Je Yesu Alikuja kwa Israeli Pekee?
Utangulizi:
Hoja inayohusiana na mipaka ya utume wa Bwana “Yesu” ni miongoni wa hoja tata sana katika mchakato wa kidini kipindi cha leo.
Maandiko kadhaa ya Kibiblia yanaonekana kutoeleweka na watu wengi na hivyo kutojua haswa msingi wa ujio wa Bwana Yesu kama ulilenga mataifa yote au Israeli pekee.
Mafungu yafuatayo yametumiwa kujenga hoja hiyo:-
Mathayo 2:6
Nawe Bethlehemu katika nchi ya Yuda humdogo kamwe katika majumbe ya Yuda: kwa kuwa kwako atatoka mtawala atakaye wachunga watu wangu Israel.
Utabiri huu unaonyesha kusudi la ujio wa Bwana Yesu kulenga Taifa la Israeli kwanza hebu fuatilia na andiko hili jingine hapo chini.
Mathayo 10:5
Hao thenashara Yesu aliwatuma akawaagiza akisema katika njia ya Mataifa msiende wala katika mji wowote wa samaria msiingie (6) afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israel.
Hapo pia Bwana Yesu anaonekana kuwaagiza wanafunzi wake kutotoka nje kuhubiri kwanza na wachukue njia kuwa tafuta kondoo wa Taifa la Israel waliopotea.
Fungu linalotumika sana pamoja na hayo yote tulokwisha yaangalia ni lile la kisa cha mama mkananayo ambacho kinaelezwa vyema katika fungu lifuatalo:-
Mathayo 15:21-22,24
(21) Yesu akaondoka huko, akaenda pande za Tiro na sidoni (22) na tazama, mwanamke mkanayo wa mipaka ile akatokea, akapaza sauti akisema unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi: binti yangu amepagawa sana na pepo.
(24) Akajibu akasema sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wanyumba ya Israeli.
Maswali ya msingi:-
Je! Mbona maandiko hayo yanaonyesha kuwa utume wa bwana Yesu haukupaswa au kukusudiwa kulenga ulimwengu wote?
Kuna sababu gani ya kina inayopelekea maandiko ya Biblia kuueleza Utume huo wa Yesu katika wazo la Taifa la Israeli?
Na Je! Nini ukweli wa fundisho na imani ya kuwa Bwana Yesu amekomboa ulimwengu wote ukilinganisha na aya hizo za Biblia zinazoonekana kulenga Israeli tu?
Uchambuzi wa Mada.
B
inafsi sikuzote huwa ninapenda kusema kuwa kamwe Biblia haijichanganyi wala kujipinga, isipo kuwa wasomaji wengi wa Biblia wamejipinga wenyewe katika fidra zao juu ya maandiko, misimamo na mipaka wanayojitengenezea katika kuyatafakari maandiko imewaponza na hivyo kutopata fursa ya kuchunguza zaidi maandiko hayo kwa kuwa pia wamepoteza kanuni ya kimsingi ya kusoma vitabu hivyo kutokana na misimamo yao.
Kanuni iliyosahaulika na wasomaji wengi hususani rafiki zangu wa kiislamu ni ile inayoelezwa na maandiko ya Kibiblia:-
Mhubiri 7:27
Tazama, asema mhubiri, “mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha na hili, ili kuitafuta jumla.”
Ndugu msomaji wangu hapo ndipo watu wengi walipopoteza njozi, Biblia inazo kanuni za kimsingi za kuzingatiwa unapoisoma hupaswi kugusa sehemu tu ya Biblia ukahisi kuwa umeshakamilisha kuisoma Biblia yote.
Tusije tukalingana na vipofu wawili
Hawa vipofu wote hawakuwahi kuona umbo la tembo kutokana na hali yao, siku moja walibahatika kupata fursa ya kutafiti mnyama huyo walau kwa kumgusa tu………
Kwa hofu kubwa kipofu wa kwanza aliingia katika chumba alichokuwapo tembo na kuanza kumpapasa ili kujua umbile lake ….Kwa kuwa hakuwa na kanuni ya “Ujasiri” alijikuta akimshika tu katika sikio na kuzungusha mkono wake mwisho alihitimisha zoezi lake kwa uelewa kuwa tembo hufanana na sahani ya chakula.
