HUDUMA YA INJILI NA
MAHUSIANO KWA WAISLAMU
Sura ya Kwanza
Amri na hukumu katika maandiko ya Qur-an na Biblia
------------------------------------------
Sura ya Pili
Siku ya Saba [Sabato] inavyoitwa katika Kiyunani,Kiarabu na Kiebrania
---------------------------------
Sura ya Tatu
Isemavyo Qur-an juu ya siku ya ibada ya kweli [Sabato]. Ni ljumaa, Jumamosi au Jumapili?
---------------------------------
Sura ya Nne
Nini chimbuko la ibada ya siku ya ljumaa ya Kiislamu? Na Je, inasimama mahala pa Sabato?
---------------------------------
Pr. Dominic Mapima
Muslim areas Evangelism Instructor.
Mobile: 0754-527143
Email: dominicmapima@yahoo.com
SIKU YA KUABUDU (SABATO) YA KWELI KWA MUJIBU WA QURAN NA BIBLIA
Kwa nini tunasali na viatu
Utangulizi.
Ninapenda kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru Mungu kwa uongozi na uwezeshaji wake katika utafiti na uandishi wa mada hii muhimu yenye lengo la kututoa katika giza la uelewa juu ya swala hili tete la kusali au kutosali na viatu katika majengo yetu ya ibada.
Hivyo nikualike ndugu msomaji wangu kuungana nami katika mchakato huu wa uchambuzi na ufafanuzi wa mada hii ili hatimaye uweze kujivunia maarifa haya muhimu kwa maisha yako ya imani na wokovu.
​
Ni kwa muda mrefu sasa kumekuwa na sauti zinazopazwa kila kona katika Tanzania na maeneo mengine ya nchi za dunia toka kwa ndugu na rafiki zetu wapendwa wa Kiislam, wakihoji juu ya kile wanachokiita kuwa ni tendo la Wakristo kupuuzia au kutotii ukweli wa Biblia kwa madai kwamba maandiko matakatifu ya Biblia kupitia agizo fulani lililotolewa kwa nabii Musa yanaelekeza Wakristo kutekeleza matendo yao ya ibada kwa kuvua viatu vyao waingiapo makanisani.
Katika toleo hili tutaangazia mambo muhimu yatakayo saidia kutoa mwangaza na majibu ya msingi juu ya hoja hiyo tete.
Mapitio ya mada:-
-
Chimbuko la hoja hiyo katika Biblia na Qur an.
-
Farsafa juu ya tukio Musa kuvua viatu / nini kusudi la tukio hilo?
-
Je’ Musa alivua viatu katika matendo halisi ya ibada katika utumishi wake?
-
Je’ mtume Muhammad naye alisali na viatu au bila viatu?
-
Bwana Yesu / Manabii na Mitume katika farsafa ya ibada na kuvaa viatu.
Kwa kuatilia kwa makini vipengele hivyo vya uchambuzi hadi mwisho ni imani yangu kuwa hautabaki kama ulivyo ikiwa u Muislam au ni Mkristo, ninachokusihi ni kufungua moyo wako ili kweli za maandiko zipate nafasi ndani yako.
Uchambuzi wa mada
​
Hebu sasa bila ya kupoteza muda tuanze kwa kuangalia kipengele namba moja kama vilivyoainishwa katika muongozo wa mapitio ya mada:-
Chimbuko la hoja hiyo katika Biblia na Qur an.
Kuibuka kwa hoja hii chanzo chake ni matokeo ya ndugu zetu na marafiki wa Kiiislam kugeukia matumizi ya Biblia katika harakati zao mbali mbali za uenezi wa Uislam duniani.
Kuanzia kule Durban - Afrika ya kusini’ mwana mihadhara mashuhuri marehemu Ahmed Deedat ndiye mwanzilishi mkuu wa hoja hizi chini ya shirika lake la uenezi wa Uislam IPC – (Islamic Propagation Centre), bwana Deedat ameandika majarida na vitabu vingi vinavyohoji na kukosoa msingi mzima na misimamo wa mafundisho ya teolojia ya Kikristo, ambapo katika kitabu kimojawapo pia ameibua hoja hii juu ya kile anachodai kutokuwepo kwa uhalali wa mtu kuingia kwenye jengo la ibada akiwa na viatu miguuni mwake.
Katika hoja yake hiyo Deedat kama ilivyo wanaharakati wengine wa uenezi wa Uislam hivi leo ananukuu kile anachokiita kuwa ni ushahidi wa katazo hilo la kusali na viatu katika kitabu hiki cha nabii Musa ndani ya Biblia:-
Kutoka 3:4-5 "Bwana alipoona kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa’ Musa’ naye akasema mimi hapa. (5) Naye akasema, usikaribie hapa. Vua viatu vyako miguuni mwako, maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu."
