top of page

JE MOTO WA JEHANAM HAUTAZIMIKA MILELE

hell-on-earth-large.jpg

Zipo sababu kadhaa zinazotufanya kuwa na hakika kabisa juu ya suala hilo.  Kwanza kabisa, dunia hii pia inatangazwa kuwa itakuwa ndiyo makao ya mwisho ya wenye haki.  Yesu alisema,  “Heri wenye upole;  maana hao watairithi nchi.”  Mathayo 5:5.  Petro, baada ya kueleza habari za dunia hii ikilipuka kwa mshindo mkuu na kuteketea, aliona nchi mpya imejazwa na haki.  “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.”  2 Petro 3:13. 


     Waovu hawawezi kuendelea kuishi katika sayari hii kwa sababu imeahidiwa, hasa ikiwa katika ukamilifu wake wote, kuwa itakuwa kwa ajili ya uzao wa kiroho wa Ibrahimu (Rum. 4:13).  Baada ya kutakaswa kutokana na laana yake yote ya dhambi, itarudia tena katika hali ile ya milki [enzi] ya kwanza, na kulandana kabisa na mpango wa kwanza wa Mungu kwa nchi hiyo.  Hatimaye itakuwa kama vile Mungu alivyokusudia iwe  -  yaani, itakuwa makao makamilifu kwa ajili ya watu wake walio wakamilifu.


     Pili, waovu hawawezi kuendelea kuishi katika dunia hii kwa sababu hawajapata kamwe 
kumtegemea Kristo kwa uzima wao wa milele.  Ni wale wenye haki tu wanaopokea karama ya uzima wa milele.  “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”  Yohana 3:16.  Lakini, je!  ni vipi kwa wale wasiomwamini?  Hakika wataangamia.  Biblia inasema,  “Mshahara wa dhambi ni mauti.”  Warumi 6:23.  Tafadhali usikose kuielewa maana iliyoelezwa kwa urahisi katika mafungu hayo.  Waovu kamwe hawaahidiwi kupewa uzima.  Wanaahidiwa kupewa mauti  -  yaani,  mauti ya milele.  Ni wale wenye haki tu wanaoahidiwa kupewa uzima  -  yaani, uzima wa milele. 


     Lakini basi, kuna njia moja tu ya kuupata uzima usio na mwisho, na njia hiyo ni kwa imani katika Yesu.  Yohana anaielezea kwa njia hii:  “Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele;  na uzima huu umo katika Mwanawe.  Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima;  asiye naye  Mwana wa Mungu hana huo uzima.”  1 Yohana 5:11,12.  Hebu na nikuulize swali:  Je!  waovu wale katika ziwa lile la moto wanaye Mwana wa Mungu?  Hasha.  Basi, wangewezaje kuwa na uzima?  Yohana anasema,  “Nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.”  1 Yohana 3:15.  Je!  wauaji wale walio katika ule moto wa jehanum wataendelea kuwa hai milele? Hasha.

 
     Ungekuwa ni uzushi wa daraja la juu kabisa kuamini kwamba uzima wa milele ungeweza kupatikana toka katika chimbuko jingine lo lote zaidi ya Yesu.  Je, waovu hao wangeupata wapi?  Paulo anatangaza kwamba ni Yesu Kristo aliye“ufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili.”  2Timotheo 1:10.  Maandiko yaliyovuviwa hayafunui chimbuko jingine lo lote la luzima wa milele isipokuwa kwa njia ya Injili ya Kristo.  Fungu linapatikana wapi katika Biblia linaloeleza kwamba wanaweza kupewa uzima wa milele wale walio waovu?  Waweza kusoma mara nyingi kuhusu wenye haki wakiupokea, lakini kamwe sio yule asiyeamini. 


     Paulo alisema,  “Angalieni, nawaambia ninyi siri;  hatutalala [hatutakufa] sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho;  maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.  Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.”  1 Wakorintho 15:51-53.


     Mafungu hayo yanasema habari za kikomo fulani katika wakati ambapo wenye haki 
watabadilishwa na kuwa viumbe wasiokufa.  Wakati ule bado uko mbele.  Unatokea Yesu arudipo, wakati wa parapanda ile ya mwisho, ufufuo utakapotokea.  Hakuna mahali po pote katika Biblia tunaposoma kwamba waovu watabadilishwa kwa njia kama hiyo.  Na hasa ni kwa sababu wao hawaipokei karama hiyo ya uzima wa milele, basi, hawawezi kuendelea kuishi katika ziwa lile la moto.


