top of page

Gundua

bible-study-lesson-tips-small-group-lead
Ugunguzi.jpg

Miongozo Mbalimbali

bible-png-clipart-12.png

20. SIRI YA KUKUA KWA USHIRIKIANO

Mapema katika miaka ile ya kuanzia 1960 na kuendelea, Ndugu Andrew, mtu wa Uholanzi, aliingiza kwa siri mzigo wa Biblia katika gari lake la Volks Wagen (Folks Vageni) na kuvuka mpaka wa Romania na kuwapita walinzi wa kikomunisti. Alipanga katika hoteli moja na kuanza kuomba kwamba Mungu amwongoze kwenda kwenye makundi ya Kikristo yanayofaa - yaani wale ambao wangeweza kuzitumia vizuri sana zile nakala zake za Maandiko.

Mwisho wa juma lile Andrew alitembea kwenda kwa karani wa hoteli ile na kumwuliza angeweza kulipata wapi kanisa.

Yule karani akamwangalia kwa njia isiyo ya kawaida kidogo na kujibu, "Hatunayo mengi ya hayo, unajua. Isitoshe, usingeweza kuielewa lugha yetu"
"Je! Wewe hukujua?" akajibu Andrew, "ya kuwa Wakristo wanazungumza lugha ya ulimwengu mzima."

"Ehee! Ni lugha gani hiyo?"
"Inaitwa Agape [Upendo]"

Yule karani alikuwa hajapata kuisikia kamwe, lakini Andrew alimhakikishia kwa kusema hivi, "Ni lugha nzuri kuliko zote ulimwenguni"

Andrew aliweza kuyapata makundi kadhaa ya kanisa katika eneo lile na kufanikiwa kupanga kuonana na mwenyekiti na katibu wa dhehebu fulani. Kwa bahati mbaya, ingawa Andrew na watu hao walijua lugha kadhaa za Ulaya, wakajikuta hawana lugha hata moja waliyoijua wote. Basi, wakakaa pale wakikodoleana macho tu. Andrew alikuwa amesafiri maili nyingi za hatari na ule mzigo wake wathamani, lakini ikaonekana ya kwamba hapakuwa na njia yoyote ya kujua iwapo watu wale walikuwa ni ndugu Wakristo wa kweli au makachero wa Serikali.

Hatimaye akaiona Biblia ya Kiroma juu ya meza katika ofisi ile. Andrew akaingiza mkono wake katika mfuko wake na kuichomoa Biblia ya Kiholanzi. Alifunua 1 Wakorintho 16:20, na kuishika Biblia akiwa amenyosha mkono wake akisonda kidole chake kwenye jina la Kitabu kile waliweza kulitambua. Mara moja nyuso zao zikang'aa kwa meru. Upesi wakaipata sura ile ile na fungu lile lile katika Biblia zao za Kiromania, Kisha wakasoma maneno haya: "Ndugu wote hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu."

Watu wale wakatabasamu na kumwangalia Andrew. Kisha mmoja wao akapekua katika Biblia yake na kupata Mithali 25:25. Andrew akalipata fungu lile na kulisoma "kama vile maji baridi yalivyo kwa mtu mwenye kiu, ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali "

Watu wale walitumia nusu saa wakiongea na kupeana habari - kwa kupitia tu katika maneno ya Maandiko. Walikuwa na furaha nyingi sana kwa urafiki wao huo uliovuka mipaka yote ya utamaduni hata wakacheka mpaka machozi yalipowatoka.

Andrew alijua kwamba amewapata ndugu zake. Alipowaonyesha mzigo wake wa Biblia, Waromania wale walitekwa nao wakamkumbatia tena na tena.

Jioni ile katika ile hoteli, yule karani alikuja karibu na Andrew na kusema kwa mshangao, 'Aisee, nilitafuta 'agape' katika kamusi. Hakuna lugha ya jina lile. Hilo ni neno la Kigiriki limaanishalo upendo.

Andrew akajibu "sawasawa. Mimi nilikuwa nazungumza kwa kutumia neno hilo mchana kutwa".

