top of page
Yachunguzeeni.png
Somo-1-Cover-Pic-278x300.png

01. Barua Toka Kwa Mungu

Tumwamini nani?

Hili ndilo swali linaloulizwa na karibu kila mtu hapa duniani. Ni nani asemaye ukweli. Kila mahali umejaa udanganyifu, dhuluma, rushwa, uonevu, vita, n.k. Tunatoka wapi? na tuko wapi? na tunakwenda wapi? Ni nani anayeweza kutuambia ukweli?

Kwa bahati nzuri Mungu, aliyeumba vitu vyote, anayejua kila kitu, na anayeweza kila kitu, ametuandikia barua ya kututoa mashaka. Mungu mwenyewe anajibu maswali yetu yote katika barua hiyo. Barua hiyo inaitwa Biblia.

Biblia siyo mkusanyiko wa mawazo ya wanadamu. Waandishi wake waliongozwa na Roho Mtakatifu.

1. Biblia yenyewe inajishuhudiaje?

“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” 2 Tim. 3:16.

“Unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho takatifu.” 2 Pet. 1:21. “Maandiko hayawezi kutanguka.” Yn. 10:35.

Biblia inajishuhudia kuwa imevuviwa, iliandikwa na watu walioongozwa na Roho Mtakatifu, na haiwezi kutanguka wala kukosolewa.

2. Je, Mungu ana uwezo gani unaomfanya kuwa mkuu kuliko miungu mingine?

“Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; Mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.” Isa. 46:9-10.

3. Ni sehemu zipi za Biblia ambazo Yesu alizitumia katika mafundisho yake?

“Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.” Lk. 24:27.

Torati ya Musa, yaani vitabu 5 vya kwanza katika Biblia.

Manabii, yaani, Isaya, Yeremia, Ezekieli, Yoshua, Samweli, Wafalme, Waamuzi na manabii wadogo 12. Maandiko ya Agano la Kale yamegawanywa katika sehemu kuu tatu – Torati, Zaburi, na Manabii.

4. Je, Agano la Kale linazungumza habari za nani?

Yesu akajibu, akawaambia, “Mwayachunguza Maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.” Yn 5:39.

“Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.” Luka 24:44.

Zingatia: Wakati wa Yesu, Agano Jipya lilikuwa halijaandikwa. Maandiko yaliyokuwapo ni Agano la Kale peke yake.

5. Kwa nini mambo yaliyowapata wazee wa zamani yaliandikwa?

“Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofkiliwa na miisho ya zamani.” 1 Kor. 10:11.

“Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini.” Rum. 15:4.

Mungu alitegemea kwamba, kwa kujifunza matukio ya Biblia, tungeweza kuuelewa vizuri zaidi upendo wake na namna anavyojishughulisha na wanadamu.

6. Je, kujifunza Maandiko kunatusaidiaje?

“Na ya kuwa tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” 2 Tim. 3:15,16,17.

7. Je, Yesu alisema tunaweza kuupata wapi ukweli?

“Uwatakase kwa ile kweli; Neno lako ndiyo kweli.” Yn. 17:17.

Wanadamu hawaujui ukweli na wengi wao hawajui kuuelezea. Ndiyo maana kuna taabu na shida nyingi zisizo na ufumbuzi.

Biblia inasema, “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Yn 8:32

8. Je, Yesu aliwaambia Masadukayo walikuwa wanapotea kwa sababu gani?

“Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui Maandiko wala uweza wa Mungu.” Mt. 22:29.

9. Ni kwa nini mtu wa jinsi ya mwili hawezi kuyaelewa Maandiko?

“Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” 1 Kor. 2:14.

10. Je, Yesu alisema ni nani atakayetuongoza na kututia katika kweli yote?

“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” Yn 16:13.

Biblia inatuambia “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na Upanga wa Roho ambao ni Neno la Mungu” (Efe. 6:17).

Hatuwezi kuujua ukweli wa mipango ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu kama Roho hatatuongoza katika kuisoma Biblia na kututafsiria yale aliyowavuvia waandishi kutuandikia.

11. Mtume anatuambia nini juu ya Biblia?

“Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.” 2 Tim. 2:15.

Siyo kusoma tu. Tujitahidi! mpaka tuonekane kuwa tumekubaliwa na Mungu. Inahitajika jitihada ili tuyaelewe mambo ya kina katika Neno la Mungu.

12. Waberoya walisifwa kwa jambo gani?

“Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Tesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza Maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.” Mdo. 17:11.

Waliyachunguza Maandiko kila siku, ili waone kama waliyokuwa wameyasikia yalikuwa sahihi au la. Leo hii kama kila mtu angechunguza Maandiko aone kama yale anayofundishwa kanisani ni sahihi au la, kungekuwa na mabadiliko makubwa katika Ulimwengu wa Kidini. Si wengi wanaopenda kuiga mfano wa Waberoya. Hebu tufanye agano na Mungu kwamba tutatumia njia hiyo hiyo kuutambua ukweli.

