top of page

UKWELI ULIOPOTOSHWA KUHUSU JEHANAM

hell-on-earth-large.jpg

Mojawapo ya masomo ya kitheolojia katika Biblia linalowafanya watu kuchanganyikiwa vibaya sana ni lile la Jehanum.  Limepapaswa-papaswa tu na wachungaji na mapadiri na kupotoshwa maana yake na walei [waumini wa kawaida] mpaka neno hilo limegeuka na kujulikana sana kama tusi na kiapo cha kawaida.  Kila mahali watu wanauliza maswali yale yale.  Jehanum ni nini na iko wapi? Mwisho wa waovu ni upi?  Je, Mungu mwenye upendo atawatesa watu vibaya sana milele hata milele? Je, mioto ile ya Jehanum itauchoma uovu uliomo ndani ya wenye dhambi milele hata milele? 


     Hayo ndiyo maswali yanaostahili kupewa majibu kamili ya Biblia, na yale mabishano  yaliyopo juu ya somo hilo yasingepaswa kutukatisha tamaa katika kuifunua kweli yote kama ilivyo katika Kristo.Kwanza kabisa, tunahitaji kuelewa kwamba iko mbingu ya kuipata na jehanum ya kuikwepa.  Yesu alifundisha kwamba kila mtu, ama ataokolewa, ama atapotea.  Hakuna mahali pa katikati pa kusimama, wala hakuna tuzo [zawadi] zitakazotolewa mara ya pili.  “Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,
na kuwatupa katika tanuru ya moto;  ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.  Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao.”  Mathayo 13:41-43. 


     Kwa kuzingatia hatima hizo mbili kwa watu wote waliopata kuzaliwa [hapa duniani], sisi
tungekuwa na bidii nyingi jinsi gani katika kuitafuta njia ile ya kweli.  Kristo alisema,  “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima.”  Usalama kamili peke yake kwa mtu ye yote ni kuchukua kwa usahihi kile alichofundisha Yesu juu ya Jehanum.  Fundisho lake ndilo peke yake linaloweza kutegemewa kabisa na ndilo la kweli.  Alisema kwamba wengine watatupwa motoni, na wengine watang’aa katika ufalme wake.


     Ni jambo lisilo la kawaida kwa kiasi fulani, Kristo ameshtakiwa na viongozi wengi wa dini wamba anafundisha uongo juu ya somo hilo.  Wamemshtaki kwamba anafundisha kuwa roho isiyokufa inaruka na kwenda zake kutoka katika mwili wakati mtu anapokufa, ama inakwenda mbinguni, ama jehanum.  Hayo siyo aliyofundisha Kristo hata kidogo.  Kamwe hakutoa dokezo lo lote kwamba roho fulani isiyo na mwili hujitenga na mwili wakati mtu anapokufa.  Na kwa hakika hakutoa wazo lo lote kuonyesha kwamba waovu hupata mateso makali milele na milele mara tu wanapokufa. 


     Hebu sasa na tupate mfano mmoja kuhusu kile Yesu alichofundisha hasa juu ya somo hili la jehanum.  “Na mkono wako ukikukosesha, ukate;  ni afadhali kuingia katika ufalme u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum.  Marko 9:43.  Maneno hayo ya Bwana  yanathibitisha bila kuacha kivuli cho chote cha mashaka kwamba ni mwili unaokwenda motoni, wala siyo roho fulani isiyoonekana.  Katika Mathayo 5:30 alizungumza juu ya “mwili   …  mzima” usitupwe jehanum.  Hii humaanisha mikono, miguu, macho, na sehemu zote nyingine za mwili huu unaoonekana.