​
Katika maandiko ya kitabu cha msahafu pia maelezo ya kisa hicho cha Musa yamenukuliwa kama tunavyosoma:-
Qur an 20:11 "Basi alipofika akaitwa, ewe Musa, bilashaka mimi ndiye Mola wako’ basi vua viatu vyako kwa kuwa wewe huko katika bonde takatifu la tuwa..."
​
Hivyo kupitia maelezo ya maandiko hayo Wanaharakati hao wa uenezi wa dini wamesikika wakifundisha kwa ujasiri kuwa jamii ya Wakristo imepotoka kwa kuingia katika majengo ya ibada na viatu huku wakiacha maelekezo hayo ya Biblia kupitia tukio hilo la Musa maelekezo ambayo kwa mtazamo wao huyaona kuwa ndiyo yanayotoa muongozo wa ibada ya kusali bila ya kuvaa viatu miguuni.
​
Katika uchambuzi wa mada hii tutaangalia mawazo hayo kwa ulinganifu wa kina ili kuondokana na utata huu uliotawala katika masikio ya watu wengi.
Farsafa juu tukio hilo la Musa kuvua viatu, na je’ nini kusudi lake?
Wazo la wajenga hoja juu ya tukio hilo linaangukia moja kwa moja katika dhana ya fundisho la ibada.
​
Na kwa kiwango cha usomaji na uchunguzi wao wamejikuta wakihitimisha hoja hiyo kwa kuondoka na wazo hilo kwamba kusudi la andiko hilo lilkuwa ni kuelekeza namna ya kuabudu kwa kutovaa viatu miguuni.
Ukweli halisi
Pamoja na maelezo au niite mapendekezo ya waalimu hao mbalimbali, binafsi kadri ya uchunguzi wa kina nilioufanya ili kuelewa farsafa au muktaza halisi wa tukio hilo, nimegundua kuwa hakuna usahihi au uhalali wowote wa kuhusisha tukio hilo la Musa kuamriwa kuvua viatu machungani ( mlima horebu) na fundisho la mfumo wa ibada makanisani au kwenye majengo mengine ya ibada.
​
Ili kupata ufumbuzi wa hilo hebu turejee kwanza historia ya maisha ya Musa
Musa alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto wa mzee Amrani na mkewe mcha Mungu aliyeitwa Yokobedi, historia inaonyesha kuwa Musa alizaliwa kwa 593 KK katika bara la Afrika nchini Misri, akiwa mtoto wa miezi mitatu aliokotwa na binti wa Farao na kulelewa katika jumba la kifalme Misri (Matendo 7:20-22).
​
Musa aliishi katika himaya hiyo ya Kifalme kwa miaka 40’ yaani toka mwaka 593 KK hadi 1553 KK, na baadae alikimbilia Midiani baada ya kumuua Mmisri mmoja aliyemkuta akimpiga Mwebrania alipokuwa ameenda kutazama ndugu zake huko, na huko Midiani aliishi kwa mkwewe Yethro aliyekuwa akifanya kazi ya Ukuhani ambaye ndiye aliyemwolea binti yake mmoja wa mwisho miongoni mwa mabinti 7 aliyeitwa Sipora, Musa aliishi hapo ukweni kwa muda wa miaka 40’ tangu mwaka 1553 KK hadi 1513 KK na ndipo akiwa na umri wa miaka 80’ alitokewa akiwa machungani na kutakiwa kwenda kuwakomboa Israel toka nchi ya Misri (Kutoka 3:1-15).
​
Mambo machache ya msingi tunajifunza katika historia hiyo ya Musa.
-
Musa alikwenda kutazama ndugu zake na kukuta Mmisri akimpiga Mwebrania na ndipo akampiga Mmisri yule na kumuua ( Kutoka 2:11).
-
Kama sehemu ya makimbilio Musa akakimbilia Midiani – ambapo ni mwisho wa magharibi mwa jangwa la Arabu, Ghuba ya Akaba kuingia mkono wan chi ya Sinai kwa mkwewe aliyeitwa ‘ Reueli au Yethro.
-
Mkwe wa Musa Yethro alikuwa ni kuhani, hivyo Musa aliishi na kuhani kwa miaka “40’.
Mambo ya kiugunduzi
Kadri ya historia ya maisha na mizunguko hiyo ya Musa tunaweza kugundua mambo ya msingi yanayoweza kujenga msingi wa ufumbuzi wa mada hii, lakini kubwa zaidi ni kuwa Musa baada ya kufanya kosa lile la kuua alikimbia na kwenda kuishi kwa kuhani Yethro.
