Je Biblia Imetiwa Mikono?
Neno Biblia ni neno lenye asili ya Lugha ya kiyunani nao huita “Biblos” neno hili linapotamkwa humaanisha “Maktaba” au Mjumuiko, Mkusanyiko wa vitabu”.
Biblia ni kitabu kilicho andikwa na waandishi wasio pungua “arobaini”ambao walikuwa sehemu na mahala tofauti lakini kwa uongozi wa roho mtakatifu waliweza kuandika maneno yaliyowiana.
-
Matendo 11;19 wanafunzi wa Yesu walitawanyika baada ya ile dhiki
-
1Petro 1:20 walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na roho mtakatifu.
-
Isaya 34:16 tafuteni katika kitabu cha Bwana mkasome.
Pamoja na hayo siku hizi za karibuni kumeibuka vikundi mbalimbali vinavyoendesha mikutano,inayojulikana kwa jina la “mihadhara” vikundi hivyo vimeibua mafundisho yasiyo sahihi kwa kudai kuwa Biblia imetiwa mkono na si kitabu cha kweli, hivyo kupitia uchambuzi huu tutaangalia mada mbalimbali kwa kuanza na mada hii tete juu ya ukweli wa Biblia, ambapo vitabu vyote yaani Biblia na Qur an vitasaidia kutoa ufumbuzi.
VIGEZO VYAO VYA KUDAI KUWA BIBLIA SI YA KWELI
Yeremia 8:8-9 inasema kuwa “kalamu ya waandishi imeifanya kuwa uongo.”
Jibu kwa kifupi
Katika kujibu swali hili, ni muhimu kuanza kwa kuangalia makosa ya kiusomaji yaliyofanywa na wajenga hoja wa mada hii.Kwa kutolichunguza kwa makini andiko hilo ili kuelewa muktadha wake, hebu tuchunguze….!
Yeremia 8:8
Mwasemaje sisi tuna akili na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini tazama kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.
Katika aya hiyo, yako mambo ya kimsingi ambayo kamwe wajenga hoja hawayazingatii jambo la kwanza. Nabii Yeremia anasema “torati ya Bwana tunayo pamoja nasi” hivyo kabla ya kujenga swali lolote ingepaswa kujulikana kwamba torati haikuwa kwingine bali ilikuwa mikononi mwa manabii, hivyo ilikuwa salama.
Sehemu ya pili, ni pale andiko linaposema “lakini tazama” kauli hii uhashiria kuwepo kwa upande wa pili wa watu au kundi lililo anzisha jitihada nyingine pinzani mbali, pindi torati ikiwa imehifadhiwa na manabii ambapo jitihada hizo zililenga kuikosoa torati ambayo ilihifadhiwa na kutunzwa na manabii.
Na sehemu ya mwisho ni ile kauli inayosema kalamu ya uongo ya waandishi “imeifanya kuwa uongo” kauli hii kamwe hailengi kuonyesha kuwa kulifanyika tendo la kuivuruga au kuibadilisha torati yenyewe la hasha” hapo limetumika neno “imeifanya” kuwa uongo, hii inamaana kuwa torati yenyewe ni ya kweli lakini wao walianzisha jitihada zao za kuikosoa
Chukulia mfano mtu akikwambia “wewe unanifanya mimi kuwa mjinga? Je- tayari umekuwa mjinga? Jibu – hapana”. Isipokuwa yeye anafanya mambo Fulani ili kufanya uonekane hivyo na hali sivyo ulivyo.
Je waandishi waliifanyaje torati kuwa uongo na kwa namna gani?
Kwa kadri ya msingi wa maandiko ya Biblia tendo la kuifanya torati kuwa uongo huhashiria “kutamka” au “kuandika maneno yanayo pingana na torati ya Bwana”.
Biblia inaonyesha kuwa kulikuwa na watu waliojaribu kutunga na kuweka sheria zao zilionekana zikipingana na zile halali za Mungu Yehova, hivyo huko ndiko kuifanya torati au sheria halali ya Mungu kuwa uongo na si badala yake kuiharibu sheria yenyewe ya Mungu kwenye kitabu husika, fuatilia ushahidi ufuatao:-
-
Isaya 10:1 Ole wao wawekao amri zisizo haki na waandishi waandikao
Maneno ya ushupavu ili kumpotosha mhitaji asipate haki
yake………
-
Yohana 19:5 Wayahudi wakajibu sisi tunayo sheria na kwa sheria hiyo
amestahili kufa kwakuwa alijifanya mwana wa Mungu.