     Ni wazo la kushangaza sana na lisilo na maana kuzua uongo kuhusu tukio hilo.  Liko kinyume kabisa na Biblia, tena linachukiza sana mawazoni.  Ezekieli alitangaza, alisema,  “Roho ile itendayo dhambi itakufa.”  Ezekieli 18:4.  Haidhuru sisi tueleweje juu ya hiyo roho ilivyo, hebu na tuikubali kweli hii ya Biblia iliyo rahisi kueleweka isemayo kwamba roho inaweza kufa kama matokeo ya dhambi.


     Kama waovu wanaishi milele katika ule moto, basi, wanacho kitu kile kile walicho nacho wenye haki [yaani, uzima wa milele], isipokuwa wao wako mahali tofauti.  Ni nani ambaye angeweza kuwapa huo uzima wa milele, kama siye Kristo peke yake?  Yohana 3:16 analimaliza suala hilo kwa wazi na kirahisi mno.  Wale wasiomwamini Mwana pekee WATAPOTEA [WATAANGAMIA].  Watakufa.  Watapatikana na MAUTI YA PILI  -  yaani, mauti ya mwisho, mauti ya milele ambayo kutokana nayo hawataweza kufufuliwa kamwe.  Ni adhabu isiyo na mwisho, adhabu ya milele, kwa sababu ni mauti siyo na mwisho, yaani, mauti ya milele.


 
MOTO USIOZIMIKA


 
     Mmoja anaweza kuzusha swali hili:  Ni vipi basi, kuhusu ule moto usiozimika ambao unawachoma waovu hao?  Je, haimaanishi kwamba hautazimika kamwe?  Kwa kweli, haimaanishi hivyo.  Kuzima maana yake ni kukizuia kitu kinachowaka kisiendelee kuwaka.  Hakuna atakayeweza kuizima mioto ile ya jehanum.  Huo ndio moto wa ajabu wa Mungu.  Hakuna hata mmoja atakayejiokoa kutoka katika moto huo kwa kuuzima.  Isaya anasema hivi juu ya moto huo,  “Tazama, watakuwa kama mabua makavu;  moto UTAWATEKETEZA;  hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto;  hautakuwa kaa la 
kukota moto, wala moto wa kukaa karibu nao.”  Isaya 47:14.  Baada ya kumaliza kazi yake, moto huo utazimika.  Hakuna awezaye kujiokoa mwenyewe na mwali wake kwa kuuzima, ila hatimaye hakuna kaa la kukota litakalobakia.  Hivyo ndivyo yasemavyo Maandiko. 


     Yeremia alitabiri kwamba Yerusalemu utateketezwa kwa moto ambao usingeweza kuzimwa (Yer.17:27), lakini uliteketezwa na kuwa majivu (2 Nya. 36:19-21).  Soma mafungu hayo na kuona jinsi Biblia inavyolitumia neno hili “kuzima.”  Halina maana ya moto usioweza kuzimika kamwe.  Lina maana ile tu lisemayo, “usiozimika.”  Hauwezi kuzimwa na mtu ye yote. Twaweza kusema nini, basi, juu ya maneno haya “milele” na “kuendelea pasipo kukoma” ambayo yanatumika kuelezea moto huo wa jehanum?  Hakuna utata wo wote kabisa, au kinyume chake, wakati tunapoiacha Biblia yenyewe kutoa maelezo ya maneno yale yaliyotumika ndani yake.  Neno hilo ni mfano wa kitu gani?  Wengi hufanya kosa la kutumia maelezo ya siku hizi kuyafafanua maneno ya Biblia bila kuyahusisha na matumizi yake ya zamani ya aya zile zinazohusika (contextual usage).
Jambo hilo hukiuka mojawapo ya kanuni za msingi za kufasiri Maandiko.


     Ukweli ni kwamba moto wa milele hauna maana ya moto ambao hautazimika kamwe.  Usemi uo huo umetumika katika Yuda 7 kuhusu maangamizi ya Sodoma na Gomora.  “Kama vile Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa kwa “moto wa milele.”


     Ni dhahiri ya kwamba Sodoma bado haiendelei kuteketezwa leo.  Bahari ile ya Chumvi (Dead Sea) inapafunika mahali pale iliposimama miji hiyo ya zamani.  Lakini yenyewe iliteketezwa kwa “moto wa  milele,” nasi tunaambiwa kwamba ilikuwa ni mfano (dalili) wa kitu fulani.  Je, ni mfano wa kitu gani?  “Tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya.”  2 Petro 2:6.


