top of page
Yachunguzeeni.png
Somo-1-Cover-Pic-278x300.png

13. Hekalu La Mungu

Je, umewahi kuona mtu akitia maji kwenye tanki la mafuta la gari lake? Bila shaka ungehisi kuwa ni mwendawazimu. Kila mtu anaponunua kitu cha thamani, iwe gari, redio au televisheni, hupewa kitabu chenye maelezo ya jinsi ya kukitumia chombo chake ili kidumu. Maelezo hayo yameandikwa na watengenezaji wa chombo hicho kwani wao ndio wanaojua jinsi kinavyoweza kudumu zaidi. Mtengenezaji wa Mwili wa Mwanadamu, naye ametoa maelezo juu ya kuutumia na kuutunza ili uweze kudumu. Mwili wa mwanadamu ni chombo chenye thamani kubwa kuliko chombo cho chote kilichowahi kutengenezwa hapa duniani. Kwa hiyo ni muhimu zaidi kuzingatia maelezo ya Mungu aliyeuumba ili uweze kudumu na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Je, Mungu ana maelezo yo yote ya jinsi ya kuutumia na kuutunza mwili wa mwanadamu? Hebu tuyachunguze Maandiko kwa pamoja na tumsikie Mungu mwenyewe anavyosema katika Maandiko yake.

1. Je, kanuni za afya ni sehemu ya dini ya kweli?

“Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.” 3 Yohana 1:2.

Ndiyo. Biblia inayalinganisha mafanikio ya kiafya na mafanikio ya kiroho. Akili ya mwanadamu, hali yake ya kiroho na mwili wake vinahusiana na kutegemeana. Kinapoathirika kimoja, kingine pia huathirika. Miili yetu ikitumiwa vibaya, akili na hali zetu za kiroho haziwezi kuwa kama zilivyokusudiwa na Mungu.

2. Kwa nini Mungu aliwapatia watu wake kanuni za afya?

“BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote,… tuone mema sikuzote ili kutuhifadhi hai.” Kumb. 6:24. “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.” Kut. 23:25.

Mungu alitupatia kanuni za afya kwa kuwa yeye ndiye ajuaye kilicho bora kwa mwili wa mwanadamu.

3. Je, kanuni za Mungu kuhusu afya zinasema lo lote juu ya kula na kunywa?

“Mle kilicho chema.” Isa. 55:2. “Mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” 1 Kor. 10:31.

Ndiyo. Mkristo atakuwa tofauti katika kula na kunywa kwake.

4. Je, Mungu aliwapatia watu wake chakula gani?

“Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu,… na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu.” Mwa. 1:29.

“Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula.” Mwa. 2:16.

Mungu aliwapa watu wake matunda, nafaka na jamii ya kokwa. Mboga ziliongezwa baadaye (Mwa. 3:18).

5. Je, wanyama safi na wasio safi walitakiwa kuingizwa ndani ya safna kwa utaratibu gani?

“Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.” Mwa. 7:2.

Wanyama safi waliingizwa wengi zaidi kwa kuwa Mungu alijua kuwa wangetumika kwa chakula na kafara baada ya mimea yote kuharibiwa na Gharika.

6. Je, baada ya Gharika Mungu aliwaruhusu watu wake kula nyama?

“Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu.” Mwa. 9:3.

7. Ni wanyama gani walioruhusiwa kuliwa?

“Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua,… hao ndio mtakaowala.” Law. 11:3.

Mnyama wa kuliwa lazima awe na sifa mbili:

A. Awe na kwato zilizopasuliwa katikati.

B. Awe mwenye kucheua na kutafuna tena.

k.m. Ngamia hucheua, lakini hana kwato. Wibari hucheua, lakini hana kwato. Sungura hucheua, lakini hana kwato. Nguruwe anazo kwato zilizopasuliwa, lakini hacheui. Hawa ni baadhi ya wanyama najisi na hata mizoga yao ni hatari. Hatupaswi kuigusa.

8. Je, katika maji nako kuna viumbe najisi?

“Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao. Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu.” Law. 11:9,10.

Samaki wa kuliwa nao lazima wawe na sifa mbili:

A. kuwa na magamba;

B. kuwa na mapezi.

Kama samaki amepungukiwa na moja ya sifa hizo ni najisi, tena ni hatari kwa mwili wa binadamu.

9. Vipi kuhusu ndege wa angani?

“Katika ndege, hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu; na mwewe, na kozi kwa aina zake, na kila kunguru kwa aina zake; na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake; na bundi, na mnandi, na bundi mkubwa; na mumbi, na mwari, na mderi; na korongo, na koikoi kwa aina zake, na hudihudi, na popo.” Law. 11:13-19.