Je! Wewe umeigundua lugha hiyo nzuri? Katika mwongozo huu utajifunza juu ya jinsi Mungu anavyoweza kutuleta sisi sote katika jamii yake kubwa ya upendo.

1. Kanisa Lilianzishwa Kwa Ajili Ya Ushirika

Yesu alilianzisha kanisa ili kukidhi hitaji la msingi la kibinadamu la malezi na kusaidiana. Sisi sote tunayo mahitaji yetu. Na hivyo ndivyo kanisa linavyohusika na mambo hayo yote. Hapo ni mahali tunapokuja ili kushirikiana na kusaidiana. Maandiko yanalidhihirisha kanisa lile lenye nguvu la Mitume ambalo liliwaita wanaume na wanawake kuja katika ushirika uliojaa furaha ambao ulikwenda juu ya njia yote hadi kwa Mwenyezi:
"Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kujiunga nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike" - 1 Yohana 1:3,4.

Mioyo yenye mawazo sawa iliyofungwa pamoja kwa njia ya mawasiliano na Yesu na mawasiliano ya wao kwa wao, huionja "furaha kwa kiwango chake chote! Wote wanaongea lugha moja, lugha ile ya upendo.

Wakristo wanakuwa sehemu ya familia iliyotandaa. Wanakuwa ndugu na dada katika Kristo kwa kuwa wote wanayo roho ya undugu. Kadiri unavyozidi kupanuka umoja huo wa imani, ndivyo kadiri vifungo vyenye nguvu zaidi vinavyokuwepo miongoni mwa Wakristo.

Washiriki wa makanisa yale yaliyoanzishwa na mitume wa Yesu walifungwa pamoja wakiwa na itikadi zao zinazofanana, kwa upendo wao waliokuwa nao kwa Mungu na kwa shauku yao ya kumtumikia na kuugawia ulimwengu huu neema yake. Kifungo hicho cha ushirika wao wa karibu sana kilikuwa kimojawapo ya sababu zilizowafanya watu wale wachache wasiokuwa na nguvu, ambao walikuwa wakiteswa, kuupindua ulimwengu wa wakati ule.

2. Kanisa Aliloanzisha Kristo

Je! Hivi Kristo analo kanisa, au wazo zima juu ya shirika la dini ni mavumbuzi tu ya wanadamu? Yesu anajibu hivi:
"Juu ya MWAMBA huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda" - (Mathayo 16:18).

Yesu ndiye ule Mwamba wa kutia nanga zetu, Jiwe la pembeni la kanisa lake.

Je! Ni kusudi gani ambalo lilikuwa sehemu ya msingi wake?

"Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ni jiwe la pembeni" - Waefeso 2:20.

Je! Injili ile ilipohubiriwa, Bwana alifanikiw akufanya nini?
"Na Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa" - (Matendo 2:47, KJV).

Yesu alipoanzisha kanisa lile, aliahidi kwamba "milango ya kuzimu haitalishinda"(Mathayo 16:18), na kanisa la Kikristo mpaka sasa linaendelea kuwapo. Limepata kuwa na maadui wenye nguvu nyingi kabisa kuanzia na wafalme wale wa Dola ya Kiroma hadi kwa madikteta wa Kikomunisti lakini damu ya wafiadini imelifanya lizidi kuwa na nguvu nyingi. Mkristo mmoja alipochomwa moto kwenye mti wa kuchomea au alipotupwa kwa simba, wengine kadhaa walijitokeza kuchukua nafasi yake. Watu wenye nadharia ya kushuku mambo ya Mmungu wamefanya kila waliloweza kujaribu kutoa sababu zao na kulipotosha kanisa. Lakini ile kweli ya Kikristo inashindana nao kwa ufasaha sana kuliko hapo kwanza katika kizazi hiki cha sayansi na kinachopenda mambo ya ulimwengu.