     Aha!  maneno hayo!  Yaani, kwamba ule moto wa milele ulioufanya Sodoma kuwa majivu ni mfano wa kile kitakachowapata waovu hatimaye.  Kama fungu hilo linasema kweli, basi, moto ule ule ulioiteketeza Sodoma na Gomora utawateketeza pia waovu katika ziwa lile la moto.  Huo utakuwa ndio moto wa milele.  Je, hii ina maana kwamba utawafanya waovu kuwa majivu pia?  Biblia inasema Ndiyo.  “Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru;  na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi;  na siku ile inayokuja ITAWATEKETEZA, asema BWANA wa majeshi;  hata haitawaachia shina wala tawi  …  Nanyi mtawakanyaga waovu;  maana  WATAKUWA MAJIVU CHINI YA NYAYO ZA MIGUU YENU;  katika siku ile niifanyayo, asema BWANA wa majeshi.”  Malaki 4:1,3.

 
     Hakuna maneno katika lugha yo yote yanayoweza kuyafanya maneno hayo kuwa  na nguvu au kueleweka wazi zaidi.  Moto huo wa milele unateketeza kila kitu milele zote.  Hata SHETANI, ambaye ndiye Shina, hatimaye ATATEKETEZWA KABISA na kuwa majivu [Eze. 28:15-19;  Isa. 14:10-20;  Ufu. 12:7-12].  Ni ulinganifu ulioje huo ya kwamba tunapoiacha Biblia kueleza maneno yake yenyewe ndipo picha kamili inaonekana.  Ni kuchezea maneno kijanja kulikoje huko ambako kungehitajika ili kuweza kuikwepa maana hiyo iliyo wazi ya maneno hayo.  Lakini wale ambao katika maisha yao yote wamekuwa wakipendelea kuyafuata mapokeo [mafundisho ya wanadamu – Mk. 7:113; Mt. 15:1-14]
wanaweza kuyasoma maneno hayo yasemayo, “itawateketeza  …  watakuwa majivu”  
na bado wao wakasisitiza kwamba waovu wangali hai na ya kwamba wanaendelea kuteseka motoni. 


     Hakika, yapo baadhi ya mafungu juu ya somo hili yaletayo utata, lakini tunagundua kwamba hayo yote yanapatana wakati yanapofikiriwa maneno yanayotangulia na yale yanayofuata (context) katika aya nzima, na wakati ule Biblia inapoachwa kujifafanua yenyewe.


     Hata yale maneno ya Kristo katika Mathayo 25:46 hayaleti utata wo wote wakati ule tunapoichukua maana yake ile iliyo dhahiri.  “Na hao watakwenda zao na kuingia katika adhabu ya milele;  bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.”  Wengi wanasumbuliwa na usemi huo wa “adhabu ya milele,” lakini basi, zingatia kwamba hausemi “kuendelea kuadhibiwa milele.”  Si kitu kama adhabu hiyo ni kitu gani, itadumu milele.  Je, Biblia inatuambia sisi kwamba adhabu hiyo ni kitu gani? Ndiyo.  “Mshahara wa dhambi ni MAUTI.”  Warumi 6:23.  Kwa hiyo, Yesu alikuwa anasema tu kwamba mauti hiyo ingedumu milele.  Isingeweza kufikia mwisho wake.  Isingeweza kamwe kukatishwa kwa njia ya ufufuo. 


     Paulo anarahisisha zaidi kwa kusema maneno haya:  “Katika mwali wa moto;  huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;  WATAKAOADHIBIWA kwa  …”  Hebu sikiliza sasa, Paulo atatuambia sisi adhabu hiyo ni kitu gani. “WATAKAOADHIBIWA kwa MAANGAMIZI YA MILELE, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake.”  2 Wathesalonike 1:8,9.  Kwa hiyo, adhabu hiyo ni MAANGAMIZI [MAUTI] YA MILELE  -  yaani, maangamizi [mauti] yanayoendelea milele na milele.  Kutokana na hayo [maangamizi/mauti] hapatakuwa na ufufuo, wala tumaini la uzima.


     Lakini basi, ni vipi kuhusu yule funza asiyekufa?  Wengi wameyasoma maneno hayo ya Yesu juu ya Jehanum, “ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki” (Marko 9:45,46).  Wengine wameyafafanua na kusema kwamba funza huyo ni roho.  Je, hivyo ndivyo Yesu alivyomaanisha? Hakuna po pote katika Biblia palipo na dokezo lo lote lisemalo kwamba roho ni kama funza. 