Kipofu wa pili naye vivyo hivyo alijikuta akiangukia upande wa mkonga wa tembo na kuondoka na uelewa kuwa tembo hufanana na nyoka mkubwa.
Maswali ya kimsingi ya kujadili:-
Je ! hawa vipofu wote walikuwa sahihi?
Na kutokuwa sahihi kwao kunatokana na kukosea kanuni gain?
Na je! Katika habari ya usomaji wetu wa vitabu kisa hicho kinatuonya makosa gani tutendayo katika usomaji wa maandiko haswa kwa kuzingatia kanuni ya Mhubiri 7:27?
Tusije tukawa vipofu wa kiroho katika kusoma maandiko kwasababu kutozingatia kanuni hiyo ya msingi.
Bwana Yesu aliwahi kusema:- “Wana macho lakini hawaoni.”
Hebu sasa tutumie macho yetu vyema tena yale ya kiroho na hivyo tuweze kuchunguza maandiko haya vyema bila ya kupoteza kanuni hiyo ya kulinganisha.
Mbona Utume wa Bwana Yesu ulikatazwa kwa Israeli hapo awali?
Ndugu msomaji wangu wa Makala hii ya Darubini kama ulivyokwisha kuona katika mafungu ya hapo mwanzo, kuwa utabiri na maelezo kadhaa ya Utume wa Yesu unaonekana kukazwa zaidi kwa upande wa Israeli kama tusomavyo:-
Mtawala ………… atakae wachunga Israeli (Mathayo 2:6)
Katika njia ya mataifa msiende …….. waendeeni kondoo wa Israeli. (Mathayo 15:24)
kwanini mkazo kwa Israeli?
Kutoka 19:5-6
“Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kwelikweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapo kuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu: maana dunia yote ni mali yangu. (6) Nanyi mtakuwa kwangu Wafalme na Makuhani, na Taifa Takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayo waambia wana wa Israeli.”
Andiko hilo la Biblia linaonyesha sababu ya msingi ya kuonekana mkazo mkuu ukilenga Taifa la Israeli, maandiko hayo yanaonyesha kuwa Mungu alilichagua taifa hilo kama kituo cha kazi yake. Fuatilia maelezo:-
-
Mtakapokuwa tunu kwangu kuliko kabila zote.
-
Maana Dunia yote ni mali yangu
-
Mtakuwa kwangu wafalme na makuhani
-
Maneno utakayo waambia Israeli
Kwa ujumla maandiko ya Biblia yanaonyesha kuwa tangu awali Mungu alipokuwa amepanga Mpango wake wa Ukombozi aliamua kuchagua kituo Maalumu cha kuanzia kazi hiyo.
chukulia mfano wa mfanya biashara, anapotaka kuanza biashara lazima awe na mahali au ofisi maalumu ya kuanzia mipango yake ya biashara na kwa kadri ya mwenendo na matokeo ya biashara hiyo huweza kumwezesha kupanua wigo na hivyo kuenea zaidi katika maeneo mengine.
Qur-a inakubali kuwa Mwenyezi Mungu alichagua Taifa la Israeli katika mwanzo wa kazi yake na kupitia uzao huo Mungu aliteuwa watumishi wakao eneza ufalme wake:-
Qur-an 29:27
Na tulimpa (kumzaa Nabii) Is-haqa na (kumjukul Nabii) Yakubu, na tukaweka katika kizazi chake unabii na (kupata) kitabu, na tukampa ujira wake katika Dunia, naye akhera kwa yakini atakuwa miongoni mwa watu wema.
Bwana mwenyewe aya nyingine ya Qur-an ni Surati Al-Aaraf ambayo nayo inaweka mkazo unaonyesha kuwa kizazi cha Israeli kilichaguliwa na kwaajili ya kuwa kituo cha kuanzia mpango wa wokovu.
Qur-an 7:137
Na tukawarithisha watu waliokuwa wanaonekana madhaifu (waliokuwa wakionewa, nao ndio hao Ban Israili), (tukawarithisha miji ya) masharti ya ardhi na magharibi yake ambayo tuliitia baraka (nyingi miji hiyo)…… na likatimia neno jema la mola wako wa wana wa Israeli kwa kule kuvumilia kwao ……..
