top of page

Gundua

bible-study-lesson-tips-small-group-lead
Ugunguzi.jpg

Miongozo Mbalimbali

bible-png-clipart-12.png

26. JE! MUNGU ANAO UJUMBE WA PEKEE KWA AJILI YA SIKU ZETU?

Ramon Umashankar alizaliwa katika tabaka ya juu ya Kihindu (Brahmin). Wakubwa wake kwa umri walimfundisha akiwa na umri ndogo ya kwamba yeye alikuwa mungu, na ya kwamba ili kuufikia uungu wake ni lazima afanye mazoezi ya yoga na kutafakari. Yeye kama kijana mbichi [tineja], Ramon alianza kushangaa kama kweli angempata Mungu kupitia kwa sanamu zile mbali mbali zilizoabudiwa katika mahekalu ya Kihindu [Kibaniani].

Ramon akaanza kuichunguza Biblia na madai ya Kristo. Yeye alikuwa amemheshimu Yesu siku zote kwa unyenyekevu wake aliokuwa nao, lakini sasa Ramon akasikia kwamba huyo Yesu alidai kwamba alikuwa ndiye Mwana pekee wa Mungu. Tena aligundua kwamba Wakristo wengi walionekana wanayo amani ambayo kutafakari kwa miaka mingi kulikuwa kumeshindwa kuifikia. Lakini, Ramon bado alikuwa amedhamiria kuipata kweli katika dini yake ya Kibaniani.

Lakini baadaye aliiona filamu iliyoonyesha maisha yake Kristo. Kwa mara yake ya kwanza alitambua kwamba Yesu alikuwa amepatikana na mateso na hofu kama mwanadamu. Kabla ya hapo alikuwa amedhani kwamba Yesu kwa njia fulani alikuwa ametumia uweza wake wa Uungu kuyakwepa maumivu yale yaliyotokana na kusulubiwa kwake. Lakini sasa, alishindwa kueleza habari za msalaba ule. Alishangaaa na kujiuliza-uliza: Hivi ilikuwa-kuwaje huyo Yesu aliweza kuyapitia mateso makubwa kama yale - kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi?

Ramon alipoendelea kutafakari juu ya kifo cha Kristo, alizidiwa nguvu kwa kudhihrishwa kwa upendo kama ule. Aliamua kukitupilia mbali cheo chake kinachotamaniwa sana na watu wa Brahmini [tabaka la juu la Kibaniani] na kutoa maisha yake kwa Yesu, Mwokozi wake. Alipoyalinganisha mambo yote na ule upendo wa kujitoa mhanga wa Kristo, Ramon alisema hivi, "Kila kitu cho chote kingine kikasambaratika."

Mbrahmini huyo kijana alikigundua kiini cha ile kweli ya Ukristo: yaani, Yesu Mwokozi wa ulimwengu.

1. Dini Ipi Inaokoa?

Yesu ndiye Njia - njia pekee - ya wokovu.

"Wokovu haupatikani katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo." - Matendo 4:12.

Biblia inafundisha wazi kwamba sisi tumepotea katika dhambi, na hivyo tunakabiliwa na adhabu ya dhambi: yaani ile mauti (Warumi 6:23). Wote wametenda dhambi (Warumi 3:23), kwa hiyo wote wanakabiliwa na hiyo mauti. Na Yesu ndiye yule mmoja - mmoja pekee awezaye kutuokoa sisi kutoka katika laana ya dhambi.

"Kila mmoja amtazamaye Mwana na kumwamini yeye atapata uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho" - (Yohana 6:40).

Kuna dini moja tu ya kweli:
"Bwana mmoja, IMANI MOJA, ubatizo mmoja" - (Waefeso 4:5).

 

2. Je! Mungu Anao Ujumbe Wa Pekee Kwa siku zetu?

Ndiyo! Ujumbe huo wa aina tatu unaonekana katika Ufunuo 14:6-16. kutangazwa kwa ujumbe huo uliotolewa na malaika hao watatu kunafikia kilele chake wakati ule wa kuja mara ya pili kwa Kristo (fungu la 14-16).