Mojawapo ya changamoto kuu kuliko zote kwa kanisa ilikuja mara tu baada ya kukubalika kwake kama dini rasmi ya Dola ya Roma. Kanisa likapata utajiri mwingi - na hatimaye likaharibika. Likaonekana limekufa kiroho katika zile zama za giza. Lakini siku zote Bwana alihifadhi sehemu ya maana ya waumini waliokuwa wajasiri na waaminifu ambao katikanyakati zile zisizokuwa na matumaini na ngumu, waling'aa sana kama nyota wakati wa usiku usiokuwa na mbalamwezi.

Paulo analinganisha uhusiano uliopo kati ya Kristo na Kanisa lake na uhusiano ule wa upendo, unaotunza, wa mume kwa mke wake (Waefeso 5:23-25). Kanisa ni familia, kila mshiriki akifanya uhusiano wake na washiriki wengine wa familia hiyo na kuchangia katika usitawi wao (Waefeso 2:19)

Paulo pia analionyesha kanisa kama mwili hai, Kristo mwenyewe akiwa ndiye kichwa chake (Wakolosai 1:18).

Tunapokuwa tumebatizwa, tunatoa ushuhuda wa imani yetu ndani ya Yesu na kuwa washiriki wa ule "mwili" yaani kanisa.

"Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote TUMEBATIZWA kwa Roho mmoja KATIKA MWILI HUO MMOJA; na sote tukanyweshwa Roho huo mmoja" - (1 Wakorintho 12:13).

Kitabu cha ufunuo kinaonyesha picha ya Kristo aliyefufuka akitembea katikati ya makanisa akionyesha ulinzi wake alionao juu yake (Ufunuo 1:20,12,13). Kristo hajawaacha watu wake kamwe, wala hatawaacha kamwe.

3. Kanisa Lenye Kusudi Maalum

Kuhudhuria kanisani ni kwa maana sana kwa Mkristo. Tunahitaji msaada wa wengine kuifanya imani yetu iwe hai na iendelee kukua.
Kanisa pia lina wajibu wa maana wa aina tatu:

i) Kanisa linalinda kweli.
Likiwa ni "nguzo na msingi wa kweli" (Timotheo 3:15), kanisa linatetea na kuilinda kweli ya Mungu mbele ya ulimwengu.
Tunahitaji hekima ya pamoja ya waumini wengine ili kutusaidia kukuza mawazo yetu juu ya kweli zile zilizo za muhimu za maandiko.
ii) Kanisa ni kielelezo cha jinsi neema ya Mungu iwezavyo kuwatendea wenye dhambi. Mabadiliko aliyoyafanya Kristo katika maisha ya waumini humtangaza Mungu atuitaye sisi "Katika nuru yake ya ajabu" (I Petro 2:9).
iii) Watu wa Mungu ni mashahidi wake kwa ulimwengu huu wenye shida. Kabla tu hajarudi mbinguni, Yesu aliwaahidi wanafunzi wake, alisema.

"Lakini mtapokea nguvu Roho Mtakatifu akiisha kuwajilia juu yenu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na ktika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi" - (Matendo 1:8).

Ni heshima kubwa kwa kanisa kuupeleka huo ujumbe wa pendo kuu la Mungu ulimwenguni kote.

4. Limeanzishwa Kwa Ajili Ya Kutiana Nguvu

Kanisa lile alilolianzisha Kristo lilikuwa na mfumo halisi. Mtu aliweza kuingizwa au kutoingizwa katika ushirika wake (Mathayo 18:15-18). Kanisa la Mungu liliwachagua viongozi, tena lilikuwa na makao makuu ya ulimwengu pamoja na sehemu za kukutania za kila mahali (Matendo 8:14;14:23;15:2 1Timotheo 3: 1-13) Walipokwisha kubatizwa, waumini walijiunga na kundi lililokuwa limeanzishwa. (Matendo 2:41 na 47).

Kanisa lipo kwa ajili ya kutiana moyo.

