top of page
Yachunguzeeni.png
Somo-1-Cover-Pic-278x300.png

11. Alama Ya Mnyama

Moja kati ya maonyo yenye lugha kali kabisa katika Biblia linapatikana katika Kitabu cha Ufunuo. Katika onyo hilo Mungu anaelezea adhabu watakayopata wale watakaopokea alama ya mnyama. “Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa (alama) katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji.” Ufu. 14:9-10.

Ukisoma fungu la 12 linasema, “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu,” hao wazishikao Amri za Mungu, na Imani ya Yesu.” Hapa tunayaona makundi mawili ya watu katika siku za mwisho. Wale wenye alama (muhuri) ya Mungu, ndio wale wazishikao Amri za Mungu, na Imani ya Yesu, na wengine ni wale wenye alama ya mnyama, ndio wale waliokubaliana na hila za Ibilisi.

Lakini kama mtu hajui alama ya mnyama ni ipi, bila shaka ataishia kuwa nayo hata bila kujua kuwa anayo. Je, una uhakika kuwa unaweza kuitambua alama ya mnyama? Bila hivyo maisha yako yako hatarini.

Somo hili linaweza kufunua ukweli dhidi ya mambo ambayo umekuwa ukiyaamini na kuyapenda sana tangu utoto. Lakini kwa kuwa Mungu katika upendo wake anatutumia ujumbe huu maalum, ni vyema kuupokea na kufuata ushauri wake.

“Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.” Ufu. 1:3.

1. Kwa kuwa tunataka kujifunza juu ya Alama ya Mnyama, mnyama mwenyewe ni kitu gani?

“Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani.” Dan. 7:17.

Katika unabii mnyama anawakilisha ufalme, serikali au taasisi yenye mamlaka.

2. Mnyama anayeelezewa katika Ufunuo 13 ana sifa zipi?

“Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia mnyama yule. Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?

“Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake; na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa. Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika Kitabu cha Uzima cha MwanaKondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.

“Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.” Ufu. 13:18.

Mnyama huyu anaonekana wazi kuwa ni taasisi ya kidini inayopingana na Mungu. Ni taasisi inayotaka kusujudiwa au kuabudiwa. Hebu tuziangalie alama nane za kuweza kuitambua taasisi hii.

A. Inapokea mamlaka yake toka kwa Joka (fungu la 2).

Joka hapa anawakilisha Shetani (Ufu. 12:3,4,9), lakini Shetani alifanya kazi yake kwa njia ya ufalme wa Roma. Mfalme wa Kiroma Herode alijaribu kumwua Yesu kwa kuua watoto wa Bethlehemu (Mt. 2:16-18). Hivyo Joka anamaanisha pia ufalme wa kipagani wa Roma.

Kuna taasisi moja tu ya kidini iliyopokea kiti cha enzi na mamlaka toka Ufalme wa Roma. Historia inatueleza wazi kuwa taasisi hiyo ni Kanisa la Roma.

“Kanisa la Roma lilijiingiza mahali pa Ufalme wa Roma na kuuendeleza. Papa ni mrithi wa Kaisari.” Bila shaka alama ya kwanza inahusu Mamlaka ya Papa.

B. Ni ufalme ulioenea dunia nzima (fungu la 3,7).

Hakuna anayeweza kubisha kuwa mamlaka ya papa ilienea dunia nzima katika karne za kati. Alama hii tena inahusu Mamlaka ya Papa.

C. Ingedumisha uwezo wake kwa miezi 42.

Miezi 42 ni sawa na siku 30 x 42 = 1260. Katika unabii siku moja ni sawa na mwaka mmoja (Eze. 4:6). Uwezo wa Mamlaka ya Papa ulifkia kilele mwaka 538 B.K. kutokana na barua ya Mfalme Justinian iliyomtambua askofu wa Roma kama mkuu wa makanisa yote. Hata hivyo, uwezo wa Mamlaka ya Papa ulikomeshwa mwaka 1798 ambapo Jemadari wa Kifaransa, Berthier, aliingia Roma na kumteka Papa. Kuanzia mwaka 538 B.K. hadi mwaka 1798 ni miaka 1260 kamili.