Ujumbe wa Malaika wa Kwanza.


"Kisha nikamwona malaika mwingine, akiruka juu ya anga akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote na watu wa lugha zote na rangi zote. Naye akasema kwa sauti kubwa, "Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na nchi, bahari na chemchemi za maji" - (Ufunuo 14:6,7).

Ingawa Maandiko yanaonyesha picha ya kuvutia ya ujumbe huo wa aina tatu kwa njia ya mfano wa hao malaika watatu, watu wa Mungu ndio wajumbe hasa wautangazao kwa ulimwengu mzima. Hawahubiri injili mpya, bali "injili ya milele" kwa ulimwengu mzima- yaani, kwa kila taifa na kabila na lugha na jamaa. "Injili ya milele" ya Kristo ni ujumbe ule ule wa wokovu ambao watu katika kipindi kile cha Agano la kale waliupokea " kwa imani" (Waebrania 3:16-19; 4:2; 11:1-40); ni mafundisho yale yale aliyoyatangaza Yesu mwenyewe; ni injili ile ile iliyounguruma katika karne zile zote za kipindi cha Kikristo.

Injili hiyo rahisi, iokoayo, ya Yesu Kristo ilikuwa karibu imetoweka kabisa katika Kanisa kwa zaidi ya miaka elfu moja katika kipindi cha zama za giza (Dark Ages), lakini matengenezo ya Kanisa (Reformation) yaliifufua, na watu wa Mungu wanaihubiri ulimwenguni kote leo. Malaika wa kwanza anatangaza ujumbe wa injili iyo hiyo, lakini inahubiri katika mwelekeo mpya - yaani, wa ulimwengu mzima - kwa ajili ya watu wanaoishi kabla tu ya kuja Yesu mara ya pili.

Wale wanaoupokea ujumbe huu wanajikuta wanaitwa ku "mch[a] Mungu na kumtukuza [kuakisi tabia yake]." Wanauonyesha ulimwengu tabia ya Mungu ya upendo, sio tu kwa maneno yao, bali pia kwa maisha yao yenye ushuhuda wenye nguvu. Wanatoa ufunuo wa kusisimua wa kile Mungu awezacho kufanya kupitia kwa watu waliojazwa na Roho wa Kristo.

Hivi ni lini utakapotangazwa huo ujumbe wa malaika hao watatu katika ulimwengu mzima? Wakati saa ya "hukumu yake [Mungu] imekuja." Mwongozo 13 unaeleza kwamba Yesu alianza kazi ya hukumu inayotangulia kabla ya kuja kwake katika mwaka ule ule, yaani, 1844, Yesu aliwavutia watu ulimwenguni kote kuanza kuhubiri ujumbe huo wa Ufunuo 14.

Ujumbe huo unatuagiza sisi ku"msujudi[a] yeye aliyezifanya mbingu, [na] nchi" [Ufunuo 14:7]. Mungu anatutaka sisi ku "ikumbuk[a] siku ya Sabato [t]uitakase" kwa sababu "kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi" (Kutoka 20:8-11). Katika mwaka ule wa 1844 Darwin alipokuwa anaitoa nadharia yake ya evalusheni [kutokea vyenyewe tu vitu vyote], Mungu alikuwa anawaita watu wake kurudi na kumsujudia yeye kama Muumbaji wao. Wakati ule ule hasa, wale waliokuwa wakiuhubiri ujumbe huo wa malaika watatu waliigundua Sabato ya siku ya saba ya neno la Mungu, nao wakaanza kuitunza kwa kumheshimnu Muumba wa Mbingu na Nchi.

(2) Ujumbe wa malaika wa pili.
"Malaika wa pili akafuata, akasema, 'Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, uliowafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uasherati wake unaowafanya kuwa vichaa.!! - ufunuo 14:8.