Chunguza zaidi katika maandiko hayo mengine:
Qur-an 7:159-160… Tukawagawanya kabila kumi nambili.
Qur-an 20:80 … enyi Israeli tulikuokoeni na ……tukakupeni sharia.
Bwana Yesu pia alisema wokovu unatoka kwa Wayahudi
Yohana 4:19-22 …………………………………………………………………………..
Ufumbuzi wa hoja hii kwa kadri ya maandiko hayo tuliyo yasoma.
Ndugu mpendwa kwa kadri ya maandiko hayo tunachojifunza ni kuwa,Taifa hilo la Israeli lilipewa kipaumbele hicho kwakuwa ndilo ambalo Mwenyezi Mungu alilichagua ili kuanzia kazi yake hapo na si vinginevyo.
Swali:
Je ni jinsi gani mataifa mengine yalihusika na ukombozi huo?
Kwa maandiko tuliyo yasoma tumeona kwa mkazo maelezo juu ukombozi yakilenga taifa moja tu la Israeli na hii ni kutokana na sababu hiyo niliyokwisha ieleza punde.
Pamoja na hayo swali linalobaki ni kuwa Je! Maandiko mengine yanaelezaje juu ya mipaka ya utume wa Bwana Yesu na yakuwa wazo kuu la Utume huo wa masihi lilikuwa ni kwa Israeli tu au maandiko mengine yanaelezaje hilo?
Ndiyo:
Fungu linalojengewa hoja zaidi (Mathayo 15:24) lenyewe tu linaonyesha kuwa Utume wa Yesu pamoja na kuanzia Israeli bado ulilenga pia kwa Mataifa ya Ulimwengu wote.
Fatilia kwa makini aya hiyo,
Mathayo 15:24-27 unaweza kuona kuwa pamoja na Bwana Yesu kusema kuwa alikuja kwa
Israeli bado mwisho wa yote alimhudumia yule mama wa nje ya Israel
sawasawa na imani yake.
Fundisho:
Hilo ni ishara iliyolenga kuonyesha kuwa hapo mbele mlango wa wokovu ungeweza kufunguka kwa Mataifa hata yaliyo nje ya Israeli.
Hebu sasa tuliangalie hilo kwa upana:
Yohana 11:51-52
Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake bali kwa kuwa alikuwa kuhani mkuu mwaka ule alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwaajili ya taifa hilo. (52) Wala si kwaajili ya taifa hilo tu, lakini pamoja na hayo awakusaye watoto wa Mungu walotawanyika wawe wamoja.
Hilo ni moja kati ya mafungu yaliyo wazi sana kuhusiana na mipaka ya Utume wa Yesu Duniani.
Zingatia:
(Vs 52) wala si kwaajili ya Taifa hilo tu “……
Sehemu hii inanisaidia kutambua umuhimu wa kusoma maandiko kwa kulinganisha, ni jambo rahisi tu ikiwa utaishia katika kitabu kile cha Mathayo 15:24 tu unaweza kubaki na wazo hilo lisilosahihi kuwa huenda Bwana Yesu ni wa Israeli tu, lakini Biblia inasema si kwa Israeli tu.
Ndugu mpendwa usidanganyike na walimu wa uongo kamwe, chunguza Mwenyewe uone.
Mfumo kama huo wa Utume wa Bwana Yesu ulitumiwa na Muhammad pia.
Maelezo:
Hapo mwanzoni lilikuwa ni jambo linalonishangaza sana ninapoona jamii ya waislam wakipata ugumu wa kuelewa mfumo huu wa kiutume wa Bwana Yesu kuanza Israeli na kisha Ulimwenguni.
Hilo linatokana na ukweli kuwa hata ndani ya Qur-an kuna muundo kama huo katika kazi ya Utume wa Muhammad, na zipo kauli mbalimbali zinazo ashiria kuwa Muhammad alilenga kwanza taifa la Waarabu kabla ya kuvuka kwa mataifa mengine.
fuatilia aya hii …………………….