10. Na wadudu, je?

“Tena vyote vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne, hivi ni machukizo kwenu. Pamoja na hayo, hivi vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne ni halali kula, hao walio na miguu mirefu, ya kurukia juu ya nchi; katika hao mna ruhusa kuwala; nzige kwa aina zake, na panzi kwa aina zake, na parare kwa aina zake. Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu.” Law. 11:20-23.

11. Kitu gani kingine ni hatari kwetu katika hao walio safi?

“Neno hili litakuwa amri ya daima,… ya kwamba hamtakula mafuta wala damu kabisa.” Law. 3:17.

Damu na mafuta hubeba vijidudu vingi vya magonjwa. Ni hatari kwa afya ya mwili.

 
12. Je, Biblia inazuia matumizi ya pombe?

“Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima.” Mithali 20:1. “Usiitazame mvinyo iwapo ni nyekundu; iitiapo bilauri rangi yake, ishukapo taratibu; mwisho wake huuma kama nyoka; huchoma kama fra.” Mithali 23:31,32. “Waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu,… wala walevi.” 1 Kor. 6:9,10. “Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia.” Hab. 2:15.

Biblia inakataza matumizi ya pombe.

13. Na sigara, je?

Hata paketi ya sigara imeandikwa kabisa kuwa uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako.

A. Matumizi ya tumbaku huathiri afya na kuuchafua mwili (1 Kor. 3:16,17).

B. Nikotini ni sumu inayoleta mazoea na kumfanya mtumiaji kuwa mtumwa (Rum. 6:16).
Watumiaji wa nikotini ni watumwa wa nikotini (Mt. 4:10).

C. Mazoea ya kutumia tumbaku huleta uchafu (2 Kor. 6:17).
Yesu hakutumia tumbako hata kidogo; tufuate nyayo zake (1 Yoh. 2:61 Pet. 2:21).

D. Matumizi ya tumbaku ni kupoteza fedha kwa kitu kisicholeta faida mwilini (Isa. 55:2).

E. Matumizi ya tumbaku hayamvuti ye yote karibu na Yesu (1 Pet. 2:11).
Matumizi ya tumbaku ni tamaa mojawapo ya mwili ipiganayo na roho.

F. Matumizi ya tumbaku hupunguza maisha ya mtumiaji.
Hii ni kuvunja amri isemayo, ‘Usiue’ (Kut. 20:13).
Ukitaka kuahirisha mazishi yako, acha kuvuta tumbako.

14. Kwa nini Mungu azuie vitu hivi ambavyo watu wanafurahia kuvitumia?

“BWANA… hatawanyima kitu chema hao waendao kwa ukamilifu.” Zab. 84:11. “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” 1 Kor. 3:16,17.

15. Je, hatuna uhuru wa kufanya lo lote na miili yetu?

“Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” 1 Kor. 6:19,20.

Miili yetu si mali yetu wenyewe. Tulinunuliwa kwa thamani kubwa (1 Pet. 1:18,19). Ni lazima tumtukuze Mungu kwa kila jambo tunalofanya katika miili yetu.

16. Je, Yesu hakuzifutilia mbali kanuni hizi?

“Maana BWANA atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto. Kwa maana BWANA atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na BWANA watakuwa wengi. Watu wale wajitakasao, na kujisafsha katika bustani, nyuma yake aliye katikati; wakila nyama ya nguruwe, na machukizo, na panya; watakoma pamoja, asema BWANA.” Isa. 66:15-17.

Yesu mwenyewe ameahidi kuwaangamiza watu wanaojitakasa, yaani, wanaojifanya kuwa watu wa Mungu, huku wanakula vitu najisi. (Soma pia Isa. 65:2-7).

Mungu ni mwenye upendo mkuu. Ametupatia maelezo kamili juu ya kila kipengere cha maisha yetu. Anataka kukaa ndani yetu. Lakini anataka kukaa katika miili yenye afya njema; miili inayomtukuza kwa kila jambo. Yesu alikuja duniani kuwatakasa wanadamu wenye dhambi. Hakuja duniani kutakasa nguruwe. Alikuja kuwafa wanadamu, siyo kambale! Hata sasa Yesu anataka kukutakasa. Anataka kusamehe dhambi zako zote na kukufanya uwe mtoto wake. Anataka kukupa uwezo wa kumtukuza katika mwili wako. Ndiyo maana alishuka hadi duniani, akafa msalabani ili akuokoe.

Je, utakubali sasa kumpaYesu mwili wako wote kwa sababu aliununua kwa thamani kubwa? Je, uko tayari kupokea uwezo wake wa kushinda mazoea yote mabaya na kuanza maisha mapya ndani yake?

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15

bottom of page