     Kinyume cha fundisho hilo la Kristo, mimbara za [wahubiri wa] siku hizi huvumisha habari zinazotoa picha za kusisimua za roho zinazofikirika tu ambazo huuacha mwili huu mtu anapokufa  - yaani, roho zisizokuwa na mwili wala umbo lo lote.  Mtazamo huo, japo unaweza kupendwa sana na watu wengi, ni kinyume na yale aliyofundisha Yesu.  Zingatia vema, maana yule Bwana aliye Mwalimu Mkuu alisema tena na tena katika vitabu vya Injili  -  ya kwamba wale wanaotupwa katika moto wa jehanum watakwenda mle wakiwa na MIKONO, MIGUU, MACHO na viungo vyote vya mwili.  Hawatakwenda katika hali fulani ya nafsi iliyo nyepesi kama hewa ambayo haina umbo lo lote au kama roho.

 
     Sasa tuko tayari kuyachunguza mambo makuu manne ya kweli toka katika Biblia ambayo huulizwa juu ya hatima ya [mwisho wa] waovu.


 
ADHABU HUTOLEWA BAADA YA HUKUMU 

     Ukweli muhimu wa kwanza juu ya jehanum ni huu:  WALE AMBAO HAWAJAOKOLEWA HAWAENDI MAHALI KO KOTE AMBAKO WANAPEWA ADHABU MARA TU  WANAPOKUFA, BALI WANALINDWA KABURINI MPAKA SIKU YA HUKUMU
WATAKAPOPEWA ADHABU YAO.  Kristo aliufundisha waziwazi ukweli huo katika mfano 
unaojulikana sana wa ngano na magugu.  Baada ya mwenye nyumba kupanda ngano katika shamba, mtumishi wake akaja na kutoa taarifa kwamba magugu yalikuwa yanaota miongoni mwa ngano.  Swali lake likawa kwamba, je, ayang’oe magugu yale wakati yakiwa bado machanga sana.  Jibu la mwenye nyumba lilikuwa ni hili,  “La;  msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.  Viacheni vyote vikue hata WAKATI WA MAVUNO;  na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao,  Yakusanyeni  kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome;  bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.” Mathayo 13:29,30.


     Basi hebu na uyafuatilie maneno yake Kristo anapoeleza maana ya mfano huo:  “Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu [Kristo];  lile konde [shamba] ni ulimwengu;  zile mbegu njema ni wana wa ufalme;  na yale magugu ni wana wa yule mwovu;  yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi;  mavuno ni mwisho wa dunia;  na wale wavunao ni malaika.  Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni;  ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia [sio sasa mtu anapokufa].  Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto;  ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.” Mathayo 13:37-43.   


     Hakuna awezaye kuufanya mfano huo uwe rahisi zaidi kwa kuyapanua yale aliyosema Yesu.  Uko wazi mno hata mtoto mdogo anaweza kuuelewa.  Alisema kwamba yale magugu yaliwawakilisha waovu na ya kwamba wangetupwa motoni “katika mwisho wa dunia.”  Ilikuwa ni wakati wa mavuno ambapo kazi ile ya kutenganisha ingefanyika, na yeye alisema waziwazi kwamba “mavuno ni mwisho wa dunia.”  Yawezekanaje basi, kwa mtu ye yote kuyaelewa vibaya maneno hayo ya Kristo?  Wazo zima la waovu kwenda motoni wanapokufa linapingana na mafundisho dhahiri ya Bwana wetu yasemayo kwamba watatupwa motoni katika mwisho wa dunia.

 
     Kwa kuwa hukumu [adhabu] yao pia inatokea baada ya Kristo kuja, basi, tunaweza kuona jinsi ambavyo ingekuwa vigumu kabisa kwa mtu ye yote kuadhibiwa kabla ya wakati ule.  Haki inadai kwamba mtu aletwe hukumuni kabla ya kuadhibiwa kwake.  Petro anatangaza, anasema,  “Basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa katika majaribu, na kuwaweka wasio haki hata siku ya hukumu ili wapate kuadhibiwa.”  2 Petro 2:9, KJV.  Je, hilo linaleta maana, au sivyo?  Hebu tuseme mtu mmoja angeletwa mahakamani akishtakiwa kuiba, na hakimu aseme, “Mwekeni mbali kwa miaka kumi; baada ya hapo tutaendesha kesi yake.”  Hebu sikiliza, hata hakimu wa kibinadamu asingekuwa hana
haki kiasi hicho!  Angeshtakiwa kwa kitendo hicho.  Hakika Mungu asingekuwa na hatia ya kufanya upuzi kama huo. Tukiiruhusu Biblia itupe maana ya kile isemacho, basi, hapawezi kuwapo na shaka lo lote katika suala hili.  Waovu “wanawekwa” mpaka lini?  Mpaka “siku ya hukumu.”  Ili wafanywe nini?  Ili wapate kuadhibiwa!  Hii humaanisha kwamba hawawezi kuadhibiwa kabla ya siku ile ya hukumu.  