Maandiko hayo yanonyesha vile ambavyo wanadamu nao walivyokuwa na jitihada za upande wao wa kuasisi sheria na taratibu zao ambazo kwa kadri ya maandiko zinaonekana kupingana na zile za halali za Mungu,hivyo hizo ndizo sheria “torati” za
uongo.
Pia kama nilivyokwisha eleza kuwa kwa upande mwingine tendo hilo la Kalamu ya uongo ya waandishi kuifanya torati kuwa uongo humaanisha kutamka au kufundisha yaliyo kinyume na torati hiyo ya Bwana,lakini huenda hoja ikawa ni kuwepo kwa neno kalamu ya uongo ambalo hufanya kuwepo na maana moja tu ya kuandika, katika hili biblia inaweka wazi kuwa hata mdomo huweza kuwa kalamu pia”waswahili wanasema maneno uumba”unapoongea uongo ni sawa na kuandika uongo huo kwenye bongo za wengine. Hivyo maneno ni kalamu.
Tukio linganifu katika mafunuo ya Qur-an
K
atika mafunuo ya Qur-an maelezo na picha hiyo ya kibiblia tuliokwishaiona huonekana pia, tatizo la kuibuka kwa makundi ya watu waliojaribu kugeuza au kuyafanya maneno ya Mungu au vitabu vilivyoaminiwa na jamii fulani kuwa uongo linaonekana kutawala katika pande zote za kidini. Hebu tupitie aya kadhaa za Qur an:-
-
Qur –an 15:91 “Ambao wameifanya Qur an kuwa mkusanyiko wa uongo
alioukusanya nabii Muhammad akadai kuwa ni maneno ya
Mwenyezi Mungu.”
-
Qur an 3:78 “ Kuna watu wanaopinda ndimi zao kwa kusoma vitabu ili tufikiri
kuwa maneno yao hayo ni ya kitabu cha Mwenyezi Mungu hali
hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu nao wanamsingizia
Mwenyezi Mungu uongo mkubwa……”
kwa ushahidi huo wa maandiko ya Qur an tunaweza kupata picha ya jumla juu ya hoja hii nyeti, maandiko hayo ya Qur an hususani ile aya ya kwanza yanaonyesha tukio linganifu na lile la Kibiblia, hapo pia inaonekana kuwepo kwa makundi ya watu fulani waliokosoa na kuibeza Qur an kuwa ni mkusanyiko wa uongo tendo linalolingana sawia na lile la Torati ya Bwana.
Qur an inasema kuwa watu hao waliifanya Qur an kuwa ni mkusanyiko wa uongo.
Hoja ya msingi:
Je’nisahihi kutumia ushahidi wa andiko hilo pekee kuthibitisha mapungufu ya Qur an?
Endapo jibu si sahihi vivyo hivyo hakuna usahihi wowote wa madai ya kupotoshwa kwa Biblia kwa kuwa kinachoonekana katika muktaza wa aya hiyo ya Biblia ni maelezo yanayo onyesha upinzani unaolikabili neno hilo la kweli toka wa waandishi na watunzi wa maneno na vitabu vya uongo.
Maswali ya kujibu Kwa wanaodai kupotoshwa Kwa Biblia
-
Nani alifanya upotoshaji huo?
-
Wapi na ni lini upotoshaji huo ulifanywa?
-
yako wapi magombo ya asili ambayo hayakupotoshwa ili kusaidia kujua maeneo ya vifungu vilivyopotoshwa?
-
Kulikuwa na sababu zipi zilizofanya Mungu anyamaze na kutolinda mafunuo yake ya wokovu kwa wanadamu wake?
-
Je nini ukweli na maana ya Mungu kutoa maelekezo yanayoonyesha uhakika na kutokuwepo uwezekano wa kubadilishwa kwa mafunuo yake matakatifu?
Fuatilia Aya zifuatazo:-
Mathayo 5:18 “yodi wala nukta ya torati haitaondoka…………..
Zaburi 15:4 “ameapa hayabadili maneno yake……………..
Qur-an Surat Ban Israel17:77 Ndiyo desturi ya wale tuliowatuma (tuliowapa utume) kabla yako katika mitume wetu. Wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.
Qur-an Surat Fatir 35 : 43 wala hutapata mahadiliko katika kawaida(desturi) ya Mungu
(allyoiweka)wala hutakuta mageuko katika kawaida ya
Mwenyezi Mungu.