Malaika wa pili anaonya anasema, "Umeanguka Babeli Mkuu." Ufunuo 17 unaonyesha picha ya "Babeli" ya kiroho - yaani, Ukristo ulioasi - kama mwanamke kahaba (fungu la 5). Anasema akiwa tofauti na mwanamke safi wa Ufunuo 12 anayeliwakilisha kanisa la kweli la Kikristo. Mwanamke anayewakilisha Babeli ni mwanamke aliyeanguka [aliyeasi] ambaye aliwafanya "mataifa yote kunywa mvinyo wa uasherati wake unaowafanya kuwa vichaa." Mvinyo wa mafundisho ya uongo umeenea kote katika mfumo potofu wa Ukristo. Ujumbe huo wa malaika wa pili unawaita watu wa Mungu kuyapinga mafundisho hayo ya uongo ya Ukristo huo ulioasi.

Babeli unawakilisha mseto wa mifumo mingi ya Ukristo ulioasi. Ni wa hatari mno kwa sababu unaipotosha picha ya Mungu na kuifanya kama vikaragosi [sanamu za kuchekesha]: yaani, unamfanya Mungu kuwa ni mlipiza kisasi na mwenye madai mengi, unamfanya Mungu kama babu yetu mwenye upendo ambaye ni mwema mno kuweza kumsumbua mtu awaye yote juu ya dhambi zake. Kanisa lenye afya litatoa picha yenye uwiano mzuri wa sifa zote za Mungu, kisha litaonyesha jinsi haki na rehema yake inavyofungamana na kweli isemayo kwamba Mungu ni upendo.

Mungu anawaita watu wake anasema "tokeni" Babeli (Ufunuo 18:4), anataka wayakatae mafundisho yale yasiyotoka katika Biblia, kisha wayafuate mafundisho ya Kristo.

(3) Ujumbe wa malaika wa tatu
"Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake, yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemininwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo. Moshi wa moto unaowatesa hupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana. Hivyo lazima watakatifu, yaani watu wanaotii amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu" - (Ufunuo 14:9-12).

Ujumbe wa malaika wa tatu unaugawa ulimwengu wote katika makundi mawili. Upande mmoja wanasimama Wakristo waasi [ yaani, wasiofuata mafundisho ya Biblia] ambao hu "msujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea alama yake katika kipaji cha uso wake au katika mkono wake." Upande ule mwingine wanasimama wale wanaoikataa mamlaka ya mnyama, yaani. Wale "watakatifu wanaozitii amri [kumi] za Mungu na kuendelea kuwa waaminifu kwa Yesu."

Zingatia tofauti iliyopo kati ya makundi hayo mawili yanayopingana. Wale wanaoipokea alama ya mnyama ni waabudu wanaoyalegeza masharti ya imani ambao wanafuata mawazo yaliyotungwa na wanadamu yaonekanayo kama yanafaa pamoja na kuzifuata desturi zao. "Watakatifu wanatabia hizi zinazowatambulisha: "uvumilivu" utii kwa "Amri za Mungu" kisha "wanaendelea kuwa waaminifu kwa Yesu."

Baada ya ujumbe huo wa aina tatu kutangazwa ulimwenguni kote, Yesu atakuja ku "vun[a] wale waliookolewa:
"Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkononi mwake. Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, "Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameivaa". Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa" - (Ufunuo 14:14-16).

3. Kanisa La Kristo La Siku Za Mwisho
Je! umevutiwa sana na Mkristo mwenye nguvu, aliye imara, na kushangaa kuiona bidii aliyo nayo katika kumwabudu Mungu, uvumilivu wake, na imani yake, na kutamani sana kuwa na uzoefu wa kiroho unaofanana na huo? Mungu alitoa ujumbe wake wa pekee kwa ajili ya siku zetu katika Ufunuo 14 kwa sababu unaweza kuleta uzoefu wa maisha kama huo.

Kama tulivyojadili katika Mwongozo 25, Ufunuo 14:17 unawatambulisha Wakristo wa siku hizi za mwisho kuwa ni "wanaozitii amri [kumi] za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu." Ufunuo 14:12 unaeleza habari za kundi hilo kuwa ni la "watakatifu kwa Yesu."