"Hebu na tufikirie jinsi tuwezavyo kuhimizana katika upendo wa kazi nzuri. Tusiache kukusanyika pamoja, kama wengine walivyozoea kufanya, bali TUTIANE moyo sisi kwa sisi - na kuzidi kufanya hivyo kadiri mwonavyo. Siku ile (ya kuja kwake Kristo) kuwa inakaribia. "-Waebrania 10:24,25.

Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo yafanywayo na kundi la Kanisa lenye afya. Washiriki wake wanajengana katika imani, wanatiana moyo wao kwa wao. Mungu alilianzisha Kanisa lake ili kuwatia nguvu watu wa Mungu na pia kutoa huduma kwa ulimwengu huu. Twaweza kufanya mambo mengi sana tukiwa pamoja kuliko tuwezavyo kufanya mambo mengi sana tukiwa pamoja kuliko tuwezavyo kufanya kama mtu mmoja mmoja hapa na pale. Chukua mfano mmoja tu. Kanisa la Waadventista Wasabato. Sisi tunaendesha kazi ya uganga katika eneo kubwa sana ulimwenguni kote - kuanzia yale magari ya afya yaliyo ndani kabisa ya mji mkuu kwenda kwenye kliniki zilizo katika visiwa vilivyojijenga mbali katika bahari ya Pasifiki ya Kusini. Taasisi zetu za elimu zimewaletea makumi ya maelfu ya vijana maarifa ya maisha bora ndani ya Kristo - kuanzia Chuo kikuu cha Loma Linda, kinachoongoza katika kazi ya kupandikiza mioyo, kwenda kwenye shule ndogo kabisa za misheni zilizotawanyiika ndani ya nchi zote za Afrika. Sisi tunashughulika na njaa na maafa kupitia ADRA. Makanisa yaliyo katika maeneo mbali mbali yanawavika nguo na kuwalisha maskini na wasio na kwao katika maelfu ya vituo vya huduma kwa jamii. Nayo makundi ya waumini wa Kiadventista wanahubiri ujumbe wa wokovu katika nchi zaidi ya 200. Ni lile kundi la Wakristo waliojitoa wakfu tu lililoundwa ambalo lingeweza kuleta matokeo hayo kwa ulimwengu mzima.

Kristo na mitume walilifananisha Kanisa na mwili, na kuonyesha kwamba sehemu zote za mwili zinahitajika (1Wakorintho 12:21-28). Sehemu zote za mwili hazifanani kabisa, lakini zote ni za muhimu na zote hazina budi kufanya kazi pamoja kwa ushirikiano.Jicho lililojitenga na mwili haliwezi kuona.

Mkono uliokatwa hauna faida yeyote. Si kitu kama sisi tu jicho, mkono, au kidole tu, hatuwezi kutenda kazi yetu kwa ajili ya Kristo kwa ufanisi kama kila mmoja wetu anajitegemea mwenyewe kabisa. Kuwa mshiriki wa kanisa, kuungika na viungo vingine vya mwili hututua nguvu sisi kama wakristo.

5. Furaha Ya Kuabudu

Ndani kabisa ya mioyo yetu imo shauku ya kumwabudu Mungu, na haja hiyo yaweza kufifia au kutoweka tusipoiiruhusu kufanya kazi yake. Je! Mtunga Zaburi alijisikiaje alipofikiria kwenda mahali pale pa ibada?
"NALIFURAHI pamoja na wale walioniambia, "Na twende nyumbani mwa BWANA" - (Zaburi 122:1).

Je! Muziki una sehemu gani katika ibada ya watu wote?
"Mwabuduni BWANA kwa furaha, "Njoni mbele zake kwa nyimbo za furaha" - (Zaburi 100:2).

Biblia inatuambia kwamba kutoa sadaka ni sehemu murua ya ibada ya Mungu.

"Leteni sadaka mkaziingie nyufa zake. Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu" - (Zaburi 96:8-9).

Maombi nayo pia ni sehemu ya maana ya ibada ya watu wote.