     Katika mfano huo Yesu alitumia neno “Gehenna” badala ya neno “Jehanum.”  Ilitukia kwamba Gehena palikuwa ni mahali halisi palipokuwa pakiwaka moto nje kidogo tu ya kuta za Yerusalemu. Bila shaka, wale waliokuwa wakimsikiliza Kristo waliweza kuuona moshi ukipanda juu kwa kujipindapinda toka katika lile Bonde la Gehena, ambako mizoga na takataka ziliendelea daima kuchomwa moto.  Endapo kitu cho chote kiliangukia nje ya ndimi za moto zilizokuwa zinateketeza, basi, kililiwa mara moja na mabuu au funza.  Picha dhahiri za matukio ya kuteketezwa kabisa kwa vitu vile zikiwa mbele ya macho yao, Yesu aliutumia ule moto wa Gehena kama kielelezo cha maangamizi kamili yatakayofanywa na moto ule wa Jehanum.  Moto ule ulikuwa hauzimiki kamwe, na funza  daima walifanya kazi yao juu ya mizoga ile  -  hiyo ni picha ya maangamizi kamili.


     Labda fungu linaloeleweka vibaya kwa urahisi kuhusu jehanum ni dokezo la Yohana la moshi unaopanda juu “hata milele na milele” [Ufu. 14:11].  Kwa wale wasioyajua matumizi mengine ya kifungu hicho cha maneno katika Biblia ni kweli yanaweza kuwaletea utata mwingi sana.  Lakini kulinganisha mafungu katika Agano la Kale na Agano Jipya huonyesha kwamba neno hili “milele” limetumika mara 57 katika Biblia kuhusiana na kitu fulani ambacho tayari kimeufikia mwisho wake. Kwa maneno mengine neno hili “milele” sio kila mara lina maana ya “pasipo mwisho.” 


     Mifano mingi inayojulikana ingeweza kutajwa, lakini miwili au mitatu inafaa kuangaliwa.  Katika Kutoka 21, masharti yamewekwa kuhusu sheria ya utumwa.  Mazingira fulani yalihitaji kumtumikia bwana kwa maisha yote ya mtumwa yule.  Katika hali kama zile sikio lake lilitobolewa kwa uma, na Maandiko yanasema hivi,  “Ndipo atamtumikia sikuzote [milele – KJV],” fungu la 6.  Lakini, je, ni kwa muda gani yule mtumwa angeweza kumtumikia bwana wake wa kibinadamu?  Kusema kweli, kwa kadiri tu alivyoendelea kuwa hai.  Kwa hiyo, neno hili “milele” [sikuzote] halikuwa na maana moja tu ya pasipo mwisho.

 
     Hana alimchukua mwanawe Samweli na kwenda naye kwenye hekalu la Mungu, ambako [Samweli] ange“ka[a] huko daima [milele – KJV].”  1 Samweli 1:22.  Lakini katika fungu la 28 tunaambiwa waziwazi kwamba “wakati wote atakaokuwa hai amepewa BWANA.”  Maana ya awali  ya neno hili “milele” huonyesha kwamba ni kipindi cha wakati kisichojulikana.  Kwa kawaida linaeleza kipindi cha wakati ambacho kitu fulani kinaweza kuendelea kuwapo chini ya mazingira yaliyopo.  Hata kukaa kwake Yona katika tumbo la nyangumi kunaelezwa naye kama ni milele.”  (Yohana 2:6). 


     Mtu mmoja anaweza kupinga na kusema kwamba hili pia lingeweza kuwawekea kikomo cha maisha ya wenye haki kule mbinguni, kwa sababu wanaelezwa kama wanamtukuza Mungu milele. Neno ni lile lile linalotumika kwa waliookolewa na kwa waliopotea.  Lakini tofauti kubwa sana ipo katika mazingira yao.  Watakatifu wamepokea karama ya uzima wa milele.  Maisha yao sasa ni sawa na yale ya Mungu.  Uzima wa milele maana yake “kisichoweza kufa.”  Neno hili “milele” likitumika kuhusiana nao lingeweza kuwa na maana ile tu ya “pasipo mwisho,” kwa sababu wao ni raia waliopewa tayari miili isiyokufa [1 Kor. 15:51-54].  Lakini neno hilo “milele” linapotumika kuwaelezea waovu, tunazungumzia habari ya viumbe wale walio na mwili unaokufa ambao wanaweza 

kufa na ni lazima wafe.  “Milele” yao inategemea jinsi miili yao inayokufa inavyoweza kustahimili katika moto ule unaowaadhibu kwa kadiri ya matendo yao. 