Hebu na tufanye muhtasari wa sifa za tabia ya Wakristo wa siku za mwisho.

i. Wana"kuwa na ushuhuda wa Yesu." Hata Shetani anapoionyesha hasira yake dhidi yao, wao "wanaendelea kuwa waaminifu kwa Yesu." Imani yao haitokani na nafsi yao wenyewe ni kipawa toka kwa Mungu (Waefeso 2:8). Kanisa la Mungu la siku hizi za mwisho linamwona Kristo katika tabia yake halisi na kwa neema kwa njia ya imani wanakuwa minara hai ya ukumbusho inayoshuhudia uweza wa Kristo anayekaa ndani yao.

ii. Wanayo "imani…. Ya Yesu" ( Ufunuo 14:12, KJV). Imani aliyokuwa nayo Yesu, yaani, imani aliyoifundisha, imani aliyoiweka katika maisha yake, sasa inaijaza mioyo yao. Hawanayo tu kweli, wanai"tunza" kweli - yaani, wanaifuata. Kwao dini ni maisha, imani yao inafungamana na matendo yao, tena imani hiyo inafungamana na utii wao. Katika maisha yao ya nje wanaionyesha "imani ya Yesu." Wamekwisha kugundua ya kwamba mafundisho makuu ya Biblia, yakitumiwa katika maisha yao ya kila siku, yanawapa maisha ya Kikristo yenye nguvu. Wamegundua kwamba kweli hizo kuu za Biblia zinaamsha upendo na kicho chao kwa Kristo, mambo ambayo hukidhi haja na shauku zote za moyo wa kibinadamu.

iii. "Wanazitii amri [kumi] za Mungu" - Amri zile Kumi, yaani, sheria ya maadili ya Mungu. Juu ya mambo hayo yote mengine wanataka kutii kila alipendalo Mungu, kutii kila amri yake. Wanauonyesha upendo wao kwa Mungu na upendo wao kwa watu wengine kwa kuzifuata amri zote [kumi] za Mungu, pamoja na ile ya nne inayotuamuru kumwabudu Muumbaji wetu kwa kuiheshimu Jumamosi, yaani, Sabato ya siku ya saba.

iv. Wanautangaza ujumbe wa "injili ya milele" ulimwenguni kote (Ufunuo 14:6). Injili hutangaza kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, halafu alifufuka kutoka kaburini ili sisi tupate kuwa na kanisa la Kristo la siku hizi za mwisho limekuwa likiwaita watu kila mahali kutoka katika machafuko ya kidini na kujenga uhusiano pamoja wa ile kweli ya Biblia peke yake.

v. Wanasukumwa na hisia ya kuharakisha mambo kwa sababu "saa ya mavuno imekuja, kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa" (Ufunuo 14:15), na mamilioni bado hawajamwona Kristo.

vi. Wanajitoa kabisa kutekeleza utume waliopewa na Mungu. Kwa sababu "Babeli Mkuu" umeanguka, wao wanaendelea kuwasihi wale wanaoishi katika machafuko hayo ya kidini, wakiwaambia "Tokeni kwake, enyi watu wangu" (Ufunuo 18:4). Wanatamani kuwaeleza wengine juu ya uhusiano wa ajabu walio nao pamoja na Kristo, na furaha waliyo nayo wao kwa wao.

Yote hayo na zaidi yanaiunganisha mioyo ya mamilioni ya Wakristo wa siku hizi za mwisho walioitwa na ujumbe huo wa malaika hao watatu ili watoke. Maisha yao yenye furaha yanawafanya kujiunga na mtume Yohana kutangaza kote mwaliko huu:
"Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kujiunga nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike" - (1 Yohana 1:3,4).

Kwa njia ya Roho wake na kwa njia ya kanisa lake, Yesu anakualika wewe pia ili uje kwake na kusalimisha kila kitu kwake yeye:
"Roho na bibi-arusi [kanisa] wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, 'Njoo!' ye yote mwenye kiu na aje; na ye yote atakaye, na atwae zawadi hii inayotolewa bure ya maji ya uzima.". - Ufunuo 22:17.