"Njoni tusujudu katika ibada tupige magoti mbele za BWANA MUUMBAJI wetu' - Zaburi 95:6

Kujifunza Biblia na kuhubiri ni kitovu cha ibada ya Agano Jipya. Kuanzia na lile hubiri la Petro katika ile siku ya Pentekoste, ambalo linapatikana katika Matendo 2, na kuanzia katika nyakati zile za wanamatengenezo ya kanisa wale wakiporotestanti hadi katika hizi siku zetu, kila uamsho mkuu wa kidini umejengwa juu ya mahubiri yatokanayo katika Biblia. Hivi kwa nini? Kwa sababu "Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu. Lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili" - (Waebrania 4;12-13).

6. Je Kitu Gani Ni Chema Kuhusu Kanisa?

Wengine hupinga na kusema kwamaba kanisa limejaa watu ambao si wakamilifu. Lile alilolisema Henry Ward Beecher ni la kweli:
"Kanisa sio nyumba ya sanaa ya maonyehso ya Wakristo maarufu, bali ni shule kwa ajili ya kuwaelimisha hao wasio wakamilifu.

Kwa kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwetu aliye mkamilifu, basi kanisa halitakuwa kamilifu pia.

Katika mmojawapo wa mifano yake Yesu alitukumbusha sisi kwamba magugu huota pamoja na ngano (Mathayo 13:24-30). Tunapozisoma nyaraka za Paulo za Agano Jipya, tunagundua kwamba kanisa lile la mitume lilikuwa na matatizo makubwa sana. Na kanisa la leo mara nyingi lina upungufu mkubwa. Lakini,. Tafadhali, kumbuka kwamba hakuna washriki wenye makosa wawezao kuliharibu au kulivuruga lile Jiwe kuu la Pembeni la kanisa - yaani, Yesu Kristo mwenyewe. Basi, ndani ya makanisa yasiyo makamilifu yatupasa kukaza macho yetu juu ya Mwokozi wetu anayetuhudumia na kulipa jambo hilo umuhimu wa kwanza. Licha ya makosa yake, kanisa ni mali yake, basi, ninyi kazeni macho yenu juu ya Kristo.

"Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake. Alifanya hivyo ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada yakulifanya safi kwa kulioshakatika maji, kusudi ajipatie kanisa lililo takattifu na safi kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au cho chote cha namna hiyo" (Waefeso 5:25 - 27).

Kanisa ni la maana sana kwa Yesu hata akajitoa nafsi yake kwa ajili yake alipokufa kwa ajili ya kila mmoja wetu na kanisa kwa jumla. Kwa hiyo, ushirika wa kanisa kwako wewe ungepaswa kuwa wa maana. Je ! hivi wewe ni mshiriki wa mwili wa Kristo?

7. Kulipata Kanisa Hilo

Je! Ni imani ngapi za kweli alizonazo Yesu uliwenguni humu?
"Kuna mwili (kanisa) mmoja , na roho mmoja…. Bwana mmoja, Imani Moja, Ubatizo mmoja" - (Waefeso 4:4,5).

Kwa vile Kristo anayo "imani moja" tu, je! Twawezaje sisi kujua ni imani ipi hiyo? Yesu anatupatia sisi ufunguo wake huu:
"Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe" - Yohana 7:17. (Angalia pia Yohana 8:31,32).

Tunapojitoa wenyewe kufanya mapenzi ya Mungu, atatusaidia sisi kujua endapo mafunzo hayo yanatoka kwa Mungu, au ni mapokeo tu ya wanadamu. Tunapolitafuta hilo kanisa jambo kuu ni kuchunguza jinsi linavyoliheshimu na kulitii Neno la Mungu. Ushirika wa kweli umejengwa juu ya maandiko, sio juu ya kiongozi mmoja mwenye uwezo wa ajabu au taasisi moja kuu.

Endelea kufanya ugunduzi wako mwingi katika miongozo hii, tembea katika nuru anayokufunulia Mungu kutoka katika Biblia, naye atayafunua mapenzi yake kwako. Mkristo anayekua ni mtu anayeufungua moyo wake na akili yake ili kuipokea ile kweli kama Mungu anavyoifunua kutoka katika Neno lake.

bottom of page