D. Ni taasisi yenye kufanya makufuru (fungu la 5,6).

Biblia inaelezea kuwa makufuru ni kudai kuwa yeye ni Mungu, na kudai kuwa ana uwezo wa kusamehe dhambi (Yn 10:33Luka 5:21).

Mamlaka ya Papa tena inayo alama hii, kwani inadai kuwa mapadre wanaweza kusamehe dhambi. Angalia jinsi Katekisimu moja inavyosema: Swali: Je, Padre husamehe kabisa dhambi, au huwa anatangaza tu kwamba zimeondolewa?

Jibu: Padre husamehe kabisa dhambi kwa uwezo aliopewa na Yesu Kristo.

Pia mamlaka hii hudai kuwa Mungu. Hii hapa ni baadhi ya kauli zake: (1) “Wewe ni Mungu mwingine hapa duniani.” (2) “Papa siyo mwakilishi wa Yesu Kristo tu, lakini ni Yesu Kristo mwenyewe aliyefchwa katika mwili.”

E. Ni taasisi iliyopata Jeraha la Mauti, kisha likapona, na “dunia nzima ikamstaajabia” (fungu la 3).

Mamlaka ya Papa ilipata pigo la mauti mwaka 1798 Papa alipotekwa na Jemadari Berthier na kufa uhamishoni. Ulaya yote ilidhani kuwa huo ulikuwa mwisho wa Mamlaka ya Papa. Lakini leo hii kila mtu anatambua kuwa Mamlaka ya Papa ndiyo yenye ushawishi na mvuto kuliko zote duniani. Jeraha la mauti lilipona pale Kiongozi wa Italia (Musolini) alipomrudishia Papa Mamlaka ya Kiserikali na kuunda Taifa la Vatikani mwaka 1929. Leo hii mamilioni wanaiangalia Mamlaka ya Papa kama tumaini pekee la umoja, upendo, amani na uungwana. Hivyo tena Mamlaka ya Papa inayo alama hii. 

VICARIUS FILII DEI

V - 5            F - 0             D - 500

I - 1              I - 1              E - 0 

C - 100        L - 50            I - 1      

A - 0             I - 1                   501

R - 0             I - 1   

I - 1                   53

U - 5

S - 0    

      112

112 + 53 + 501 = 666

 

F. Ina namba ya siri 666. Ufunuo 13:17-18 inatuambia tuihesabu hesabu ya mnyama maana ni hesabu ya kibinadamu.

Zingatia kuwa baadhi ya heruf za Kirumi hutumika pia kama namba. Hivyo basi, hesabu ya jina la mtu ni jumla ya heruf zote zilizo katika jina lake zinazotumika kama namba.

Binadamu tunayemfkiria kila tunapozungumza juu ya Mamlaka ya Papa ni Papa mwenyewe. Moja kati ya majina rasmi ya Papa ni “MWAKILISHI WA MWANA WA MUNGU” kwa Kirumi ni ‘VICARIUS FILII DEI’. Kitabu cha Ufunuo kinasema kuwa jumla ya namba za Kirumi katika jina lake ni 666. Hebu tuone.

Hivyo Mamlaka ya Papa inayo alama hii tena.

G. Ni Taasisi au Mamlaka ya Kidini.

Inajihusisha na mambo ya kiroho. Neno “kusujudia” limetumika mara 4 katika Ufunuo 13. Sura hii inahusu ibada ya bandia. Hii ni alama nyingine inayoonekana katika Mamlaka ya Upapa.

H. Itafanya vita na kuwatesa Wakristo (fungu la 7).

Historia inaonyesha wazi kuwa Mamlaka ya Papa ilitesa na kuangamiza Wakristo, hasa katika kilele cha utawala wake katika karne za kati. Wanahistoria wengi wanasema zaidi ya watu milioni hamsini waliuawa kwa ajili ya imani zao katika kipindi cha dhiki kuu. Kanisa lilidhani kuwa lilikuwa linamsaidia Mungu kuondoa “uzushi.” Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba lilitesa na kuangamiza. Mamlaka ya Papa tena inayo alama hii.