 

Je, hivi Biblia inatueleza sisi mahali wanapowekwa mpaka wakati ule?  Kristo mwenyewe alisema,  “Msistaajabie maneno hayo;  kwa maana saa yaja, ambayo watu WOTE waliomo makaburini wataisikia sauti yake.  Nao watatoka;  wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.”  Yohana 5:28,29.

 
     Jambo hilo ni dhahiri jinsi gani!  Yesu alisema kwamba wema na wabaya watatoka MAKABURINI MWAO kupokea, ama uzima, ama adhabu ya kutengwa na Mungu milele.  Hilo huonyesha kwamba kuanzia wakati ule wanapokufa hadi wanapotoka katika ufufuo hawapokei thawabu, wala adhabu yoyote.  Yote hayo hutokea wakati ule wanapotoka mle.  Wanawekwa mpaka siku ile kama vile Petro alivyodokeza, ila Kristo alionyesha waziwazi ni wapi watakapowekwa  -  “makaburini.” 


     Endapo yanahitajika maneno yaliyo wazi zaidi ya hayo, basi, msikilize Yesu asemapo maneno haya katika Luka 14:14:  “Utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.”  Au msikilize tena asemavyo katika Mathayo 16:27, “Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake;  ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.”  Ni lini itakapokuwa hiyo “ndipo”?  Atakapokuja na malaika zake.  Hakuna zawadi au thawabu inayotolewa kwa mtu mpaka katika ufufuo wa wenye haki, atakapokuja na malaika zake wote.  Mafungu hayo yanauvunjilia mbali ubishi wote.  Yakichukuliwa katika aya zake, hayana shaka lo lote juu ya maana yake, wala hayana maana iliyojificha.


     Tena Kristo ananukuliwa akisema hivi katika sura ile ya mwisho kabisa ya Biblia,  “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.”  Ufunuo 22:12.  Hapo anatukumbusha sisi kwamba “kila mtu” – yaani, kila mtu binafsi  -  atapokea ujira wa haki wakati ule Kristo atakaporudi duniani.  Ayubu alitangaza “kwamba mwovu huwekwa hadi siku ya maangamizi.  Watatoka katika siku ile ya ghadhabu.”  Ayubu 21:30, KJV.  Danieli aliandika kwamba hao “walalao katika mavumbi ya nchi wataamka [watafufuka], wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.”  Danieli 12:2. 


     Je!  linaweza kuwapo shaka lo lote kuhusu mahali wanapowekwa waovu kabla ya kukabili ufufuo, hukumu, na adhabu yao?  Sisi tunao ushuhuda wa Petro, Danieli, Ayubu, na Bwana mwenyewe.  Hakuna nafasi ya kukwepa suala hili la msingi.  Wanawekwa kaburini.


     Sasa tunalifikiria jambo kuu la pili la kweli kuhusu jehanum:  HAKUNA YE YOTE MIONGONI MWA WALE AMBAO HAWATAOKOLEWA ATAKAYETUPWA KATIKA MOTO WA  JEHANUM MPAKA BAADA YA KUJA KWA YESU MARA YA PILI KATIKA MWISHO WA DUNIA.  Japokuwa tumekwisha kuona tayari ushahidi thabiti juu ya pointi hii, hebu na tuangalie ushahidi zaidi.  Akiwa anaeleza juu ya adhabu ya waovu, Yohana aliandika hivi:  “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti.  Hii ndiyo mauti ya pili.”  Ufunuo 21:8.