Tendo hilo la Musa kuishi kwa kuhani Yethro’ linatupa msingi wa kuelewa kusudi hasa la Musa kutakiwa kuvua viatu kama lililenga fundisho la mfumo wa ibada au la’_ufumbuzi huo tunaupata kwa kujiuliza maswali yafuatayo;-
Endpo Musa aliishi kwa kuhani’ swali Je’ nini kazi ya kuhani?
Kadri ya Biblia tunagundua kuwa kuhani kazi yake ni:-
-
Kusimamia na kuendesha ibada za upatanisho wa dhambi kadri ya mfumo na utaratibu uliowekwa na Mungu katika hekalu la dunia/ kwa kifupi ni msimamizi na mwendeshaji wa ibada.
Hivyo kutokana na jukumu hilo la kuhani tunaweza kupiga picha ifuatayo juu ya maisha ya Musa akiwa kwa kuhani huyo tukilinganisha na tukio la mlima Horebu, kwa kuzingatia mwenendo wa maisha ya makuhani kuwa:-
-
Kwa kuishi huko na kuhani’ basi huenda nabii Musa alikuwa akihusishwa au kushiriki katika maisha ya ibada za nyumbani kwa kuhani huyo kwa kuzingatia msimamo wa makuhani katika matendo ya kidini tokea katika ngazi ya familia.
-
Kwa hali hiyo kama kuvua viatu ingalikuwa ni sehemu ya mfumo wa ibada basi Musa angekuwa ameshajifunza au kuona kwa kuhani huyo Yethro’ katika ibada za nyumbani na hivyo kusingekuwa na haja ya Mungu kutoa maelekezo tena kwa Musa juu ya kuvua viatu pale Horebu endapo pia kusudi la kuwepo kwake kule porini lingekuwa ni kutekeleza matendo ya ibada.
Lakini pamoja na hoja hizo za msingi bado inapaswa ieleweke kuwa tukio hilo la agizo la kuvua viatu kwa Musa lilitolewa kwa Musa pindi akiwa katika shughuli za kawaida za kimaisha za kuchunga wanyama tena kipindi ambacho bado hakuwa na nafasi yeyote ya utumishi kwakuwa uteuzi wake ulikuwa bado, na kwa hali halisi Musa alikuwa mlimani tena kwenye mapori kwakuwa alikuwa akilisha wanyama na hakuwa kanisani wala katika eneo la mazingira ya kiibada.
​
Pamoja na hayo kile kinachoonekana kuwachanganya wapendwa wangu na ndugu Waislam ni agizo tu kwa Musa kutakiwa kuvua viatu vyake, na kwa hali hiyo kulichikulia kwamba tendo hilo kuwa ndicho kinapaswa kuwa kielelezo cha mifumo ya ibada zetu za makanisani na katika majengo mengine ya ibada.
​
Sababu ya kina / kwanini kuvua viatu katika Biblia?
Kile nilichotangulia kusema awali ni swala la uaminifu na moyo wa dhati katika kusoma maandiko, kimsingi Biblia ina majibu kwa kila swali la imani hivyo jukumu letu ni kuichunguza kwa makini tu.
​
Na katika kufikia kina halisi cha uchunguzi wa neno la Mungu hasa kwa hoja zenye utata kama hii, ni vyema kanuni ya usomaji wa Biblia inayoelekezwa na kitabu cha Mhubiri ikazingatiwa.. rejea: Mhubiri 7:27 Tazama, asema mhubiri, “mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha na hili, ili kuitafuta jumla.”
​
Mhubiri anaweka bayana kuwa kanuni ya msingi katika usomaji wa maandiko imejengwa katika mfumo wa kanuni ya kulinganisha maandiko mbalimbali katika harakati za kutafuta fafsiri au maana ya kile ulichosoma, na kwa kutumia kanuni hiyo ya Biblia nitaomba sasa tuungane kusoma nukuu hii ya andiko la kitabu cha nabii Ruthu ili kugundua chimbuko na sababu ya kina juu ya tamaduni hii ya kuvua viatu, na yakuwa ilikuwa na madhumuni gani basi kwa wana wa Israel na hata Mungu amtokee Musa kwa kuanza na agizo hilo hilo la kuvua viatu.
Ruthu 4:7 Basi ilikuwa desturi zamani za kale katika Israel, kwa habari za kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israel.
​
Pamoja na kwamba kinachoshikiliwa zaidi na wajenga hoja ni utakatifu wa eneo kuwa ndiyo sababu iliyofanya Musa kutakiwa kuvua viatu, lakini kile anachoeleza Ruthu ndiyo sababu ya kiasili na kina hasa, kwakuwa kimsingi Biblia kama tutakavyoona mbele bado tena inaonyesha Mungu akiagiza yeye mwenyewe na wakati mwingine kupitia malaika akiwataka manabii na mitume kuvaa viatu vyao katikati ya utakatifu na uwepo wake.
