top of page
Yachunguzeeni.png
Somo-1-Cover-Pic-278x300.png

05. Mfalme Anakuja

Dunia haijawahi kuwa na matatizo kama iliyo nayo sasa hivi ambayo yanaonekana kana kwamba hayana ufumbuzi. Magazeti ya kila siku yanaandika juu ya matatizo ambayo mwanadamu hawezi kuyamudu. Ufumbuzi wa kudumu kwa matatizo haya unaweza kupatikana wapi? Biblia yako inalo jibu. Kristo alizungumzia tukio ambalo litatatua matatizo yote ya wanadamu. Hakuna ufumbuzi mwingine!

Miaka 2000 iliyopita, mwishoni mwa huduma yake hapa duniani, Yesu alizungumza juu ya siku ya kusulibiwa kwake. Wanafunzi hawakuweza kuamini kuwa janga kama hilo lingeweza kumpata Kiongozi wao ambaye walimpenda. Kristo alijua kwamba wangehitaji tumaini thabiti katika siku za usoni. Akawapaatia ahadi nzuri iliyopo katika Yohana 14:1-3: “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.”

Kutimia kwa ahadi hii wakati wa kuja kwa Yesu mara ya pili ni tumaini pekee la ulimwengu. Hebu tuangalie Neno la Mungu linafundisha nini juu ya tukio hili la ajabu – Kuja kwa Mfalme wetu!

1. Je, tunaweza kuwa na uhakika kuwa Yesu atarudi tena duniani?

“Kristo… atatokea mara ya pili.” Ebr. 9:28. “Nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena.” Yn 14:3.

2. Je, Yesu atarudi tena kwa jinsi gani?

“Walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokua akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.” Mdo. 1:9-11.

Maandiko yanaahidi kuwa Yesu atarudi kwa jinsi ile ile alivyoondoka – akionekana katika mwili halisi.

Mathayo 24:30 inasema: “Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.”

3. Je, kuja kwa Yesu mara ya pili kutaonekana na watu wote au kundi fulani tu la watu?

“Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona.” Ufu. 1:7. “Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” Mt. 24:27.

Unyakuo wa siri, unaoaminiwa na wengi na kufundishwa siku hizi, haupo kwenye Biblia. Ni uzushi wa wanadamu. Kuja kwa Yesu mara ya pili litakuwa tukio halisi, litakaloonekana duniani kote. Yesu mwenyewe ataonekana akija katika mawingu kuikomesha dunia na kuwapa tuzo au kuwaadhibu watu wote.

4. Ni nani atakayekuja pamoja na Yesu?

“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake.” Mt. 25:31.

Malaika wote wa mbinguni watakuwa pamoja na Yesu atakaporudi. Nao watawakusanya haraka wateule na kuwaandaa kwa ajili ya safari ya kwenda minguni (Mt. 24:31).

5. Lengo la kuja kwa Yesu mara ya pili ni lipi?

“Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” Ufu. 22:12. “Nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yn 14:3. “Apate kumtuma Kristo Yesu… ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote.” Mdo. 3:20,21.

6. Kutatokea jambo gani kwa watu wenye haki?

“Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni… nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.” 1 Thes. 4:16,17. “Sote tutabadilika… na wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu… Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika.” 1 Kor. 15:51-53. “Tunamtazamia…Bwana Yesu Kristo, atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu.” Flp. 3:20,21.

Wenye haki waliokufa, watafufuliwa na kupewa miili mikamilifu isiyokufa kama ule wa Yesu. Nao wale wenye haki walio hai, watapewa miili kama ule wa Yesu na kwa pamoja na wale waliofufuliwa watanyakuliwa ili kumlaki Bwana hewani.

7. Kutatokea nini kwa watu waovu?

“Kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.” Isa. 11:4. “Na waliouawa na Bwana siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili.” Yer. 25:33.

Waovu watauawa na Yesu.

8. Je, kuja kwa Yesu kutaiathiri vipi dunia yenyewe?

“Palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.” “Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.” Ufu. 16:18,20. “Nikaangalia, na tazama, shamba lililozaa sana limekuwa ukiwa, na miji yake yote ilikuwa imebomoka mbele za BWANA.” Yer. 4:26. “BWANA ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa.” “Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa.” Isa. 24:1,3.

Dunia itakumbwa na tetemeko kubwa litakaloiacha dunia hii katika hali ya kuharibiwa kabisa. Itakuwa tupu!