Ushahidi huo wa maandiko ya vitabu vyote viwili unaonyesha na kuthibitisha vile ambavyo hoja zinazo tolewa kwa kudai kuwa Biblia imeharibiwa si hoja za kimsingi na zaidi ya yote ni hoja zinazoonekana kushusha nguvu na uwezo wa Mungu wa kulinda na kusimamia mambo yake,lakini zaidi ya yote ni kutaka kumfanya mwongo pale alipoahidi kulinda maneno yake na kutokubali mageuzi katika mafunuo yake.
“Kamwe Biblia haijapotoshwa na haiwezi kupotoshwa”
Biblia ni mhimili wa Qur an – “Fatilia uchambuzi huu”
Katika sehemu hii “Biblia Mhimili wa Qur-an” tutapiga picha ya mbele zaidi katika kuyaelewa haswa mafunuo hayo na umuhimu wake. Sehemu hii kwa umakini zaidi tutafanya linganisho litakalo tupatia kipimo halisi cha kuelewa mhimili haswa wa kitabu hicho cha Msahafu wa Qur-an, katika mada hii wazo kuu litakalo rahisisha kazi yetu ni lile tunalolipata kupitia sura ya “87:18”ndani ya msahafu.
Qur- an Sura ya 87:1
“Hakika hayo mnayoambiwa humu (ndani ya Qur- ran) yamo katika vitabu vilivyotangulia. Vitabu vya Ibrahim, Musa, Isa na manabii wengine………………..”
Maneno hayo ya Qur-an yanatupatia Mwangaza unaotupa msingi wa kuichunguza vyema mada hii ya muhimu, maelezo ya Qur-an katika Aya hiyo yanaonyesha kuwa msingi wa mafunuo hayo ya Qur-an unategemea sana na kujengwa juu ya yale yaliyokwisha funuliwa awali katika vitabu vilivyo katika mkusanyiko wa “Biblia takatifu” hata hivyoMaandiko ya Qur-an kwa uwazi huyataja na kuyathibitisha mafunuo hayo ya kibiblia kwa kadri ya Aya zifuatazo:-
1. Torati - Musa
Qur-an 2:53 Na tulimpa Musa kitabu (Torati) cha kupambanua na
kuongoa ………
Qur-an 28:48 “Mnayakataa alopewa Musa”
2. Zaburi – Daud
Qur-an 4:163 Na Dawdi tukampa “Zaburi”
Qur-an 17:55 Dawd tukampa “Zaburi”
3. Injili-Bwana Yesu/Isa
Qur-an 5:47 watu wa “Injili” wahukumu kwa yale aliyotelemsha
Mwenyezi Mungu ndani yake.
Mafungu hayo ya Qur-an kwa uwazi mkubwa yana onyesha uzito na ukweli wa vitabu hivyo vya kale, kwa maana nyingine ndiyo maana Qur-an inaweka wazi kuwa mafunuo hayo (ya Qur-an) yanatokana na msingi wa Biblia (87:18).
Jamii kubwa ya Wayahudi walisoma na kuelewa vyema msingi wa mafundisho ya Biblia haswa maandiko ya Torati ya “Musa”.
Hivyo kwa sehemu walijaribu kulinganisha maono hayo ya Muhammad na yale ya awali ya Biblia ambapo waliona kuwepo kwa tofauti kadhaa katika mfunuo hayo mapya ya “Muhammad”.
Kumbuka Muhammad alijieleza kuwa mafunuo yake yanarejea katika vitabu hivyo vya awali kama tulivyosoma (Qur-an 87:18). Lakini pamoja na hayo matukio kadhaa aliyo yasimulia Muhammad akirejea historia hizo za zamani yanaonekana kugeuka au kuongezwa na hivyo kupishana na Biblia. fuatilia mifano ifuatayo:-
1. Kujengwa kwa Mnara
maelezo ya Qur-an kuhusu tukio hilo yanapatikana ndani ya mafunuo hayo katika sura ya Qur-an 28:38 ambapo sura hiyo inaonyesha kuwa :-
“Farao alimwambia Amani ajenge mnara huo”.
Maelezo hayo hayako sahihi kwa kadri ya historia Maana farao aliishi miaka ya 800 na Amani aliishi miaka ya 900 baada ya Farao.Hata hivyo Biblia inaonyesha waliojenga mnara huo kwa kadri ya kitabu cha Mwanzo 10:32/11:4.huku kiongozi akiwa ni “Nimrodi”
2. Tukio la gharika
Fundisho la Biblia
Maandiko ya Biblia hueleza kisa hiki Maarufu kupitia Mafunuo hayo:-
Mwanzo 7:1-7 Bwana akamwambia Nuhu, ingia wewe na jamaa yako yote
Katika safina: kwa maana nimekuona u mwenye haki mbele zangu katika
kizazi hiki. Nuhu akaingia katika safina yeye na wanawe na Mkewe na wake za wanawe pamoja naye kwa sababu ya maji ya gharika.