4. Mavuno Ya Aina Mbili

Ujumbe wa malaika hao watatu unafikia mwisho wake Yesu anaporudi duniani kuwavuna waliookolewa wa vizazi vyote (Ufunuo 14:14-16). Yesu
anawakusanya wote waliookolewa na kuwachukua kwenda nao kule kwenye "makao mengi" mbinguni (Yohana 14:1-3, KJV). Anafutilia mbali dhambi, magonjwa, huzuni na mauti. Watakatifu wanaanza kuishi maisha mapya mazuri sana pamoja naye milele hata milele (Ufunuo 21:1-4).

Yesu atawa"vuna pia waovu wakati wa kuja kwake".
"Kisha, malaika mwingine akatoka katika hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali. Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni, akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, "Nawe tia huo mundu wako mkali ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!" Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu chombo cha ghadhabu ya Mungu. Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya maji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko wenye kina kufikia hatamu za farasi na urefu upatao kilometa mia tatu" -(Ufunuo 14:17-20).

Huo utakuwa ni wakati wa kuhuzunisha sana wa maangamizi ya milele tukio la kuhuzunisha mno kwake Kristo, kwa sababu atalazimika kuwaangamiza wale wanaokataa kuokolewa. Yesu "huvumilia kwa ajili yenu, hapendi mtu ye yote aangamie, bali kila mmoja aifikilie toba" (2 Petro 3:9).

Yesu anapokuja kuvuna mavuno ya nchi, je! wewe utakuwa katika mavuno yapi? Je! utasimama miongoni mwa nafaka iliyokomaa pamoja na waliokombolewa wa vizazi vyote (Ufunuo 14:13-16)? Au utakuwa mingoni mwa zile zabibu zilizoiva sana za ghadhabu pamoja na wale waliopotea? (mafungu 17-20).

Jambo hilo limewekwa wazi. Upande mmoja, Yesu anasimama mikono yake iliyotobolewa kwa misumari ikiwa imenyoshwa kwako, akikusihi wewe ili upate kusimama pamoja na "watakatifu wanaozitii amri [kumi] za Mungu na kuwa na imani ya Yesu" (fungu la 12). Upande ule mwingine ni sauti za wanadamu tu, zinazokusihi sana zikikuambia kwamba utii wako kwa mafundisho yote ya Biblia na kwa zile amri zote [kumi] za Mungu hauna maana.

Siku moja kundi lililokuwa katika ukumbi wa hukumu wa Pilato lilikabiliwa na jambo ambalo linafanana ajabu na hilo. Upande mmoja alikuwako Yesu, mwenye hali ya uungu-ubinadamu, yaani, Mungu-mwanadamu. Upande ule mwingine alikuwako Baraba, mtu asiye na uwezo wo wote, yaani, asiyeweza kujisaidia mwenyewe, wala waliokuwa katika kundi lile ambao walilishuhudia tukio la kuhuzunisha sana. Lakini, basi, yale maneno ya Pilato yenye amri yalipovuma katika kundi la watu wenye tabia mbalimbali, yakisema, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?" sauti nyingi za watu wale zikaunguruma kwa hasira, "Baraba!"
"Basi," akauliza Pilato nimtendeje Yesu aitwaye Kristo?"

Kwa sauti moja lile kundi likapiga makelele, "Na asulubiwe!"

Na hivyo ndivyo Yesu, asiye na hatia yo yote, alivyosulibiwa; na Baraba, mwenye hatia, akaenda zake akiwa huru. (Angalia Mathayo 27:20-26).

Je! wewe unamchagua nani leo hii, Baraba au Yesu? Je, unachagua kufuata mawazo na mafundisho yaliyotungwa na wanadamu ambayo yanagongana na amri [kumi] za Mungu, tena yanagongana na injili ya milele ya Yesu? Au wewe unataka ku"zitii amri [kumi] za Mungu na kuendelea kuwa [m]waminifu kwa Yesu?" kumbuka, Yesu ndiye anayeahidi kumtuma Roho wake Mtakatifu kutatua matatizo yako yote, kuiponya kila huzuni kubwa uliyo nayo moyoni mwako, na kuitosheleza kila shauku uliyo nayo.

 

bottom of page