Katika andiko hilo nabii Ruthu anataja mambo kadhaa yanayolengwa au kukusudiwa katika tendo la kuvua viatu kama ifuatavyo:- Ruthu 4:7.
-
Ilikuwa ni utekelezaji wa desturi ya zamani katika Israeli
-
Ilikuwa ni uthibisho wa utayari wa kazi ya kukomboa au mambo ya rehani.
-
Ilikuwa ndiyo ishara ya kuthibitisha mambo katika Israeli
Kwa kile kinachomaanishwa kupitia tendo hilo la kuvua viatu kwa Waisrael kadri ya ufafanuzi wa andiko hilo la Ruthu, utangundua kuwa wale wanaojenga hoja ya kuwalaumu wale wanaoingia katika majengo ya ibada na viatu hivi leo, wanafanya hivyo ikiwa ni matokeo tu ya kutotumia muda wa kutosha kuchunguza mambo kwa kina kabla ya kuibua hoja au mafundisho.
​
Hivyo kile alichofanya Musa kwa kutii agizo hilo la kuvua viatu ilikuwa ni kuonyesha utayari wake wa kuwa kiongozi wa njia kwa Wana wa Israel katika harakati za kuwakomboa toka katika utumwa wa Farao. Vinginevyo kama dhana kuu ingekuwa ni utakatifu wa eneo basi tungekuwa na swali la kujiuliza kwamba:-
“Kwakuwa nchi yote ilikuwa ni takatifu je’ Musa alihifadhi viatu hivyo wapi? Au je ni wapi imeandikwa kuwa Musa alikimbia kutoka nje ya ardhi hiyo ya Horebu kwenda kutupa viatu vyake ili kutonajisi utakatifu wa eneo hilo?”
Na kwa msingi huo basi ni bayana kuwa tendo hilo la kuvua viatu lililenga zaidi kupima utayari wa Musa kwaajili ya kupatiwa jukumu hilo la kuwakomboa wana wa Israel kama ambavyo kitabu cha Ruthu kinaeleza kuwa ilikuwa ni uthibisho pia kwa habari ya kukomboa.
​
Hata hivyo kwajumla tukio lenyewe halikuwa tukio la Musa kuabudu au kufundishwa mfumo wa ibada badala yake kile kinachoonekana hilo lilikuwa ni tukio la kumtawadha nabii Musa kwa jukumu la kukomboa watu wa Mungu.
Tukio kama hilo linaweza kufanana na kile tunachofanya mara kadhaa tunapokamilisha kuchagua viongozi wetu kwa upande wa uongozi wa Serikali..
Jifunze kwa mfano;
Kwa kawaida huwa baada ya kumchangua raisi wa nchi pamoja na taratibu nyingine, huwa anapoapishwa huonekana pia akivalishwa shuka begani na kushikishwa ngao na mkuki na wazee wa jadi kisha kuketi katika kigoda.
Kimsingi tendo hilo ni tendo linalotendwa kwa siku moja tu likiwa na lengo la kutoa kiashiria kuwa huyo aliyeko mbele sasa ni kiongozi wa nchi. Na baada ya hapo kiongozi huyo huvua mavazi hayo na kuendelea na majukumu yake....
Hivyo kile kilichotendeka kwa Musa kama ilivyo kwa tamaduni zetu hizo, ni tukio la kutawadhwa na kuthibitishwa kuwa sasa ni kiongozi wa umma wa Israel na hivyo matukio hayo ya kumthibitisha maana yake inakomea katika eneo husika la tukio hilo... hivyo kwamaana hiyo tendo hilo lisingepaswa kuhusianishwa na mifumo ya kawaida ya ibada.
Je’ Musa alivua viatu katika matendo halisi ya ibada katika utumishi wake?
Hii ni moja ya sehemu muhimu sana katika uchambuzi wa mada hii, katika sehemu hii ndipo pia tunaweza kukaza wazo la msingi juu ya dhumuni hasa la agizo la Musa kuvua viatu kama tulivyokwishaona hapo nyuma, kwakuwa kimsingi kama agizo hilo lililenga mfumo endelevu wa ibada basi niwazi kwamba hatutarajii kuona Mungu huyo huyo akitoa agizo jingine la kumtaka tena Musa kuvaa viatu katika matendo ya ibada.
Lakini hapa ni kinyume, na ndipo pia tunakuwa bayana na kuona ukweli wa uchambuzi tuliofanya hapo nyuma na kuona jinsi ambavyo tukio hilo halikulenga kuelekeza mfumo wa ibada ya kuvua viatu katika majengo yetu.