ROHO PAMOJA NA MWILI KUANGAMIZWA 

     Jambo hilo hutufikisha kwenye ukweli wa mwisho unaohusu ajali ya waovu.  BAADA YA WALE AMBAO HAWATAOKOLEWA KUADHIBIWA KWA KADIRI YA DHAMBI ZAO, HUKU WAKIWA NA MIILI PAMOJA NA ROHO ZAO, WATAFUTILIWA MBALI HATA WASIWEZE KUWAKO KABISA MILELE HATA MILELE.  Yesu alieleza jambo hilo kwa urahisi sana,  “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho;  afadhali mwogopeni yule awezaye KUANGAMIZA MWILI NA ROHO PIA KATIKA JEHANUM.”  Mathayo 10:28.


     Katika nuru ya usemi huo, mtu anawezaje kuendelea kudai kwamba wafu wana miili isiyokufa?  Yesu, awezaye kutoa karama ya uzima peke yake, anakana kwamba hakuna uwezekano wo wote kwa wale walio katika jehanum kuendelea kuishi humo katika umbile liwalo lote lile.  Uhai wao utatoweka milele zote, na mwili wao utaharibiwa kabisa katika ndimi zile za moto.


     Mtunga Zaburi aliandika maneno haya:  “Bali wasio haki watapotea [wataangamia], nao
wamchukiao BWANA watakuwa kama mafuta ya wana-kondoo:  WATATEKETEZWA KABISA;  KAMA MOSHI WATATOWEKA.”  Zaburi 37:20, KJV.  “Maana bado kitambo kidogo ASIYE HAKI HATAKUWAPO, utapaangalia mahali pake wala HATAKUWAPO.”  Fungu la 10. 


     Maneno hayo ya ufafanuzi yenye nguvu sana katika lugha ya kibinadamu  yametumika kuelezea maangamizi katika jehanum, lakini watu hao bado wanasisitiza kwamba waandishi hao hawana maana ile ile hasa kama vile maneno yao yanavyosema.  “Angamiza”, “teketeza”, “choma kabisa”, “kula”, “mauti”  -  je!  maneno hayo yana maana fulani iliyojificha,  yaani, maana iliyo kinyume cha maneno hayo katika Biblia kuliko vile ilivyo katika vitabu vingine?  Sisi hatuna sababu yo yote ya kufikiri hivyo.  Ukweli ni kwamba theolojia imemfanya Mungu wetu mkuu mwenye upendo kuwa kama zimwi.  Picha yake wanayoionyesha ni ya ukatili kuliko ule wa Hitler.  Ingawa Hitler aliwatesa sana
watu na kufanya majaribio juu ya miili yao, hatimaye aliwaachilia ili wapate kufa.  Lakini ati Mungu ataziweka hai roho hizo zisizoweza kufa kwa kusudi la kuziona zikigaagaa na kupiga yowe milele hata milele, hivyo ndivyo wanatheolojia wanavyodai.  

HAKI YA MUNGU YATHIBITISHWA 

     Picha kama hiyo sio tu kwamba inauwakilisha vibaya sana upendo wa Mungu, pia inapotosha ukweli wa haki yake.  Hebu fikiria kwa dakika moja hivi athari za fundisho hilo ambalo lingeipeleka mara moja na kuifungia  katika jehanum isiyo na mwisho kila roho iliyopotea dakika ile ile aliyokufa yule mwovu.  Tuseme kwamba mtu mmoja alikufa yapata miaka 5000 iliyopita akiwa na dhambi moja tu aliyoipenda sana katika  maisha yake.  Roho yake ingekwenda mara moja motoni na kuteswa vibaya sana milele hata milele.  Kisha piga picha ya kifo kingine;  kile cha Adolph Hitler, aliyesimamia mauaji ya mamilioni ya watu.  Kulingana na fundisho hilo linalopendwa sana na watu wengi, roho yake pia ingeingia mara moja jehanum kuteswa humo milele na milele.  Lakini mtu yule aliyepotea
kwa sababu ya dhambi yake moja tu, ataendelea kuungua humo kwa zaidi ya miaka 5000 kuliko Hitler. Je, jambo hilo lingekuwaje la haki?  Je, Mungu angeweza kutenda kwa njia kama hiyo?  Jambo hilo lingeupinga usemi wa Biblia usemao kwamba kila mmoja ni lazima aadhibiwe kwa kadiri ya matendo yake [Luka 12:45-48;  Ufu. 22:12]. 