13. Je, Biblia inaulinganisha na nini msaada tunaoupata kutokana na kujifunza Biblia?

“Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.” Zab. 119:105.

14. Tutafanyaje ili tusitende dhambi?

“Jinsi gani kijana aisafshe njia yake? Kwa kutii, akilifuata Neno lako.” Zab. 119:9.

Je, Unabii unathibitishaje kama Biblia imevuviwa?

Biblia inasema

“Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.” Isa. 42:8,9.

“Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yango.” Isa. 46:9,10.

Utabiri wa Biblia juu ya mambo ambayo yangetokea baadaye, unathibitisha uvuvio wa Biblia, mambo hayo yanapotokea.

“Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofkiliwa na miisho ya zamani.”

 

Angalia mifano ifuatayo:

A. Kuinuka na kuanguka kwa falme nne zilizotawala dunia:
Babeli, Umedi na Uajemi, Uyunani na Rumi. (Danieli 2,7,8.)

B. Koreshi kuwa Mpiganaji ambaye angeiteka Babeli. “Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi (mtiwa mafuta) wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofchwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.” Isa. 45:1-3.

C. Baada ya kuangamizwa, Babeli isingekaliwa tena. “Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza.” “Haya! juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu.” (Isa. 13:19,2). “Na Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu, ajabu, na mazomeo, pasipo mtu wa kukaa huko.” Yer. 51:37.

D. Misri kutokuwa na amri tena kati ya Mataifa. “Nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni. Utakuwa duni kuliko falme zote, wala hautajifunua tena juu ya Mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya Mataifa.” Eze. 29:14,15. “Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, BWANA, nimenena neno hili.” Eze. 30:12,13.

E. Majanga ya kushtua dunia na hofu kadiri tunavyoelekea siku za mwisho. “Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya Mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika.” Lk. 21:25,26.

F. Kuporomoka kwa maadili katika siku za mwisho. “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako na nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio saf, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.” 2 Tim. 3:1-5.

G. Unabii juu ya matukio katika maisha ya Yesu. “Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.” Lk. 24:27. “Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya Maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.” Mdo. 18:28. Kwa kuwa wakati huo Agano Jipya lilikuwa halijaandikwa, ni wazi kuwa Maandiko yanayozungumziwa hapa ni Agano la Kale. Utabiri wa Agano la Kale juu ya Masihi ulikuwa dhahiri na ulitimizwa na Yesu wa Nazareti kiasi cha kumfanya Yesu mwenyewe na Apolo kuutumia kuwathibitishia Wayahudi kuwa Yesu alikuwa ndiye Masihi.

           Unabii                              Maandiko ya Agano la Kale             Kutimia katika Agano Jipya

Kuzaliwa Bethlehemu                                       Mika 5:2                                    Mt. 2:1

Kuzaliwa na Bikira                                              Isa. 7:14                               Mt. 1:18-23

Kuwa wa ukoo wa Daudi                                   Yer. 23:15                               Ufu. 22:16

Jaribio la kuuawa na Herode                              Yer. 31:15                             Mt. 2:16-18

Kusalitiwa na rafki                                               Zab. 41:9                         Yn. 13:18,19,26

Kuuzwa kwa vipande 30 vya fedha                    Zek. 11:12                           Mt. 26:14-16

Kusulibiwa                                                           Zek. 12:10                       Yn. 19:16-18,37

Nguo zake kupigiwa kura                                     Zab. 22:18                            Mt. 27:35

Kutokuvunjwa mifupa                                    Zab. 34:2; Kut. 12:46               Yn. 19:31-36

Kuzikwa katika kaburi la tajiri                                 Isa. 53:9                         Mt. 27:57-60

Mwaka, Siku, na Saa ya kifo chake              Dan. 9:26,27; Kut. 12:6             Mt. 27:45-50

Kufufuka siku ya tatu                                              Hosea 6:2                        Mdo. 10:38-40

Moja kati ya uthibitisho mkuu kwamba Biblia si kitabu cha kawaida tu kilichoandikwa na watu wema, ni uwezo wake wa kubadili maisha ya watu. Inaweza kumbadilisha mtu mwovu kabisa na kumfanya kuwa Mkristo mwaminifu. Inaweza kumfanya mtu asiye mwaminifu, kutaka kurejesha alichochukua, au kusahihisha uongo aliosema. Ni uwezo gani wa ajabu ulio katika kitabu hiki unaobadilisha kiajabu matamanio na makusudi ya watu? Ni uwezo wa kufanya miujiza wa Roho wa Mungu anayefanya kazi kupitia kitabu hiki kutuonyesha Mwana–Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu.

Je, ungependa kuielewa Biblia vizuri zaidi?

Je, utatenga muda maalum kila juma kwa ajili ya kujifunza Biblia? Kwa kutambua kwamba Biblia ni barua ya Mungu inayokueleza mapenzi yake, je, unakusudia kuishi sawasawa na neno lake kama asemavyo katika Biblia?

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15

bottom of page