9. Je, Biblia ina maelezo yo yote juu ya kukaribia kuja kwa Yesu?

Ndiyo! Biblia ina maelezo. Yesu mwenyewe alisema, “Myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.” Mt. 24:33. Bwana aliweka ishara katika nyakati zote tangu kupa kwake hadi kuja kwake mara ya pili. Zimeorodheshwa hapa. Hebu zisome kwa makini.

A. Kuangamizwa kwa Yerusalemu.

Unabii: “Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.” “Walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani.” Mt. 24:2,16.

Kutimia: Yerusalemu uliangamizwa na mpiganaji wa Kirumi, Tito, mnamo mwaka 70 B.K.

B. Mateso au dhiki.

Unabii: “Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.” Mt. 24:21.

Kutimia: Kimsingi unabii huu unahusu kipindi cha dhiki iliyotokea wakati wa Zama za Giza na ilisababishwa na kanisa lililoasi. Dhiki hii ilichukua zaidi ya miaka 1000. Zaidi ya Wakristo milioni 50 waliuawa kwa ajili ya imani yao katika kipindi cha dhiki kuu.

C. Jua kutiwa giza.

Unabii: “Mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza.” Mt. 24:29.

Kutimia: Ulitimia kwa siku ya giza lisilokuwa la kawaida tarehe 19 Mei, 1780. Haikuwa kukamatwa kwa jua. Watu wengi walihisi kuwa siku ya hukumu imekaribia.

D. Mwezi kuwa kama damu.

Unabii: “Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo.” Yoeli 2:31.

Kutimia: Mwezi ulikuwa mwekundu kama damu siku ile jua lilipotiwa giza tarehe 19 Mei, 1780.

E. Nyota kuanguka toka mbinguni.

Unabii: “Nyota zitaanguka mbinguni.” Mt. 24:19.

Kutimia: Nyota zilianguka kwa wingi usiku wa tarehe 13 Novemba, 1833. Kwa muda wa karibu masaa manne anga lilikuwa likiangaza.

F. Yesu kuja katika mawingu.

Unabii: “Ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo Mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboloeza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.” Mt. 24:30.

Kutimia: Hili ndilo tukio linalofuata. Je, uko tayari?

10. Tutajuaje kwamba tumefkia ukingoni mwa historia ya dunia? Je, Biblia inaelezea hali ya dunia na watu wake katika kizazi cha mwisho?

A. Migogoro Makazini.

“Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi.” “Nanyi vumilieni,… kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia.” Yak. 5:4,8.

Migogoro ya kikazi imetabiriwa kuwa itatokea katika siku za mwisho.

B. Vita na Machafuko.

“Nanyi mtakaposikia habari za vita na ftina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutokea kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi.” Lk. 21:9.

Vita na mauaji ya kiraia yanaathiri maelfu duniani kote. Ni kurudi kwa Yesu tu kutakakokomesha maumivu na uharibifu wa vita.

C. Machafuko, hofu, na vurugu.

“Tena, kutakuwa… na katika nchi dhiki ya Mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjia mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayojupata ulimwengu.” Lk. 21:25,26.

Hali ya wasiwasi iliyopo duniani leo, haipaswi kutushangaza. Yesu aliitabiri. Inapaswa kutushawishi kuwa kuja kwake ku karibu.

D. Kuongezeka kwa maarifa.

“Hata wakati wa mwisho… maarifa yataongezeka.” Dan. 12:4.

Enzi ya Kompyuta na Mitandao inathibitisha wazi jambo hili. Hata mtu mwenye akili ngumu kuamini anapaswa kukiri kuwa ishara hii imekwisha kutimia. Maarifa yanaongezeka katika nyanja zote.

E. Watu wenye kudhihaki, wenye mashaka katika dini wanaoukataa ukweli wa Biblia.

“Siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki.” 2 Pet. 3:3. “Utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima… Watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.” 2 Tim. 4:3,4.

Si vigumu kuona wenye dhihaka siku hizi kama utimilifu wa unabii huu. Hata viongozi wa dini wanakataa mafundisho ya wazi ya Biblia juu ya uumbaji, Gharika, Uungu wa Kristo, Kuja kwa Yesu na ukweli mwingine mwingi wa Biblia.

F. Kuporomoka kwa maadili – Kupoa Kiroho.

“Siku za mwisho… watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe,… wasiowapenda wa kwao,… wasiojizuia,… wasiopenda mema,… wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake.” 2 Tim. 3:1-5.

Talaka zinaongezeka, uhalifu, ukahaba. Kuongezeka kwa washiriki wengi kanisani wakati hali ya kiroho inashuka, dhuluma.

G. Kutafuta anasa.

“Siku za mwisho… watu watakuwa… wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu.” 2 Tim. 3:1-4.