​
Matukio ya mbele yote yanayohusu ibada za nabii Musa yanataja jinsi Musa alivyofanya au kuruhusiwa kuyafanya ibada zake akiwa amevaa viatu vyake, na tukio kubwa maarufu zaidi ni lile la ibada ya kwanza ya pasaka katika nchi ya Misri, kumbuka ibada hiyo ndiyo imefanya msingi wa ibada ya leo ya pasaka kupitia kafara ya damu ya Yesu ambayo inaadhimishwa na Wakristo karibu katika makanisa yote. Ibada hii Musa aliambiwa aifanye akiwa amevaa viatu...
​
Kutoka 12:11-12 Tena mtamla hivi, mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, “mmevaa viatu vyenu miguuni”, na fimbo zenu mikononi mwenu, nanyi mtamla kwa haraka ni pasaka ya Bwana (12) maana nitapita katika nchi ya misri usiku huo.....
Maelezo hayo ya Biblia ni bayana, tena Mungu mwenyewe kwa kinywa chake anamwagiza nabii Musa kuendesha ibada ya pasaka na tena basi ibada hiyo anatakiwa kuifanya yeye na Wana wa Israel wakiwa wamevaa viatu vyao.........
Kwa andiko hilo tungeweza hata kuhitimisha mada hii kwakuwa kila kitu sasa kiko bayana, lakini tunaweza kuendelea kufanya mikazo zaidi ili kwamba ndugu msomaji wangu umalize mashaka yote juu ya hili, na basi kwa kulinganisha agizo lile la kuvua viatu lililodhaniwa kuwa ndiyo fundisho la mfumo wa ibada na tukio hili halisi la ibada tunaweza kujiuliza maswali ya fuatayo:-
-
Kama tendo la Musa kuambiwa vua viatu vyako lililenga mambo ya ibada na kumtaka Musa awe akivua viatu katika matendo ya ibada, je’ sasa ni Mungu yupi tena anayemtaka Musa kuvaa viatu katika ibada hiyo ya pasaka na tena Mungu huyo akiahidi kupita hapo Misri usiku huo na huku tayari wana wa Israel wakiwa wamevaa viatu vyao?
-
Na je’ inaaminisha nini vitabu vyetu vinapomtambulisha Mungu kuwa si mwenye kigeugeu endapo kama maagizo hayo ni ya kujipinga? Rejea; (Qur an 17:77/ Yakobo 1:16-18)
Ndugu msomaji wangu hayo ni maswali ya changamoto na kumsha ufahamu wetu, lakini kama tulivyokwishaona ni kuwa kamwe agizo lile la kuvua viatu halikulenga kuelekeza mfumo wa ibada kwa Wakristo , na badala yake ilikuwa ni tukio la kumtawadha Musa ili kupewa dhamana ya kuwakomboa Israeli toka utumwa wa Farao. (Rejea’ Ruthu 4:7 Basi ilikuwa desturi zamani za kale katika Israel, kwa habari za kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israel.)
Nabii Musa akiwa jangwani Baada ya kutoka Misri chini ya nabii Musa wana wa Israel walikuwa na mikutaniko mbalmbali ya kiibada Jangwani...
Qur an 7:138 Na tukawavusha wana wa Israil baharini ( wakasalimika na balaa za Firauni) na wakawafikia watu waliokuwa wakiabudu masanamu yao. Wakasema “Ewe Musa! Tufanyie waungu na sisi ( yaani masanamu....(Nabii Musa akasema) Hakika ninyi ni watu mufanyao ujinga...........
Matendo 7:38 Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani, pamoja na yule malaika aliyemtokea..
Maandiko hayo kimsingi yanaweka bayana juu ya kuwepo kwa matendo ya ibada kwa wana wa Israil baada ya kuvuka bahari ya shamu na kuendelea na msafara jangwani, andiko la Qur an linataja jaribio la watu waasi kuwataka wana wa Israel kujihusisha na ibada ya sanamu tendo linalotajwa na Qur an kuwa lilikataliwa na nabii Musa.
Kwa upande mwingine maandiko ya Biblia nayo yanaonyesha kuwa wana wa Israeli walikuwa katika umoja wa kanisa ambao kimsingi ni umoja wa watu walioitwa kutoka gizani na kujiunganisha pamoja wakimwabudu Mungu.(Greec: Ekllessia)
Habari gani juu ya viatu?
Kumbukumbu 29:4-5
-
Lakini Bwana hakuwapa macho ya kuona..
-
Name miaka arobaini nimewaongoza jangwani..
-
Nguo zenu hazikuchakaa mwilini..
-
Viatu vyenu havikuchakaa miguuni mwenu...
