14. Kunena Kwa Lugha
iku moja nilipokuwa nikisafri katika basi, niliingia katika mazungumzo na mtu aliyekuwa amekaa kando yangu. Alipohisi kuwa mimi ni Mkristo aliniuliza,
“Je, wewe ni Mkristo?”
“Ndiyo.”
“Je, umejazwa na Roho?”
“Ndiyo, vinginevyo nisingekuwa Mkristo wa kweli.”
“Nina maana kuwa unanena kwa lugha?”
“Kama hivi, “Ninhage minzi ga kung’wa”
(Nilisema, Nipe maji ya kunywa kwa lugha yangu).
“Sina maana hiyo. Nataka kujua kama unanena kwa lugha isiyojulikana.”
Nikamwuliza, “Ndugu, hivi kweli unaamini kuzungumza lugha isiyojulikana ni ushahidi kuwa umejazwa na Roho Mtakatifu?” Inawezekana wewe pia unaamini hivyo. Lakini Biblia inatufundisha nini juu ya jambo hili muhimu.
1. Je, ni nani anayeshirikiana na Baba na Mwana katika Utatu Mtakatifu?
“Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja.” 1Yoh. 5:8.
2. Je, mtu anazaliwaje mara ya pili?
“Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.” Yn 3:5.
3. Je, Roho Mtakatifu ana kazi gani?
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote niliyowaambia.” Yn 14:26. “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki na hukumu.” Yoh.16:8. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” Yn 16:13,14. “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Mdo. 1:8. “Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” Rum. 14:17.
A. Hufundisha na kututia katika kweli yote. Watu waliojazwa na Roho Mtakatifu wataujua na kuukubali ukweli wa Neno lake.
B. Hutupatia nguvu ya kushuhudia juu ya wokovu wake.
C. Hutupatia haki, amani, na furaha.
D. Hutusadikisha juu ya dhambi, haki na hukumu.
4. Pamoja na hayo, Roho Mtakatifu hutupatia nini?
“Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha.” 1 Kor. 12:7-10.
Roho Mtakatifu hugawa karama kwa watu waliompokea Yesu.
5. Je, waumini wote hupata karama moja tu?
“Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” “Je! wote ni mitume? wote ni manabii? wote ni waalimu? wote wanatenda miujiza? wote wana karama za kuponya wagonjwa? wote wanena kwa lugha? wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.” “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.” 1 Kor. 12:11, 29-31; 13:1-3.
Roho Mtakatifu hugawa karama kwa kila mtu kama apendavyo yeye, lakini hawapatii watu wote karama moja, zinatofautiana.
6. Ni watu gani wanaopokea Roho Mtakatifu?
“Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.” Mdo. 5:32. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.” Yn 14:15,16.
Roho Mtakatifu hutolewa kwa wale wanaomtii Mungu. Yesu huwaombea wapate Roho Mtakatifu wale wampendao na kuzishika amri zake.
7. Je, ni karama ipi ambayo tunatakiwa kuitafuta zaidi?
“Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.” 1 Kor. 14:1.
8. Je, Yesu aliwaahidi nini ili wawe mashahidi wake?
“Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.” Lk. 24:49
Aliwaahidi uwezo toka mbinguni ili waweze kushuhudia.
9. Je, walipokea uwezo huo?
“Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.” “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Mdo. 2:1,4.
Ndiyo! Walijazwa na Roho Mtakatifu na mara wakaanza kunena kwa lugha nyingine. Biblia haisemi lugha mpya. Inasema lugha nyingine.
“Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.” Mdo.2:6
10. Kwa nini Mungu aliwapa uwezo wa kunena kwa Lugha nyingine?
“Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.” “Waparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamflia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu.” Mdo. 2:5,9-11.
Walikuwepo watu wa kabila nyingi na Mungu alitaka kila mtu asikie na kuelewa ujumbe uliokuwa ukitolewa na Mitume. Hatimaye watu hawa wangerudi makwao wakiwa na Habari Njema ya wokovu.
11. Je, watu waliosikiliza walielewa?
“Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.” “Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?” Mdo. 2:6,12.
Kila mmoja alikuwa akiwasikia wakinena kwa lugha yake mwenyewe, matendo makuu ya Mungu. Mdo. 2:11.
12. Je, ni lugha ipi inayofaa kunena kanisani?
“Lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafudhisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.” 1 Kor. 14:19.
Ni afadhali kunena maneno machache yanayoeleweka kuliko elfu yasiyoeleweka.
13. Je, ni watu wangapi wanaruhusiwa kunena katika kusanyiko moja kanisani?
“Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.” 1 Kor. 14:27.
Si zaidi ya watatu, tena wapeane zamu, na ni lazima ifasiriwe ili watu waelewe.
14. Je, hawa watatu wanaweza kunena maneno yasiyoeleweka?
“Lakini na asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa.” 1 Kor. 14:28. “Haya! ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga na wasioamini, je! hawatasema ya kwamba mna wazimu?” 1 Kor. 14:23.
Hairuhusiwi kupiga makelele yasiyoeleweka kanisani! “Anyamaze kanisani!”
15. Lakini sasa, kwa nini watu wananena Lugha kinyume na utaratibu unaoelezwa na Biblia?
“Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.” Ufu. 16:14.
16. Je, nitatofautishaje kati ya roho za mashetani na Roho Mtakatifu?
“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” 1 Yoh. 4:1. “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” Isa. 8:20.
Biblia inasema, “Na roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani, vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu” 1 Kor. 14:32,33.
Roho wa Mungu humwongoza mtu kumpenda Kristo na kuwa mtii kwa amri za Mungu. Kutoshika amri za Mungu ni ushahidi wa wazi kuwa mtu huyo hajajazwa na Roho Mtakatifu. “Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” 1 Yoh. 2:3,4.
Inawezekana umekuwa ukitamani kwa muda mrefu kujazwa na Roho Mtakatifu, ili uweze kupokea karama zake. Yesu ameahidi kukupa Roho huyo kama ukimpenda na kuzishika amri zake (Yn 14:15,16). Kwa njia ya Roho Mtakatifu Yesu anabisha kwenye mlango wa moyo wako (Ufu. 3:20). Anataka kuingia ili akujaze na Roho wa kweli.
Je, utafungua moyo wako sasa ili akubadilishe na kukupa uwezo wa kufanya mapenzi yake?