Dunia imechanganyikiwa kwa kutafuta anasa. Asilimia ndogo sana ya watu huenda kanisani, lakini kumbi za starehe zinafurika.

H. Kuongezeka kwa uhalifu, mauaji na ukatili.

“Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa” Mt. 24:12. “Wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.” 2 Tim. 3:13. “Nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu.” Eze. 7:23.

Ni wazi kabisa ishara hii imetimia. Uhalifu na uvunjaji wa sheria vinaongezeka kwa kasi ya kutisha.

I. Matetemeko yenye kuleta uharibifu, dhoruba, na njaa.

“Kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali.” Lk. 21:11.

Matetemeko, tufani, mafuriko, n.k. vinaongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea. Teluthi ya wakazi wa dunia wana njaa na maelfu hufa kwa njaa kila siku. Magonjwa yasiyotibika yanatishia dunia.

J. Ujumbe maalum kwa ulimwengu katika siku za mwisho kabisa.

“Habari Njema ya Ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” Mt. 24:14.

Ujumbe wa Onyo Kuu la Mwisho juu ya kuja kwa Kristo mara ya pili unahubiriwa katika Lugha na Kabila zaidi ya 900.

Karibu asilimia 95 ya wakazi wa dunia wanaweza kuupata ujumbe huu. Kabla ya kurudi kwa Yesu kila mtu duniani atakuwa amekwisha kuonywa juu ya kurudi kwake upesi.

K. Kugeukia Umizimu.

“Nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.” 1 Tim. 4:1. “Hizo ndizo roho za mashetani.” Ufu. 16:14.

Leo hii watu wengi, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya Viongozi wa Mataifa, wanatafuta ushauri kwa wapiga bao na wenye mizimu. Umizimu umevamia makanisa pamoja na fundisho la uongo juu ya kutokufa kwa roho. Biblia inafundisha kuwa wafu, wamekufa.

11. Je, kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia kiasi gani?

“Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.” Mt. 24:32-34.

Biblia iko wazi katika jambo hili. Ishara karibu zote zimetimia. Hatuwezi kuijua siku wala saa ya kurudi kwa Kristo (Mt. 24:36), lakini tunaweza kuwa na uhakika kuwa sisi ndio watu tutakaoishi na kumwona Yesu akirudi.

12. Shetani anasema uongo mwingi juu ya kurudi kwa Yesu mara ya pili, pamoja na maajabu na miujiza, atawadanganya wengi. Nitahakikishaje kuwa sidanganyiki?

“Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara.” Ufu. 16:14. “Nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.” Mt. 24:24. “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” Isa. 8:20.

Shetani amebuni mafundisho mengi ya uongo juu ya kuja kwa Yesu mara ya pili na anawadanganya mamilioni kuwa amekwisha kuja au atakuja kwa namna ambayo haitajwi kwenye Biblia. Lakini Yesu amekwisha kutuonya juu ya mbinu za Shetani, akisema, “Angalieni mtu asiwadanganye” (Mt. 24:4).

13. Ninawezaje kuhakikisha kuwa nitakuwa tayari wakati Yesu atakaporudi?

“Ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.” Yn 6:37. “Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.” Yn 1:12. “Nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mioyo yao nitaziandika.” Ebr. 8:10. “Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” 1 Kor. 15:57.

Yesu anasema, “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.” Ufu. 3:20.

Kwa njia ya Roho Mtakatifu na dhamiri yangu, Yesu anabisha na kuomba aingie moyoni mwangu ili anibadilishe. Kama nitampa maisha yangu yote, atazifuta dhambi zangu zote (Rum. 3:25) za nyuma na kunipa uwezo kuishi maisha matakatifu (Yn. 1:12).

14. Yesu anatuonya sana juu ya hatari gani kubwa?

“Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.” Mt. 24:44. “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulaf, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo.” Lk. 21:34. “Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” Mt. 24:37.

Kuna hatari kubwa ya kuzama katika mahangaiko ya maisha haya au anasa za dhambi na kuja kwa Yesu kukatujia kama Gharika wakati wa Nuhu na kutushitukiza, tukiwa hatuko tayari na kupotea. Ndivyo itakavyokuwa kwa mamilioni ya watu.

Je, itakuwaje kwako? Yesu anarudi upesi sana katika siku tunazoishi sasa. Je, uko tayari? Hakuna jambo la muhimu kama hili.

Je, unaamua kujiandaa ili uwe tayari siku Yesu atakaporudi?

Je, uko tayari kufungua moyo wako ili Yesu aingie na kukubadilisha ili uwe mmoja kati ya watu atakaokuja kuwachukua?

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15

bottom of page