06. Amri Za Mungu
Hivi karibuni mtu mmoja aliingia kwenye Kituo cha Polisi akiwa na hasira na jasho likimtoka. Alitaka polisi wachukue hatua za haraka kuwakamata watu waliovunja na kuiba nyumbani kwake. Aliulizwa kama anaweza kuwatambua baadhi ya watu waliomwibia. Aliposema anaweza, yule ofsa wa polisi alimpeleka chumba cha taarifa mbalimbali na kumwonyesha picha zilizokuwa kwenye kitabu ili aweze kuona kama anaweza kuwatambua katika zile picha. Walipokuwa wanaendelea, yule askari alisita kwenye ukurasa mmoja na kuiangalia picha moja, kisha akamwangalia yule mtu. Akamwambia, “Wewe pia unatafutwa na polisi. Picha yako hii hapa, uko chini ya ulinzi.”
Uhalifu umekithiri kila mahali, makazini, viwandani, mijini na vijijini. Uasi, mapinduzi, wizi, ujambazi, ugaidi, utekaji nyara, ubakaji, rushwa, na kadhalika, vimeenea kila mahali.
Dunia yetu imekumbwa na balaa gani? Maadili kwa watoto yameporomoka. Ni nani wa kuwaongoza iwapo hata baba na mama si waaminifu. Waalimu na viongozi mbalimbali ni wadanganyifu. Hakuna anayeaminika. Watu wamefka mahali pa kusema kuwa kanuni ya Mungu ya wema na uovu imepitwa na wakati. Hata baadhi ya makanisa yanafundisha kuwa Amri za Mungu zimefutwa. Maneno haya ni kawaida kuyasikia yakisemwa na watu wanaojiita Watumishi wa Yesu. Matokeo yake, watu wanajifanyia wanavyopenda, na jamii inavuna ilichopanda.
Je, Mungu anayo kanuni thabiti iliyokusudiwa kuleta amani na furaha kwa wanadamu? Ndiyo. Hebu tuone Biblia inasemaje juu ya kanuni hii inayoitwa Amri Kumi za Mungu.
1. Je Mungu mwenyewe aliziandika Amri Kumi?
“Akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda (kidole) cha Mungu.” Kut. 31:18. “Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.” . Kut. 32:16.
Mungu Mkuu aliziandika Amri Kumi kwa kidole chake kwenye mbao za mawe.
2. Mungu anasema dhambi ni nini?
“Dhambi ni uvunjaji wa Sheria ya Mungu.” 1 Yoh. 3:4, HN.
Na kwa sababu Sheria ya Mungu ni kamilifu (Zab. 19:7), inagusa kila aina ya dhambi.
3. Kwa nini Mungu alitupatia Amri Kumi?
A. Alitupatia Amri Kumi ili zituongoze kwenye maisha ya furaha na uzima tele.
“Aendaye kwa unyofu ataokolewa; bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.” Mit. 29:18. “Mwanangu, usiisahau sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu. Maana zitakuongezea wingi wa siku, na miaka ya uzima na amani.” Mit. 3:1,2.
B. Kutuonyesha tofauti kati ya wema na ubaya.
“Kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” Rum. 3:20. “Singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.” Rum. 7:7.
C. Kutuepusha na hatari na maafa.
Sheria ya Mungu ni kama kioo (Yak. 1:23-25). Inatuonyesha makosa katika maisha yetu kama vile kioo kinavyoonyesha uchafu usoni. “BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai.” Kumb. 6:24. “Unisaidie nami nitakuwa salama, nami nitaziangalia amri zako daima. Umewakataa wote wazikosao amri zako, kwa maana hila zao ni uongo.” Zab. 119:117,118. Sheria ya Mungu ni kama wigo unaotukinga na uharibifu. Inatukinga na uchafu, uongo, mauaji, ibada ya sanamu, wizi, pamoja na uovu mwingine unaoharibu maisha, amani na furaha. Sheria nzuri zote hulinda, na sheria ya Mungu hulinda pia.
4. Kwa nini Sheria ya Mungu ni ya muhimu sana kwetu?
“Semeni ninyi, na kutenda kama watu waatakaohukumiwa kwa Sheria ya Uhuru.” Yak. 2:12.
Kwa sababu Amri Kumi ndicho kipimo atakachotumia Mungu kuwapima watu katika hukumu. Hili na suala la kufa na kupona.
5. Je, Sheria ya Mungu inaweza kubadilishwa au kufutwa?
“Lakini ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati (sheria).” Lk. 16:17.
“Mimi sitalihalifu agano langu, sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.” Zab. 89:34. “Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, Maagizo yake yote ni amini, yamethibitika milele na milele, yamefanywa katika kweli na adili.” Zab. 111:7,8.
Biblia iko wazi kabisa. Kama Sheria ya Mungu ingeweza kubadilishwa, Mungu angebadilisha mara baada ya Adamu na Hawa kutenda dhambi, badala ya kumtuma Mwanawe kuja kufa badala ya mwenye dhambi ili kulipa fdia ya Sheria iliyokuwa imevunjwa. Hili lisingewezekana kwa sababu Amri za Mungu si kama sheria zilizotungwa Bungeni. Ni kanuni za tabia takatifu ya Mungu, ambazo zitadumu na kuwa sahihi kadiri Mungu aishivyo.