     Kuna mitazamo miwili inayovuka mpaka ambayo hivi sasa inaenezwa kote kuhusu adhabu ya waovu.  Mtazamo mmoja ni ule unaoamini kwamba ulimwengu wote utaongolewa (Universalism), ambao unadai kwamba Mungu ni Mwema mno kuweza kumwacha mtu ye yote kupotea.  Mtazamo mwingine ni huo wa fundisho hilo linaloogofya mno la mateso yasiyo na mwisho ambayo yataendelea  milele hata milele katika shimo refu lenye giza la utungu na mateso.  Mitazamo hiyo yote miwili imepotoka.  Ukweli uko katikati yake.  Mungu atawaadhibu waovu kwa kadiri ya matendo yao, ila  hataruhusu uovu wao uendelee milele kwa tendo lake hilo.


     Mimi nasadiki kweli kweli ya kwamba watu wengi wanyofu wa moyo wamegeuziwa kando mbali na Mungu kwa sababu ya kuchukia kwao kutokana na njia hiyo ya kuielezea vibaya tabia yake.  Hawawezi kumpenda mtu yule ambaye kwa udhalimu wake atawaweka waovu katika mateso yasiyo na mwisho bila kuwa na kusudi lo lote la maana mbele yake.  Hakuna uwezekano wa kuwawezesha  kuishi maisha ya kawaida.  Ni roho ile tu ya kutaka kulipa kisasi ambayo ingetumika kwa mpangilio kama huo usioelezeka.  Je, Mungu yuko hivyo?  Baada ya kuisikia kweli ya Biblia kuhusu jehanum, mwenyekiti mmoja wa benki alinikumbatia mabegani na kusema,  “Joe, mimi nimekuwa muumini  tena.  Kwa miaka mingi nimekuwa nikisadiki kwamba sisi hatuna habari zinazomhusu  Mungu, wala hatuwezi kuzijua, kwa sababu nilikuwa nimefundishwa kwamba Mungu angewatesa vibaya sana 
waovu milele na milele.”


 
HAKUNA MAUMIVU TENA WALA MAUTI


     Siku moja hivi karibuni Mungu atautakasa ulimwengu mzima.  Athari zote za dhambi zitatoweka milele.  Hapatakuwa na dhambi, wala wenye dhambi, wala mwovu wa kutujaribu.  Itakuwa sawa kabisa na vile alivyopanga Mungu hapo mwanzo.


     Yohana alizielezea habari za makao yetu ya baadaye kwa maneno haya,  “Naye (Mungu) atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena;  wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena;  kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”  Ufunuo 21:4. 


     Je, hivi wewe unaweza kuona mwanya wo wote katika maneno hayo ya thamani ya kuwapo kwa mateso yo yote kwa upande wa mtu ye yote katika dunia yote iliyoumbwa upya?  Mungu alisema kwamba kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena.  Je, unaliamini Neno lake au unachagua kuamini  mambo ya mwanadamu ya kukisia-kisia tu?  Mafungu manne tu kabla ya kuiandika ahadi hiyo, Yohana alieleza namna waovu watakavyotupwa katika ziwa lile la moto.  “Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.  Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya;  kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita.” Ufunuo 20:15;  21:1. 


     Ziwa la moto liko papa hapa juu ya uso wa sayari hii ya dunia yetu kwa mujibu wa Ufunuo 20:9. Lakini tafadhali zingatia kwamba mahali hapa wanapoteketezwa waovu patapita, na Mungu ataiumba upya nchi mpya mahali pake.  Ndipo Ufunuo 21:2,3 unapoielezea Yerusalemu Mpya ikishuka, na fungu lile la nne linasema kwamba huzuni haitakuwapo tena, wala maumivu, wala kilio, wala mauti.


     Ili maumivu zaidi yasipate kuwapo, haiwezekani pia kuwapo jehanum inayoendelea kuwaka milele.  Mambo hayo mawili hayawezi kuchanganywa pamoja.  Tungemshukuru Mungu kila siku ya kwamba mpango wake hatimaye utakomesha mateso yote.  Shetani hatakuwapo hapa kusababisha maumivu hayo, naye Mungu anaahidi kwamba ufalme wake mpya hautakuwa na kivuli cho chote cha maumivu.

bottom of page