Andiko hilo la kumbukumbu linaonyesha muujiza ambao Mungu aliwatendea wana wa Israeli, ambapo miongoni mwa matendo hayo ya miujiza ni tendo la kufanya viatu vya wana wa Israel kutochakaa katika miguu yao, kipindi chote cha miaka arobaini ya jangwani.
Hivyo hoja ya msingi hapo ni kuwa kumbe wana wa Israel wakiwa hapo jangwani bado walikuwa na viatu, swali la msingi ni kuwa:-
je’ ni mahali gani katika maandiko ambapo Mungu aliwalekeza wana wa Israel waingiapo kwenye kanisa la jangwani wawe wanavua viatu hivyo vinavyotajwa?
Na endapo ushahidi huo wa kutakiwa kutovaa viatu hivyo wakati wa ibada basi wale wanaojenga hoja ya kukosoa wanaoingia na viatu hawatakuwa na uhalali wa kujenga hoja hiyo kwakuwa ni hoja isiyo na utetezi wa kimaandiko.
Je’ mtume Muhammad naye alisali na viatu au bila viatu?
Hii ni hoja ya msingi sana katika uchambuzi wote wa mada hii, kwakuwa pamoja na mitazamo yetu juu ya maswala ya kidini lakini tunakubaliana kuwa manabii tunaowaamini kadri ya makundi ya imani zetu ndiyo wanaotoa sura nzima ya kanuni na masharti juu ya mwenendo wa wafuasi katika imani zao hivyo kadri ya vile inavyoaminika kuwa wao hupokea maelekezo kwa Mungu...
Hivyo katika kipengele hiki tutaangalia kwa upana wake juu ya ibada za mtume Muhammad anayeaminiwa na jamii ya ndugu zetu Waislam ili kuona naye anatoa kielelezo gani kitakacho tusaidia kupata suluhisho la utata wa hoja hii katika ulimwengu wetu wa imani. Maandiko mawili ya msingi katika Qur an ndiyo yatakayotupatia kanuni na njia ya kutafiti hoja hii:-
Qur an 33:21
Bilashaka mnao mfano mwema (riwadha nzuri) kwa mtume wa Mwenyezi Mungu....
Katika andiko hilo la kwanza tunaona kuwa Qur an ikimtaja Muhammad kama ndiye anayepaswa kuwa mfano au kilelezo katika matendo ya kidini na hivyo jamii ya Waislam inapaswa kuiga toka kwake.
Andiko hilo pamoja na mambo mengine linatupatia kibali au uhalali wa kuchunguza ili kuona mwenendo wa ibada za mtume Muhammad mwenyewe ambazo kimsingi ndizo zinapaswa kuigwa na wapendwa wetu Waislam. Hata hivyo ni vyema ieleweke kuwa maandiko ya masahafu wa Qur an hayataji kwa upana mwenendo wa matendo ya ibada ya mtume, lakini yanatoa mwongozo wa kanuni ya kufanya. Hebu soma ayah ii:-
Qur 42:10
Mkihitirafiana katika jambo lolote, rejeeni katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na hadithi za mtume.
Hivyo njia inayotajwa na andiko hilo ni kutafuta ufumbuzi juu ya hoja yeyote kwa kurejea katika vitabu vilivyo nje ya Qur an vilivyopitishwa kama vitabu halali vya teolojia ya Uislam, vinavyoitwa vitabu vya hadithi.
Hebu sasa tuandalie katika vitabu hivyo vya hadithi kuelewa ukweli huo:-
Nukuu 1’ Book’ Sahih Al-Bukhari (Arabic English – Dr Muhsin Khan – Islamic University, Al Medina Al Munawwra / Al Maktabat Al Salafiat)
Vol 1’ Chapter 24/ (Hadith) no 383’
Narrated Abu Maslama, Sai’id Yazid Al Azid: I asked Anas bin Malik whether the Prophet had ever prayed with His shoes on. He replied “Yes.”
Tafsiri Imesimuliwa na Abu Maslama, Sai’id Yazid Al Azid; Nilimuuliza Anas bin Malik endapo mtume alishawahi wakati wowote kusali na viatu vyake. Akajibu“ Ndiyo.”
Simulizi hiyo isiyo na maneno mengi inaweka bayana juu ya namna mtume Muhammad alivyoendesha ibada zake za swala, na yakuwa kumbe Muhammad mwenyewe aliabudu na viatu vyake na hakuwa akivua viatu wakati wa ibada.
Hebu tuone nukuu nyingine:
Book’ Sahih Al-Bukhari (Arabic English – Dr Muhsin Khan – Islamic University, Al Medina Al Munawwra / Al Maktabat Al Salafiat)
Vol 1’ Chapter 25/ (Hadith) no 384 / 385
(384)Narrated Ibrahim: Hammam bin Al Harith said, “I saw Jarir bin ‘Abdullah urinating. Then he performed ablution and passed his (wet) hands over his Khuffs, stood up and prayed. He was asked abaut it. He replied that he had seen the Prophet doing the same.” ......