Muhammad kwa Waarabu kwanza.
Qur-an 26:214 Na uwaonye jamaa zako walio karibu (nawe ).
Andiko hilo la Qur-an linaweka wazi kuwa Muhammadi alipewa amri hapo awali iliyomtaka kuanza kwanza kazi ya kueneza dini yake ya Uislam kwa jamaa zake (Waarabu ) wa karibu nae.
Kwa msomaji asiye zingatia Kanuni na hivyo kusoma kwa kuhitimisha wazo katika andiko moja tu angeweza kuwa na hoja katika andiko hilo la Qur-an ambalo kimsingi linaonyesha kuwa utume wa Muhammadi ulipaswa kuhusika na watu wa karibu naye.
Pamoja na hayo uanposoma Sherehe (fafanuzi ya aya hiyo hapo chini.Uk 476 kuna maelezo ya fuatayo:-
Mtume kabla ya kupewa amri ya kuwalingania watu wote katika uislam. Kwanza aliletewa amri hii ya kuwalingania jamaa zake walokuwa karibu naye ………………
Pamoja na hayo wazo hilo lapili linafahamika tu kwa uchunguzi na kwa kusoma vifungu na maelezo mbalimbali ya Qur-an. Vinginevyo kama msomaji ataishia katika aya tu inatosha kwake kujenga wazo la kuwa Muhammad hakuwa Mtume wa Ulimwengu wote kama waaminivyo waislam na badala yake alihusika na Waarabu tu.
Jadili yafuatayo:
Ni jinsi gani jambo hilo linawiana na lile la Biblia juu ya Utume wa Yesu?
Kama vile Bwana Yesu alivyoanzia kazi Israeli na hatimaye Ulimwenguni kote ambapo tumeona wazo hilo linafanana na Muhammad alipoanza kazi kwa waarabu na baadae kutangazwa kama Mtume wa ulimwengu. Je! Wale wanaoudumu kujengea hoja Utume wa Yesu na kushikilia kuwa Yesu ni wa Israeli, unadhani ni nini kinacho wakosesha au wasicho kielewa?
Ikiwa utapata jibu kuwa huenda wanafanya hayo kwa upinzani au ubishi tu basi chukua hatua ya kuwaombea ili Mungu afungue miyoyo yao na hatimaye wagundue siri hii kuu ya wokovu kwa maisha yao.
Waarabu walilengwa zaidi katika utume wa Muhammad.
Qur-an 41:44
Na Lau kama tungeliifanya Qur-an kwa lugha isiyo ya Kiarabu wangelisema kwanini aya zake hazikupambanuliwa? Lo! Lugha isiyokuwa ya Kiarabu na (Mtume ) ni muarabu! (Mambo gani haya) ………..
Qur-an 42:7
Tumeteremsha Qur-an kwa lugha ya kiarabu…………………………………………
Maelezo hayo ya Qur-an yanaonyesha Malalamiko ambayo yangeliweza kutolewa na Waarabu endepo tu Qur-an isingekuwa kwa lugha yao.
kwa kadri ya hoja zinazojengwa dhidi ya Biblia kwa wakristo basi badala yake wakristo nao wangeweza kujenga hoja juu ya fungu hili kwa kusema kuwa Qur-an ni kitabu chenye mkazo na kuridhia Waarabu hivyo basi Muhammad ni Mtume kwa Waarabu tendo ambalo Waislam nao wanalipinga kwa vigezo vya maandiko mengine.
Katika hilo ninaona umuhimu wa kushauri wale wasomaji waaminifu wa vitabu wasitumie fursa zao za kusoma maandiko vibaya na badala yake wafuate kanuni muhimu, vinginevyo hoja yeyote inayojengwa pasipo umakini juu ya Biblia inazaa hoja kuu zaidi katika Qur-an.
Fungu jingine la Qur-an linalo kaza wazo zaidi juu ya Utume wa Muhammad kulenga kwa Waarabu hapo awali ni-
Qur-an 62:2 Yeye ndiye aliyemleta Mtume katika watu wasiyo jua kusoma,
anayetokana na wao, awasomee aya zake na kuwatakasa na kuwafunza
kitabu na hekima……
Andiko hilo linaonyesha tena kwa uwazi jinsi Utume wa Muhammad ulivyoanzia na kuwa na mkazo zaidi kwa Waarabu ………. Hapo Qur-an inasema kuwa Muhammad aliletwa kwa watu wasiyo jua kusoma.