Zingatia: Wapo Wakristo wengi wa Kikatoliki ambao ni wema, waaminifu na wenye upendo, wanaomtumikia Yesu, na Yesu anawahesabu kuwa ni watu wake.

Papa Yohana Paulo II mwenyewe anaonekana kuwa mtu mchangamfu, mwenye huruma, mwenye kupenda mapatano, na jasiri anayempenda Mungu. Hili sio somo la kuwasuta rafki zetu, Wakristo wa Kikatoliki. Hili ni shambulio dhidi ya Ibilisi aliyesababisha yote haya. Hata hivyo ni kweli kwamba Mungu mwenyewe ndiye aliyetuambia kuwa Taasisi hii ina alama ambayo hatupaswi kuipokea. Waprotestanti waaminifu, Wakatoliki, Wayahudi, na wasiokuwa katika kanisa lo lote, wanapaswa kuijua alama hii ili wasiipokee. Tunamshukuru Mungu kwa kuifunua mipango mibovu ya Shetani ya kutuangamiza sisi sote.

Ili tuijue alama hii ya Mamlaka ya Papa, ni lazima kwanza tuijue Alama ya Mungu.

3. Je, Mungu naye anayo alama?

“Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai;… Akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao.” Ufu. 7:2,3. “BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake… Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu.” Eze. 9:4,6.

Mungu anayo alama kwa ajili ya watu wake.

4. Je, tunaweza kuijua alama hiyo kwa uhakika?

“Tena naliwapa Sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye… Zitakaseni Sabato zangu; nazo zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” Eze. 20:12,20.

Kwa uhakika kabisa. Mungu ameweka Sabato ili iwe ishara ya watu wanaomtambua kwamba yeye ndiye Muumbaji na kwamba yeye ndiye anayewatakasa watu wake (angalia pia Yer. 10:10-16).

5. Biblia inasema kuwa Mamlaka ya Papa ingeazimu kufanya jambo gani?

“Naye ataazimu kubadili majira na Sheria.” Dan. 7:25.

Kubadili majira (muda) na Sheria. Mamlaka ya Papa inajigamba yenyewe kuwa ilifanya jambvo hilo. Hebu angalia mahojiano haya yaliyo katika Katekisimu ya Waumini ya Mafundisho ya Kikatoliki, katika ukurasa wa 50.

Swali: Siku ya Sabato ni ipi?
Jibu: Siku ya Sabato ni Jumamosi.
Swali: Kwa nini tunaiadhimisha Jumapili badala ya Jumamosi?
Jibu: Tunaadhimisha Jumapili badala ya Jumamosi kwa sababu Kanisa Katoliki lilihamisha utakatifu wa siku hiyo kutoka Jumamosi kwenda Jumapili.”

Mtu mmoja aliposoma mahojiano haya alishangaa, naye akidhani kuwa wachapaji walikuwa wamekosea, alimwandikia James Cardinal Gibbons wa Baltimore na kumwuliza kama kweli kanisa lilibadili siku ya Ibada kutoka Jumamosi kwenda Jumapili Kadinali alijibu: “Ndiyo, Kanisa Katoliki linadai kuwa badiliko hilo lilikuwa ni tendo lake. Na tendo hilo ni ALAMA ya uwezo wake wa kikanisa na mamlaka yake katika masuala ya kidini.”

Angalia pia mahojiano haya katika Katekisimu ya Mafundisho iliyoandikwa na Stephen Keenan.

Swali: Je, unayo njia nyingine ya kuthibitisha kuwa kanisa lina uwezo wa kuweka sikukuu?

Jibu: “Kama lisingekuwa na uwezo kama huo, lisingeweza kufanya jambo ambalo hata wanadini wa leo wanalikubali. Lisingeweza kuweka maadhimisho ya Jumapili, siku ya kwanza ya juma, badala ya maadhimisho ya Jumamosi, siku ya saba ya juma, mabadiliko ambayo hayakutokana na Maandiko.”