Tafsiri Imesimuliwa na Ibrahimu; Hammam bin Al Harith alisema, nilimuona Jarir bin‘ Abdallah akiungana na wengine na kisha akatawadha na kupitisha mkono uliolowa maji juu ya viatu vyake, kisha akasimama na kuswali. Alipoulizwa juu ya hilo. Alijibu kwamba alimuona mtume akifanya kitendo kama hicho”.....
(385)Narrated Al –Mughira bin Shu’ba: Ihelped the Prophet in perfoming ablusion and passed his wet hands over his kuhuffs and prayed.
Tafsiri
Imesimuliwa na Al – Mughira bin Shu’ba: nilimsaidia mtume katika kutawadha na ndipo akapitisha mikono yake iliyoloana juu ya viatu vyake na kusali.
Kwajumla haditi zote hizo zinazotambuliwa na kukubalika katika teolojia ya Uislam, zinaweka wazi juu ya hali halisi ya mfumo wa ibada wa mtume Muhammad kuwa desturi yake ilikuwa ni kusali akiwa na aina hiyo ya viatu vyake vinavyotambuliwa kama Khuffu’ hivyo hoja hiyo iko bayana kabisa.
Bwana Yesu / Manabii na Mitume katika farsafa ya ibada na kuvaa viatu.
Nikualike ndugu msomaji wangu tunapolekea ukingoni mwa achambuzi wa mada hii baada ya kujipatia majibu ya msingi juu ya hoja hii ya kusali au kutokusali na viatu.
Katika sehemu hii ya mwisho tutapitia kwa kifupi ili kuona jinsi mitume na manabii walivyotenda huko nyuma kwa habari ya matendo mbalimbali ya kidini na swala hili la uvaaji wa viatu, hii ikiwa ni pamoja na kujibu hoja ya msingi inayohusiana na dhana kwamba huenda panapokuwepo utakatifu basi viatu havipaswi kuwepo.
Hebu kabla hatujaenda mbali turejee kidogo kuangalia matukio machache ya manabii katika uhusiano na swala la uvaa wa viatu.
Ezekieli 24:17
Ugua lakini si kwa sauti ya kusikiwa, usifanye matanga kwaajili yake aliyekufa; jipige kilemba chako; ukavae viatu vyako.....
Katika andiko hilo nabii Ezekieli anaelekezwa na Mungu juu ya kanuni sahihi ya ibada na hapo hoja kuu ilikuwa ni juu ya ibada ya maombolezo, katika maelekezo yake kwa Ezekiel Mungu ana ainisha yaliyo sahihi kufanyika katika ibada hiyo ya maombolezo nay ale yasiyopaswa kufanyika..
Yaliyokatazwa:
-
Ugua lakini si kwa sauti ya kusikiwa
-
Usifanye matanga kwaajili ya aliyekufa
Yaliyoruhusiwa”
-
Jipige kilemba chako ( hiyo ni kadri ya desturi ya Kiyahudi)
-
Kavae viatu vyako..
Hivyo kadri ya andiko hilo Mungu mwenyewe ndiye anayetoa maelekezo kwa Ezekieli kumkumbusha kuvaa viatu vyake katika ibada hiyo ya maombolezo, na maelekezo hayo yalifuatia baada ya kumjulisha yasiyopaswa kufanywa katika ibada hiyo ya maombolezo, na hivyo basi tendo la kuvaa viatu linaangukia katika upande ule wa matendo yaliyoruhusiwa kufanywa wakati wa ibada hiyo ya maombolezo, hivyo hakukuwa na shida yeyote ya swala la uvaaji wa viatu mbali na tukio tu la Musa lililolenga kumtawadha kuwa kiongozi wa Israel
Kisa kingine katika Biblia ni kile kinachomhusu nabii Isaya ambaye aliagizwa kutembea akiwa hana viatu tena uchi, ikiwa ni tukio la kidini la kuonya juu ya uovu wa wanadamu na ugumu wao wa kuamini na kutubu, tendo hilo lililohusisha pamoja na kutembea uchi lakini Isaya kutotakiwa kuvaa viatu linatajwa na Biblia kuwa ni tendo la Ishara ya ajabu. ( rejea Isaya 20:3)
Je” eneo lenye utakatifu viatu haviruhusiwi?
Hii ni hoja ya msingi kuiangalia walau kwa kifupi, sababu ya kuangalia hoja hii pamoja na mambo mengine lakini ni tendo la kigezo hiki kuchukuliwa kama ndiyo sababu kuu ya kukaza madai ya kuvua viatu wakati wa ibada.
