top of page
Yachunguzeeni.png
Somo-1-Cover-Pic-278x300.png

08. Kuzaliwa Upya

Mhubiri mmoja alipokuwa akiendesha mahubiri kule Moscow, Urusi mnamo mwezi Machi, 1992, alivamiwa ofsini na kijana mmoja mwenye nguvu na sura ya kutisha. Mhubiri yule aliogopa, lakini baada ya muda mkalimani wake alimjulisha kuwa yule kijana alikuwa ni mmoja wa wahalifu walioshindikana katika jiji la Moscow. Alikuwa amefungwa jela mara nyingi. Sasa alikuwa akijisikia hatia na hakuwa na amani. Mhubiri yule alimsomea 1 Yoh. 1:9, “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafsha na udhalimu wote.”

Alimsimulia kisa cha yule mwizi msalabani aliyesamehewa na Yesu akiwa juu ya msalaba. Alimhakikishia kuwa Yesu bado anaokoa hata sasa. Anasamehe. Mhubiri alimtia moyo yule kijana ampokee Yesu. Yule kijana, huku akitokwa na machozi, alipiga magoti na kupokea msamaha wa Yesu.

Baada ya mwaka mmoja, Mhubiri yule alitembelea tena Moscow na kumwona yule kijana akimsifu Mungu katika kwaya. Baada ya kumpokea Yesu, alikuwa amebadilika na kubatizwa.

Ubatizo ni ishara ya kuanza maisha mapya. Ni Kuzaliwa Upya.

1. Je, ubatizo ni wa lazima?

“Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Mk. 16:16.

Jambo hili liko wazi. Ubatizo ni moja kati ya mahitaji kwa ajili ya wokovu.

2. Siku hizi kuna ubatizo wa aina nyingi. Je, wo wote kati ya huo si unakubalika mradi anayebatizwa awe mwaminifu?

“Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja.” Efe. 4:5.

Upo mmoja tu. Mwingine wo wote ni wa bandia.

3. Je, Yesu alibatizwa namna gani?

“Yesu… akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka.” Mk. 1:9,10.

Alizamishwa! Kwani baada ya kubatizwa “alipanda kutoka majini”.

Yohana pia alikuwa akibatizia mahali palipokuwa na “maji tele” (Yn 3:23). Biblia inatuamuru kufuata nyayo za Yesu (1 Pet. 2:21). Ubatizo wo wote tofauti na huu unakiuka agizo hili. Neno ‘Ubatizo’ linatokana na neno la Kigiriki “Baptizo”, ambalo maana yake ni kuzamisha au kutosa.

 

4. Lakini, je, wanafunzi au Mitume hawakubadilisha namna ya kubatiza?

“Wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo.” Mdo. 8:38,39.

Tafadhali zingatia kuwa Filipo aliyekuwa kiongozi katika Kanisa la Mwanzo, alimbatiza Mtunza Hazina wa Malkia wa Kushi kwa kumzamisha kama vile Yohana alivyomzamisha Yesu. Naye Mtume Paulo alionya kuwa ye yote afundishaye kinyume na vile alivyofundisha Yesu, “alaaniwe” (Gal. 1:8).

5. Kama Yesu na Mitume walibatiza kwa kuzamisha, ni nani aliyeanzisha haya mambo mengine yanayoitwa ubatizo?

“Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu.” Mt. 15:9.

Watu waliopotoka walianzisha aina nyingine za ubatizo kinyume kabisa na Neno la Mungu. “Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?” “Mkalitangua Neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu.” Mt. 15:3,6. Ibada inayofuata mafundisho ya wanadamu ni bure.

6. Mtu anapaswa kufanya nini ili abatizwe?

A. Kujifunza mapenzi ya Mungu.

“Basi, enendeni, mkawafanye Mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza… na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mt. 28:19,20).

B. Kuuamini ukweli wa Neno la Mungu. 

“Aaminiye na kubatizwa ataokoka” (Mk. 16:16).

C. Kutubu na kuziacha dhambi zake na kuongoka.

“Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi” (Mdo. 2:38); “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe” (Mdo. 3:19).

7. Maana ya ubatizo ni nini?

“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; tukijua nano hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.” Rum. 6:4-6.

