshughulika sana na wazo hilo la Mungu, kwa kuwa wanadamu kwa asili wanapenda dini. Hakuna mnyama yeyote ajengaye madhabahu kwa ajili ya ibada. Lakini kila mahali unapowakuta wanaume na wanawake, unawakuta wakiabudu. Ndani ya kila moyo wa mwanadamu kuna ufahamu kuwa Mungu yuko, tamaa ya kuwa rafiki wa Mungu. Tunapoitikia hiyo tamaa yetu na kumpata Mungu, hatuwi na mashaka tena juu ya kuwako kwake na hitaji letu.

Katika miaka ile ya 1990 mamilioni ya wanaomkana Mungu katika nchi ya Urusi waliachana na imani yao hiyo ya kumkana Mungu, kisha wakamgeukia Mungu. Profesa wa Chuo Kikuu cha St. Petersburg alitoa kauli yake inayofanana na maoni yaliyotolewa na wakana Mungu wengi katika Umoja wa Kisovieti iliyopita:
"Nimetafuta maana ya maisha katika utafiti wangu wa kisayansi, lakini sikuona kitu chochote cha kutegemea. Wanasayansi wanaonizunguka mimi wanazo hisia hizo hizo za ukiwa. Nilipoangalia ukubwa wa malimwengu katika somo langu la elimu ya nyota, kisha nikaangalia ukiwa uliomo moyoni mwangu, niliona kwamba ni lazima pawe na maana fulani. Kisha nilipoipokea Biblia uliyonipa na kuanza kuisoma, ukiwa katika maisha yangu ukajazwa. Nimeiona Biblia kuwa ndiyo chimbuko la pekee la matumaini kwa nafsi yangu. Nimempokea Yesu kama Mwokozi wangu, nami nimepata amani ya kweli pamoja na kuridhika katika maisha yangu".


Mkristo anamwamini Mungu kwa sababu yeye amekutana naye na kugundua kwamba anayatosheleza mahitaji makubwa sana ya moyo wake. Mungu ambaye Wakristo wamemuona kuwa yuko, anatupatia mtazamo mpya, maana mpya, makusudi mapya na furaha mpya.

 

Mungu hatuahidi sisi kwamba tutakuwa na maisha yasiyo na taabu, wala mapambano, ila yeye anatuhakikishia kwamba atatuongoza na kutusaidia kama tutakuwa na uhusiano binafsi naye. Na mamilioni ya Wakristo wanaweza kutoa ushuhuda wao kwamba ingekuwa heri kwao kuacha kila kitu kuliko kuyarudia maisha yale yasiyokuwa na Mungu.

Hii ndiyo ajabu kuu kuliko zote kwamba yule Mungu Mwenyezi aliyeyabuni, aliyeyaumba na kuyategemeza malimwengu hayo anataka kufanya uhusiano na kila mwanaume na mwanamke, kila mvulana na msichana. Daudi alishangaa sana kuhusu jambo hilo alipoandika maneno haya:
"Nikiangalia mbingu, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizozimika huko, mtu ni nini ee Mungu hata umfikirie mwanadamu ni nini hata umjali?" - (Zaburi 8:3,4).

Muumbaji wetu ana "mjali" kila mmoja wetu. Yeye binafsi anakupenda sana wewe kana kwamba wewe ulikuwa ni kiumbe chake cha pekee alichokiumba.

 

Basi tunaweza kumwamini Mungu:
(1) Kwa sababu ya ubunifu wake wenye sehemu nyingi katika kila kitu alichokiumba ambacho kinatuzunguka sisi.
(2) Kwa sababu shauku ile iliyomo ndani yetu juu ya Mungu inatufanya tusiwe na raha mpaka tupatapo pumziko letu ndani yake tena.
(3) Kwa sababu tunapomtafuta na kumpata, Mungu hutosheleza kila haja tuliyo nayo pamoja na shauku yetu - kikamilifu!

 

4. Ni Mungu Wa Aina Gani?

Ni jambo la busara tu kwamba Mungu aliye na nafsi yake apende kujifunua mwenyewe kwa viumbe wake kama vile baba atakavyo watoto wake wamjue. Na katika Biblia Mungu anatuambia yeye ni nani, tena anafananaje.

Ni mfano gani alioutumia Mungu katika kuwaumba wanaume na wanawake?

"Hivyo Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba" (Mwanzo 1:27).