Biblia hapo inaweka wazi kuwa katika tukio hilo la kihistoria pamoja na uangamivu wa watu wote lakini Mungu alinusuru familia yote ya Nuhu ambapo waliokolewa watu wanane wakiwepo watoto wote wa Nuhu.
Fundisho la Qur-an
Katika mafunuo ya Qur-an tukio hilohilo linatajwa lakini kwa jinsi tofauti na kuwa na nyongeza za kimatukio ambayo kwa kadri ya Biblia hayaonekani kuwepo.
fuatilia aya zifuatazo:
Qur-an 11:42-43.
Fungu hilo la qur-an hueleza kuwa licha ya kuokolewa kwa watu kadhaa akiwemo Nuhu mwenyewe, lakini mtoto mmoja wa “Nuhu”aliangamia kwa kugharikishwa kwenye maji.
Maelezo hayo ya Qur-an yanaendelea kwa kueleza kuwa sababu kuu ya mtoto huyo wa Nuhu kugharikishwa ni ukaidi aliokuwa nao pindi alipoambiwa kuingia kwenye safina.
Uchambuzi
Hayo ni mambo machache tu kati ya yale yenye tofauti katika mafunuo ya Qur-an na yale ya awali ya Biblia, mengineyo ni kama:-
Ndoa na talaka
- Biblia inakataza utoaji wa talaka “Mathayo 19:7”
- Qur-an inatoa ruhusa ya kutoa talaka “Qur-an 2:230”
Kuwepo kwa tendo la kuoa na kuolewa Mbinguni
- Biblia inakataa hilo “Mathayo 22:23”
- Qur-an inafundisha kuwepo kwa tendo hilo la kuoa na kuolewa na Mungu anaandaa
wanawake rasmi (mahulain) wenye macho ya vikombe “Qur-an 52:20”
Tofauti hizo za kimafundisho katika mafunuo hayo ya Qur-an ni kichocheo kikubwa kilichozua upinzani toka upande huo wa wayahudi na ndiyo maana waliibua upinzani mkali dhidi ya mafundisho ya Muhammad.
Biblia Mhimili wa Qur-an
Pamoja na mafunuo hayo mapya ya Qur-an bado mtume Muhammad aliendelea kuonyesha umuhimu na
nafasi ya “Biblia” katika imani yake hiyo ya uislam.
Mafungu na Aya kadhaa tutakazozipitia zitatusaidia kuoana ukweli huu utakao tupa mwelekeo wa kuelewa vile Biblia ilivyo tegemeo (Mhimili) mkuu wa Qur-an.Kwa kadri ya Aya kadhaa za Qur-an inaonyesha dhahili kuwa Qur-an si kitabu kinachojitegemea chenyewe, badala yake kinapaswa kupimwa na kusaidiwa na mafunuo ya Biblia takatifu
Fuatilia nukuu zifuatazo za Qur-an ili kupanua ufahamu huo katika swala hili la kimsingi:-
Qur-an 10:94… “Ukiwa na shaka katika haya tuliyo kutelemshia nenda ukawaulize
watu wasomao vitabu kabla yako…………….”
Hoja za msingi
-
Ikiwa Qur-an ni kitabu chenye kujitosheleza chenyewe kuna haja gani ya kuwauliza walosoma vitabu vya kabla ya Qur-an?
Qur an 16:43 … Nendeni mkawaulize wenye kumbukumbu za vitabu vya
MwenyeziMungu vya kale ikiwa ninyi hamjui
Jifunze kupitia mfano
Katika dunia yetu Hospitali mbalimbali zinazotibu magonjwa ya kila aina humo wapo Madaktari bingwa, kwa kawaida ili kumtambua Daktari bingwa (Mhimili) ni pale tu unapopata ugonjwa na kwenda katika hospitali unayo iamini lakini hatimaye mwisho wa yote una taarifiwa kuhamishwa na kupelekwa katika hospitali nyingine kwa uchunguzi zaidi, “bila shaka huko ndiko kwa daktari bingwa”.
Ni wazi kama utakuwa msomaji mwaminifu katika sehemu hii tutakubaliana na kupata jibu kuwa “Biblia takatifu ni Mhimili wa Qur-an” na kwamba hakuna usahihi wa mafundisho yanayosikika kudai kuwa kitabu hiki kitakatifu kimetiwa maneno ya uongo au kuharibiwa kwa namna yeyote ile.
“Bwana akubariki kwa uelewa huu.”