Mamlaka ya Papa hapa inauliza swali. Hapa kuna swali maarufu ambalo Mamlaka ya Papa imekuwa ikiwauliza mara kwa mara Waprotestanti, na cha kushangaza Waprotestanti wamekuwa hawalijibu:

“Mtaniambia kuwa Jumamosi ilikuwa Sabato ya Wayahudi. Lakini Sabato ya Wakristo ilibadilishwa kwenda Jumapili. Ilibadilishwa! Lakini na nani? Ni nani aliye na mamlaka ya kubadili amri dhahiri ya Mungu Mwenyezi? Mungu anaposema, “Ishike siku ya saba uitakase,” ni nani anayeweza kusema, hapana. Unaweza kufanya kazi na kushughulika na mambo yote ya kidunia katika siku ya saba, lakini uishike na kuitakasa siku ya kwanza badala yake? Hili ni swali muhimu ambalo sijui namna mnavyoweza kulijibu. Ninyi ni Waprotestanti na mnadai kuwa mnafuata Biblia, tena Biblia peke yake, na bado katika suala muhimu kama la kuadhimisha siku moja kati ya saba mnakwenda kinyume na andiko la Biblia na kuweka siku nyingine badala ya ile ambayo Mungu ameamuru. Amri ya kushika siku ya saba ni moja kati ya Amri kumi. Mnaamini kuwa zile nyingine tisa zinapaswa kushikwa, ni nani aliyewapa ruhusa ya kuichezea ile ya nne? Kama kweli mnashikilia msimamo wenu, kama kweli mnataka kufuata Biblia, tena Biblia peke yake, mnapaswa kutuonyesha sehemu katika Agano Jipya ambapo amri ya nne imebadilishwa. (Nukuu kutoka, Library of Christian Doctrine. Burns and Oates, uk. 3-4., London.)

Mamlaka ya Papa inadai kuwa ilibadili siku ya Ibada toka Jumamosi kwenda Jumapili na kwamba Jumapili au kushika Jumapili ni Alama ya Mamlaka na Uwezo wake. Alama au Ishara ya uwezo wa Mungu wa kuumba na kutakasa ni Sabato au kushika Sabato, na Ishara au Alama ya uwezo wa mnyama ni Jumapili.

6. Je, kuna wakati ambapo watu watalazimishwa kupokea Alama ya Mnyama?

“Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.” Ufu. 13:16,17.

Biblia inasema wazi kwamba watu watawekewa vikwazo vya kiuchumi na hata kuuawa wasipoipokea Alama ya Mnyama.

7. Nifanye nini sasa ili nisiipokee alama hiyo?

Ufunuo 14:9-11 inaonya juu ya Alama ya Mnyama; fungu la 12 linaelezea jinsi watakatifu watakavyofanya ili kuepuka alama hiyo. Watashika Amri za Mungu na kuwa na Imani ya Yesu. Bwana asifwe, ni imani ya Yesu inayofanya mwujiza kwa watu wanaoshika amri.

Ujumbe wa Onyo la Mwisho toka kwa Mungu (Ufu. 14:6-12).

Onyo hili ni pamoja na:

(a) Msujudieni Muumbaji (fungu la 7).

Maana yake ni kuishika ishara au alama ya uumbaji wake, yaani, Sabato yake.

(b) Msipokee Alama ya Mnyama (fungu la 9-10).

Maana yake usiikubali wala kuipokea ishara ya bandia ya utakatifu wa Jumapili.

Ni Mungu anayetupa maonyo haya. Shetani, adui wa Mungu anataka nimtii kwa kushika alama yake. Yesu, Mwokoziwangu anataka nimtii kwa kuiadhimishaishara au alama yake.

Je, sasa umeelewa kwamba mtu ye yote Akiipokea Alama ya Mnyama atapotea?

Yesu anabisha kwenye mlango wa moyo wako. Anasubiri jibu toka kwako. Je, utaamua kuipokea ishara yake tukufu kama ushahidi kwamba umempokea yeye kama Bwana na Mwokozi wako?

 

 

 

 

          

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15

bottom of page