Tabia Mungu ni Sheria ni
Wema Luka 18:19 1Tim. 1:8
Usafi 1Yoh. 3:2,3 Zab. 19:8
Haki Kumb. 32:4 Rum. 7:12
Kiroho 1Kor. 10:4 Rum. 7:14
Haki Yer. 23:6 Zab. 119:172
Uaminifu 1Kor. 1:9 Zab. 119:86
Upendo 1Yoh. 4:8 Rum. 13:10
Kutobadilika Yak. 1:17 Mt. 5:18
Umilele Mwa. 21:33 Zab. 111:7,8
6. Je, Yesu aliifuta Sheria ya Mungu alipokuwa hapa duniani?
“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati (sheria) au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati (sheria) haitaondoka, hata yote yatimie.” Mt. 5:17,18.
Yesu alisema dhahiri kabisa kuwa hakuja kufanya kazi hiyo ya kutangua Amri Kumi.
7. Je, watu wanaoendelea kuvunja Amri za Mungu makusudi wataokolewa?
“Mshahara wa dhambi ni mauti.” Rum. 6:23. “Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.” Isa. 13:9. “Mtu awaye yote atakayeishika Sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.” Yak. 2:10.
Watapotea, kwa sababu Biblia inasema, “Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunazishika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” 1 Yoh. 2:3,4.
8. Je, mtu anaweza kuokolewa kwa kushika amri?
“Hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya Sheria.” Rum. 3:20. “Mmeokolewa kwa Neema, kwa njia ya Imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” Efe. 2:8,9.
Jibu liko wazi. Hakuna anayeweza kuokolewa kwa kushika Sheria. Wokovu huja kwa njia ya neema peke yake, kama zawadi ya bure toka kwa Yesu, nasi huipokea zawadi hiyo kwa njia ya imani. Siyo kwa matendo. Kazi ya Sheria ni kutuonyesha kasoro tulizo nazo katika maisha. Baada ya kujua uovu wetu, tunamwendea Yesu ili atutakase na kutusamehe.
9. Ni kitu gani kinachomwezesha Mkristo aliyeongoka kweli kushika Amri za Mungu?
“Nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mioyo yao nitaziandika.” Ebr. 8:10. “Nayaweza mambo yote katika yeye (Kristo) anitiaye nguvu.” Flp. 4:13. “Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe… ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi.” Rum. 8:3,4. “Nami nitatia Roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika Sheria zangu.” Eze. 36:27.
Baada ya kutubu, Kristo haishii kusamehe tu, bali huwarejeshea sura ya Mungu wenye dhambi waliotubu. Huwafanya waende sawasawa na Sheria yake kwa njia ya uwezo wa kukaa ndani yao.
10. Je! siyo kwamba Mkristo mwenye imani na aliye chini ya neema halazimiki kushika Sheria?
“Maana dhambi ni uvunjaji wa Sheria ya Mungu” (1 Yoh. 3:4, HN/AJKK). “Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya Sheria, bali chini ya neema. Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya Sheria bali chini ya neema? Hasha!” Rum. 6:14,15. “Basi, je! twaibatilisha Sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume chake twaithibitisha Sheria.” Rum. 3:31.
Hapana. Maandiko yanafundisha kinyume kabisa. Neema ni kama msamaha wa Rais kwa mfungwa. Neema humsamehe, lakini haimpi ruhusa kuvunja hata kipengere kimoja cha Sheria. Ni motisha ya kumfanya mtu atii.
11. Je, Amri Kumi za Mungu zimesisitizwa katika Agano Jipya?
Ndiyo, tena kwa wazi kabisa. Chunguza aya hizi kwa makini.
Amri kumi za Mungu katika agano jipya
1) “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Mt. 4:10.
2) “Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.” 1 Yoh. 5:21. “Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.” Mdo. 17:29.
3) “Jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yake.” 1 Tim. 6:1, KJV.
4) “Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote.” “Basi, imesalia raha ya Sabato [“utunzaji wa Sabato”, pambizo] kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.” Ebr. 4:4,9,10.
5) “Waheshimu baba yako na mama yako.” Mt. 19:19.
6) “Usiue.” Rum. 13:9.
7) “Usizini.” Mt. 19:18.
8) “Usiibe.” Rum. 13:9.
9) “Usimshuhudie jirani yako uongo.” Rum. 13:9,KJV. (Imerukwa katika Biblia ya Kiswahili, Union Version). “Usishuhudie uongo.” Mt. 19:18.
10) “Usitamani.” Rum. 7:7.
Amri kumi za Mungu katika agano la kale
1) “Usiwe na miungu mingine ila Mimi.” Kut. 20:3.
2) “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.” Kut. 20:4-6.
3) “Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.” Kut. 20:7.
4) “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” Kut. 20:8-11.
5) “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.” Kut. 20:12.
6) “Usiue.” Kut. 20:13.
7) “Usizini.” Kut. 20:14.
8) “Usiibe.” Kut. 20:15.
9) “Usimshuhudie jirani yako uongo.” Kut. 20:16.
10) “Usitamani nyumba ya jirani yako, usitamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.” Kut. 20:17.
12. Shetani ana hisia gani kwa watu wanaoendesha maisha yao kwa kufuata Amri Kumi za Mungu?
“Joka amkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao Amri za Mungu.” Ufu. 12:17. “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao Amri za Mungu, na Imani ya Yesu.”
Ibilisi anawachukia watu wanaoshika Sheria ya Mungu ambazo ni kipimo chamaisha ya unyoofu. Je, unaamini kwamba ni lazima Mkristo ashike Amri 10 za Mungu?
Katika Yohana 15:10 Yesu anasema, “kama vile mimi nilivozishika amri za baba yangu (Amri Kumi) na kukaa katika pendo lake.”
Je, unakusudia kupita katika nyayo za Yesu na kuzishika Amri zake ili ukae katika pendo lake?
Yesu anasema pia, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”
Je, unampenda Yesu kiasi cha kuzitii amri zake kwa furaha?