JEHANAM ILIWEKWA KWA AJILI YA NANI
Jambo la mwisho, sisi tungeshangilia sana kwa sababu jehanum kamwe haikuwekwa kwa ajili yako wewe, wala kwa ajili yangu mimi. Yesu alisema kwamba “aliwekewa tayari Ibilisi na malaika zake” (Mathayo 25:41). Kama sisi tutajikwaa na kuangukia katika moto ule, litakuwa ni kosa letu kubwa mno tuliloweza kulifanya. Ungeweza kwenda kule kwa kuukanyaga mwili wa Yesu Kristo uliopondeka kwa ajili yako [Ebr. 10:26-31], tena ungeweza kwenda huko, bila kujali upendo wa Baba, maombezi ya Roho Mtakatifu, na mvuto wa mbinguni wa mamilioni ya malaika. Swali lisilojibika kabisa ulimwenguni kote ni hili: “Sisi je! tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii?” Hakuna jibu kwa sababu sisi hatuwezi kupona isipokuwa kwa njia yake Kristo na msalaba wake.
Hakuna mtu ye yote atakayepotea ati kwa kuwa tu alitenda dhambi, kwa sababu kila mmoja ametenda dhambi. Hakuna atakayeachwa kwenda mbinguni ati kwa sababu alisema uongo, aliiba, au alizini. Sababu peke yake itakayomfanya mtu ye yote apotee ni ile ya kukataa kuipa kisogo [kuachana na] dhambi yake na kujitupa mikononi mwa Mwokozi mwenye upendo ambaye anasimama akiwa tayari kutusamehe na kutusafisha na udhalimu wote [Mithali 28:13]. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili KILA MTU AMWAMINIYE ASIPOTEE [ASIANGAMIE], BALI AWE NA UZIMA WA MILELE.” Yohana 3:16.