Lakini katika sehemu hii tutaona kisa kimoja tu kinachotoa jibu zima la hoja hii nacho ni kile kinachohusu tukio la Petro gerezani; hebu tuone kwa kifupi:-
Matendo 12:5-9
-
Petro alikuwa amefungwa gerezani..
-
Kanisa lilikuwa likomba kwaajili yake..
-
Malaika alitumwa kumtoa Petro gerezani..
-
Ndipo chumba cha Petro “kikajaa nuru kutoka mbunguni”....
-
Akiwa katika nuru hiyo (takatifu) ya mbinguni, Malaika akamwamuru avae viatu vyake kisha amfuate....
Kisa hicho cha Petro kinajibu hoja hiyo bila ya kuacha swali lolote, kadri ya kisa hicho Biblia inaweka wazi kuwa mara Malaika alipoingia tu kwenye chumba cha gereza ndipo nuru ikafurika mle mchumbani, na jambo la kushangaza ni tendo la Malaika katikati ya nuru hiyo anamwagiza Petro kuvaa viatu vyake’ yaani maana yake ni kuwa Petro alivaa viatu hivyo huki akizungukwa na nuru hiyo takatifu aliyokuja nayo Malaika toka mbinguni.
Hivyo hiyo ni kumaanisha kuwa hapakuwa na tatizo lolote juu ya uwepo wa viatu katika nuru hiyo takatifu ya mbinguni iliyofurika katika chumba hicho cha gereza, na kubwa zaidi ni tamko la Malaika lililomtaka Petro kumfuata mara baada ya kumaliza zoezi la kuvaa viatu yaani kwa lugha nyingine ni kuwa Malaika bado aliendelea kumtaka Petro kudumu katika mafuriko ya nuru hiyo akiwa na viatu vyake kwa tendo hilo la kudumu kuambatana naye hadi nje ya gereza hilo.Wito wangu kwa watu wa Mungu bado ni kuwasisitiza kusoma maandiko kwa usahihi, ili kuepuka kuwaondoa wengine kwenye hali ya Mungu.
Kwa ushahidi huo ni wazi hakuna tatizo kuingia na viatu mahala penye utakatifu.
Hakuna ushahidi wa Yesu kuvua viatu katika majengo ya ibada.
Biblia inaonyesha kuwa Yesu alikuwa akivaa viatu na hakuna mahali alipovua viatu hivyo ili kutekeleza kwanza matendo ya ibada, ni vyema ikiwa ni mkristo au hata kama ni Muislam kuzingatia kuwa hoja yoyote unayojenga ikiwa ina lengo la kutaka kuonyesha mapungufu ya Wakristo katika utekelezaji wa maamrisho ya kidini, lazima kwanza hoja hiyo iwe na vyanzo vya kimandiko ikihusisha maelekezo ya kiongozi mkuu wa Ukristo yaani Bwana Yesu mwenyewe.
Rejea; Qur an 5:47
Watu wa injili wahukumu kwa yale aliyotelemsha Mwenyezi Mungu ndani yake, na wasiohukumu kwa (kufuata) yale aliyotelemsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio maasi.
Andiko hilo la Qur an linaweka bayana kuwa hukumu zozote dhini ya watu wa Injli zinapaswa kutokana na msingi wa Injili yenyewe, hivyo hii ni kumaanisha kuwa kama swala la kusali na viatu lingekuwa linapingana na msingi wowote wa mafundisho ya Injili ya Yesu basi hoja hiyo ya kusali na viatu ingekuwa sahihi na yenye nguvu.
Hivyo hii ni tofauti na wale wanaohoji leo kuonekana kutokuwa na kipengele chochote cha kusonda jamii ya Wakristo katika hoja hii kuwa kwa tendo la kusali na viatu wamekiuka kanuni Fulani zilizoamriwa na maandiko hayo.
Lakini badala yake tunaona Yesu mwenyewe akiwa na viatu ambavyo hakuna kifungu cha maandiko kinachoonyesha kuwa aliwahi kuvua viatu hivyo kwaajili ya kutekeleza ibada;
Matendo 13:25....Siwezi kulegeza viatu vya miguu yake...
Hitimisho:Nichukue fursa hii mpendwa msomaji wangu kukushukuru kwa kutumia muda wako kufuatilia uchambuzi huu, ni wito wangu endapo hapo nyuma uliyumbishwa kiufahamu juu ya hoja hii sasa usimame imara, na kama huenda hukuwahi kuwa Mkristo na huenda hoja hii ilichangia kusitisha maamuzi yako sasa fungua moyo wako umpokee Yesu.
Biblia inamaliza kwa kusema:
Yeremia 2:25 Zuia mguu wako usikose kiatu.......