Ubatizo huonyesha matukio matatu ya muhimu katika maisha ya muumini wa kweli:

(1) Kuifa dhambi;

(2) Kuzaliwa upya katika Kristo; na

(3) Kuolewa na Kristo milele. Muungano huo wa kiroho utazidi kukomaa na kuwa mtamu zaidi kadri muda unavyozidi kwenda na upendo utakavyozidi kukua.

8. Je, mtu anaweza kubatizwa kabla hajawa na uhakika kuwa ataanguka tena?

“Kwa maana kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kuushinda ulimwengu, hiyo imani yetu.” 1Yoh. 5:4.

Hii ni sawa na kusema kuwa mtoto asijaribu kutembea mpaka awe na uhakika kuwa hatateleza na kuanguka. Mkristo huzaliwa upya katika Kristo. Ndiyo maana kuongoka huitwa kuzaliwa upya.

 
“Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Marko 16:16
 
9. Kwa nini ubatizo ni muhimu kwa mwenye dhambi aliyeongoka?

“Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.” Mdo. 22:16.

Ubatizo ni ushuhuda wa hadhara kuwa mwenye dhambi aliyetubu amesamehewa na kutakaswa na Yesu (1 Yoh. 1:9), na kwamba maisha yake ya dhambi yamepita.

10. Je, Mungu hujisikiaje mtu aliyeongoka anapobatizwa kama Yesu alivyobatizwa?

Wakati wa ubatizo wa Mwanawe, alisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Mt. 3:17. Hata leo Mungu hupendezwa mtu anapobatizwa kwa kuzamishwa kama vile alivyoagiza. Wote wampendao Mungu watajitahidi kumpendeza (1 Yoh. 3:221 Thes. 4:1). “Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.” Luka 15:7.

11. Je, kuzaliwa na wazazi waliobatizwa hakutoshi?

“Waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Yn 1:13.

Kuzaliwa kwa baba na mama ni kuzaliwa katika Adamu wa kwanza, katika asili ile ile ya dhambi. Ili tupatane na Mungu na kuwa wana wake ni lazima tuzaliwe mara ya pili katika Kristo Yesu aliye Adamu wa pili kwa njia ya ubatizo.

12. Je, mtu anaweza kubatizwa mara ya pili au zaidi?

A. Kutojua ukweli wote.

“Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafka Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, je! mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.” Mdo.19: 1-5.

B. Kuasi.

“Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa au mtoza ushuru.” Mathayo 18:15-17.

13. Je, mtoto mchanga anaweza kubatizwa?

Yesu alisema, “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Mathayo 28:19. “Aaminiye na kubatizwa ataokoka.” Marko 16:16.

Ni wazi kwamba mtoto mdogo hawezi kuhubiriwa, kisha akakiri na kuamini ili abatizwe. Ni dhahiri basi kuwa ubatizo ni kwa watu waliopevuka kiakili kiasi cha kufanya maamuzi yao binafsi. Watoto wadogo hubarikiwa (Mathayo 19:13-15).

14. Je, mtu anaweza kubatizwa kwa dhati bila kujiunga na Kanisa la Mungu?

A. Wote wameitwa katika mwili mmoja.

“Ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja.” Kol. 3:15.

B. Mwili huo ni kanisa.

“Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa.” Kol. 1:18.

C. Tunaingia katika mwili huo kwa njia ya ubatizo.

“Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja.” 1 Kor. 12:13.

D. Watu wa Mungu walioongoka, huzidishwa kwenye kanisa lake.

“Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.” Mdo. 2:47. Bibi-harusi huwa anaacha jina lake na kuchukua jina la mumewe kwa upendo na kwa hiari wakati wa kufunga ndoa. Kwa njia hii huwa anaonyesha nia yake ya kuunganishwa na mumewe. Wafuasi wa Kristo pia kwa upendo na kwa hiari husalimisha mioyo na maisha yao kwa Kristo na kulipokea jina lake. Kisha huitwa Wakristo, kwa kuwa wameonyesha nia ya kuunganishwa naye.

Je, umechukua hatua inayokuunganisha na familia ya Mungu? Yesu anasema, “Njoo.” Je, wewe unasemaje baada ya kusikia wito wake? Je, utamwambia Yesu asubiri kwanza wakati unashughulika na mambo ya dunia hii?

Je, utaamua sasa hivi kuitika na kumfuata Yesu katika agizo hili takatifu?

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15

bottom of page