 

 

HAKUNA MAUTI YA PILI KABLA YA UFUFUO


     Hapo ndipo wale waliopotea wanaonekana katika mioto ya jehanum, wakipata adhabu yao kwa ajili ya dhambi zao.  Na adhabu hiyo ni nini?  “Mauti ya pili,”  asema Yohana.  Je, unatambua jambo hilo  kwamba linathibitisha nini juu ya waovu?  Linathibitisha kwamba hawatatupwa katika ziwa lile liwakalo moto na kiberiti [jehanum] mpaka baada ya ufufuo wao kutokea.  Watu hao wanakufa mauti  ya pili katika moto huo, lakini hawawezi kupatwa na mauti ya pili mpaka wapewe uhai wao mara ya pili [wafufuliwe].  Waliishi maisha yao ya kwanza katika dunia hii na kufa mauti ya kwanza, wakaingia kaburini mwao.  Kabla hawajafa mauti ya pili ni lazima wafufuliwe  -  ni lazima wapewe  uhai mara ya pili.  Hilo, kusema kweli, ndilo hasa linalotokea mwisho wa dunia.  Yesu alisema,  “Watu wote waliomo makaburini watatoka.”  Basi, baada ya kupata uzima wao mara ya pili katika ufufuo , ndipo waovu hao watakapoadhibiwa kwa dhambi zao katika moto wa jehanum, “hii ndiyo mauti ya pili” [mshahara wa dhambi – Rum. 6:23].  Pamoja na hayo, mauti ya pili ni ya mwisho, yaani, ni mauti ya milele ambayo kutokana nayo hapatakuwa na ufufuo kwao.  Lakini jambo la kulizingatia ni wakati itakapotolewa hiyo adhabu ya moto wa jehanum  -  ni baada ya ufufuo katika mwisho wa dunia. Haitokei wakati wa mauti ya kwanza [inayowapata wema na waovu – Ebr. 9:27] kama wengi mno walivyoshawishiwa kuamini.


     Je, hivi Biblia inatueleza namna watakavyotupwa waovu katika lile ziwa  la moto?  Naam, inatueleza.  Yohana anaeleza matukio ya kusisimua yanayotokea mwisho wa ile milenia [miaka elfu moja].  “Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;  naye atatoka na kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.  Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa [Yerusalemu Mpya].  MOTO [wa Jehanum] UKASHUKA KUTOKA MBINGUNI, UKAWALA.”  Ufunuo 20:7-9. 


     Hapo tunaona kwamba katika mwisho wa ile milenia waovu wote waliopata kuishi [katika dunia hii] watatoka katika ufufuo ule wa pili.  Baada ya kueleza jinsi wenye haki watakavyokuwa hai na kutawala na Kristo katika kipindi kile cha miaka elfu moja, Yohana aliandika, akasema,  “Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.”  Ufunuo 20:5.  Wafu waliosalia, kusema kweli, walikuwa ni wale waovu, na ufufuo wao utampa Shetani nafasi ya kuendeleza vita yake dhidi ya Mungu na watakatifu wake.  Anatoka kwenda kuyakusanya majeshi ya wale waliopotea ambao wamefufuliwa kutoka katika wafu.  Anao watu wa kuwadanganya tena, naye anawahakikishia ya kwamba wanaweza kuushinda Yerusalemu Mpya ambao umeshuka chini kutoka mbinguni kwa
Mungu (Ufunuo 21:2).  Wanapotembea kijeshi na kuuzingira mji ule, waovu wale ghafula
wanakatiliwa mbali [wanauawa] na moto ule ulao ambao unanyesha juu yao toka mbinguni.  HUO NDIO MOTO WA JEHANUM AMBAO NDIO ADHABU YA MWISHO KWA DHAMBI.

bottom of page