Kwa kuwa sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, basi, uwezo wetu wa kufikiri na kujisikia, kukumbuka na kutumaini, kutafakari na kuchambua mambo - chimbuko lake lote latoka kwake. Je, tabia kuu ya Mungu ni ipi?

"Mungu ni upendo" (1 Yohana 4:8).

 

Mungu hufanya uhusiano wake na wanadamu kutokana na moyo wake wa upendo. Hakuna kitu cho chote alichofanya au atakachopata kufanya ambacho hakijasababishwa na upendo wake usio na ubinafsi, ujitoao mhanga.

 

5. Jinsi Yesu Anavyotufunulia Alivyo Mungu

Katika Biblia Mungu anarudia tena na tena kueleza habari zake Mwenyewe kwamba Yeye ni Baba.

"Je! Sisi sote si watoto wa baba mmoja"?
"Je, sisi sote hatukuumbwa na Mungu yule yule?" Malaki 2:10.

Baadhi ya mababa tuwaonao leo si cho chote, bali hawapendezi. Kuna mababa wasiojali, mababa wanaotukana matusi. Mungu si kama hao. Yeye anajali, ni Baba anayeguswa sana na mambo yetu. Ni Baba apendaye kucheza na mwanawe au binti yake, ni Baba anayewafurahisha sana watoto wake kwa kuwasimulia hadithi kabla hawajaenda kulala usiku.

 

Baba yetu huyo mwenye upendo alitaka kufanya zaidi ya kule kujifunua Mwenyewe kwa njia ya maneno ya Maandiko. Alijua kwamba yule mtu tunayeishi naye ni mtu halisi kuliko yule tunayesikia tu habari zake au tunayesoma habari zake. Kwa hiyo yeye akaja katika dunia yetu kama mtu halisi - yaani, yule mtu Yesu.

"Kristo mfano wa Mungu asiyeonekana" - (Wakolosai 1:15).

 

Basi kama wewe umemwona Yesu, utakuwa umemwona Mungu. Alijishusha hadhi yake na kuwa sawa sawa na sisi akawa kama sisi - ili apate kutufundisha jinsi ya kuishi na kuwa na furaha, ili kwamba sisi tupate kuona jinsi Mungu alivyo hasa. Yesu ni Mungu aliyeonekana kwa macho. Yeye mwenyewe alisema, "Aliyeniona mimi amemwona Baba" (Yohana 14:9).

Usomapo kisa cha Yesu katika vitabu vinne vya Injili, yaani, vitabu vinne vya kwanza vya Agano Jipya, utagundua picha ya kuvutia sana ya Baba yetu aliye mbinguni. Wavuvi wale wa kawaida tu walizitupa nyavu zao ili kumfuata Yesu, na watoto wadogo wakasongamana kwenda kwake kupokea baraka zake. Aliweza, kumfariji mwenye dhambi aliyeharibika kabisa na kuzivunja nguvu za mnafiki sugu aliyejihesabia haki yeye mwenyewe. Aliponya kila maradhi kuanzia upofu hadi ukoma.

 

Katika matendo yake yote Yesu alidhihirisha kwamba Mungu ni upendo! Alikidhi haja ya mwanadamu kwa namna ambayo hakuna mtu ye yote aliyepata kufanya hivyo kabla yake au tangu wakati wake! Ufunuo wa Yesu wa mwisho ambao unaonyesha utukufu wa jinsi Mungu alivyo ulitokea pale msalabani.

"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele" - (Yohana 3:16).

Yesu alikufa sio tu kutupatia maisha yenye furaha sasa, bali kutupa uzima wa milele pia. Kwa vipindi virefu watu walishangaa, na kutumaini, na kuota
ndoto juu ya Mungu. Waliiona kazi ya mikono yake mbinguni na katika uzuri wa viumbe vya asili. Kisha pale msalabani, Yesu alikivunjilia mbali kimya cha vizazi vingi, na watu wakajikuta wanautazama ana kwa ana uso wa Mungu, wakimwona yeye kama alivyo hasa - yeye ni upendo, wa milele, tena ni upendo udumuo milele!

Wewe waweza kumgundua Mungu sasa hivi Yesu anapomfunua kwako. Ugunduzi huo utakufanya utoe uthibitisho wako binafsi, ukisema: "Baba, nakupenda!"

                                          -------------------------------------------------

bottom of page