Watu hao waliotajwa hapo ni jamii ya Waarabu walioishi katika kipindi hicho katika mji wa Makka ambao wanawekwa wazi zaidi katika kitabu cha Maisha ya Muhammad kama ifuatavyo:-
Maisha ya Muhammad Uk. 8 kifungu “F”
Kujifunza kwake
Habari ya kusoma haijakuwako katika hija 2, kwahiyo Mtume aliondokea kama makureshi wengine bila ya kujua kusoma wa kuandika ………Mtu wa awali aliye jifundisha kusoma na kuandika katika mji wa Makka ni Bwana Harb Ibn Humayya Babu yake Muawiya naye alijifunza kwa watu wa Yaman ………..
Wokovu kwa Mataifa nje ya Israeli
Kaitka muda wote ambapo Bwana Yesu alitenda kazi yake kwa watu wa Israeli na wakati Fulani kushauri wanafunzi wake kuwa wasiende kwa mataifa maandiko yanaeleza kuwa kulikuwa na uadui ambao ilimpasa aufishe (auondoe) kwanza ndipo mlango ufunguke kwa Mataifa.
Swali:
Je! ni udui gani huo?
Na ni kitu gani kilicho ufisha na kufungua mlango wa Ukombozi kwa Mataifa yote?
Katika lugha ya kibiashara tungelisema kuwa tunatafuta mtaji ambao ulimwenzesha kupanua Ofisi yake ya wokovu kwa Mataifa yote na si Israeli tu.
Fuatilia mafungu haya ya Biblia:
Waefeso 2:12
Kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni msio wa maagano ya ahadi ile mlikuwa hamna tumaini hamna Mungu Duniani.(13) lakikini sasa, katika Kristo Yesu ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu katika damu yake Kristo.(14) kwamaana yeye ndiye amani yetu aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja, akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. (Kolosai 1:17 …………..)
Kabla ya kifo chake Bwana Yesu alizuia mambo mengi kutotendwa na wanafunzi hadi hapo atakapo fufuka.
Matahayo 17:9 Msimwambie mtu yeyote hata mwana wa Adamu atakapo fufuka.
Maandiko hayo yanaonyesha kuwa kifo cha Bwana Yesu ndiyo mtaji uliomfungulia
tena kwa uhakika uwanja wake wa kiutume katika Ulimwengu wote.
Bwana Yesu mwenyewe aliwahi kusema.
Yohana 10:15-16 Nami nautoa uhai wangu kwaajili ya kondoo (16) na kondoo wengine
ninao ambao si wazi hili.
Agizo la pili la Yesu baada ya kifo na Ufufuko wake juu ya kazi ya Utume wake.
Mathayo 28:15
Basi enendeni mkawafanye “Mataifa yote” kuwa wanafunzi ……………..
Bwana Yesu anapotoa agizo lake la utendaji kwa wanafunzi anawaambia kwenda ulimwenguni kote na siyo Israeli tu maana Mtaji ulishakua.
Maandiko mengine ya mkazo:
Matendo 9:3/15 alichukue jina lako mbele ya Mataifa
Qur-an 19:21 tumfanye (Isa) muujiza kwa wanaadamu na rehema itokayo kwetu ………
Bado Biblia inaweka mkazo kuwa Utume wa Bwana Yesu ulihusika na Ulimwengu mzima.
Fungu la maandiko ya Qur-an nalo linasema kuwa Isa (Yesu) alikuja ili kuwa Rehma kwa watu na haikusema kuwa watu hawa ni Israeli tu. Na kwa kawaida Qur-an inapotaja watu hukusudia wanadamu wote.
Qur-an 4:1 Enyi watu muabuduni mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja.
Mataifa yote yalivyookolewa na Bwana Yesu
Ufunuo 7:9 “ Watu wa kila Taifa, jamaa kabila, lugha wakiwa mbele ya Yesu.”