top of page

Gundua

bible-study-lesson-tips-small-group-lead
Ugunguzi.jpg

Miongozo Mbalimbali

bible-png-clipart-12.png

16. SIRI YA PUMZIKO LA MBINGUNI

Miaka michache tu iliyopita wengine walikuwa wakibashiri kwamba muda si mrefu tungekuwa na muda mwingi sana wa mapumziko ambao tungeshindwa kujua tufanye nini nao. Hizi zilikuwa ndizo sababu nzuri kwa ubashiri ule wenye matumaini. Katika miji mikuu ya ulimwengu makompyuta yalikuwa yakizisaga-saga kazi ambazo zingechukua mwezi mzima kuzifanya kwa sehemu tu ya nukta moja. Na yale maroboti yalikuwa yameanza kuzifanya kazi ngumu sana za kuchosha katika viwanda vya kutengeneza mashine nzito.

Lakini baada ya makompyuta hayo kutoa mfumo wao na maroboti kufanya kazi zao, bado tunakosa hata pumzi kuzifanya kazi hizo muda wa siku hizi. Zaidi ya yote, familia zinakosa muda wa kukaa pamoja. Waume na wake zao huona vigumu kupanga "muda unaofaa" wa kuwa pamoja na watoto wao, licha ya wao wenyewe kuwa na muda mchache wa kuwa pamoja.

Utafiti mmoja uliofanywa katika jumuia moja ndogo ulionyesha kwamba wastani wa muda kila siku ambao mababa wanatumia wakiwa peke yao na watoto wao wadogo sana ulikuwa nukta 37! Familia hazina muda, wala hazina mawasiliano.

Je! Tunawezaje kupunguza hiyo kasi tuliyonayo kwa kiasi cha kutosha kuweza kuwa na uhusiano wetu tena?

1. Dawa Ya Maisha Yaliyojaa Mahangaiko

Yesu anayajua matatizo ya familia zilizo chini ya shinikizo hilo, naye anataka sisi tujue kwamba pumiziko la kiroho ni sehemu ya maisha bora; "NJONI KWANGU, ninyi nyote mliochoka na maisha na kulemewa na mizigo, NITAWAPUMZISHA… MJIFUNZE KWANGU, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata RAHA NAFSINI MWENU." Mathayo 11:28, 29.

Biblia inatushauri kuionja hiyo raha kwa njia mbili: Kumwendea Kristo kwa kutegemea msingi huu wa aina mbili, KILA SIKU na KILA JUMA.

2. Kuungana Na Yesu Kila Siku

Makundi ya watu wakati wote yalikuwa yakidai Kristo awasikilize wao tu. Naye Kristo bado aliweza kuonyesha moyo wa amani, mtulivu, kwa kila mmoja aliyemzunguka. Hivi ilikuwaje? Alitumia muda wake kila siku kuongea na Baba yake aliye mbinguni. Alimtegemea Baba yake daima ili kupata nguvu za kumwezesha kukabiliana na changamoto za maisha (Yohana 6:57).

Endapo sisi tunataka kuishi maisha matulivu, na manyofu kama yeye alivyoishi, basi yatupasa kumtegemea Yesu daima - turuhusu Neno lake na Roho wake kutujaza na kututengeneza. Njia bora kuliko zote ya kuzipinga nguvu zile zinazotuunguza sisi kama mtu mmoja mmoja na kututenganisha kifamilia na ile ya kutumia muda ulio bora pamoja na Kristo. Yeye anatuambia hivi:
"KAENI NDANI YANGU, nami ndani yenu…. PASIPO MIMI HAMWEZI KUFANYA NENO LOLOTE" -(Yohana 15:4,5).

Mojawapo la mahitaji yetu makuu kuliko yote kwa kipindi chetu hiki ni lile la kutega nguvu za Kiroho zipatikanazo kwa njia ya kujenga uhusiano wa siku - kwa siku na Yesu. Jambo moja la maana sana linalotakiwa kusisitizwa juu ya uhusiano wetu na Kristo ni kazi yake iliyokamilika pale msalabani pumziko la kweli, usalama halisi, mambo hayo yanaweza kuwapo tu kwa sababu ya lile jambo moja kuu alilolifanya Yesu ambalo linatajwa wakati ule alipolia kwa sauti kuu alipokuwa akifa, alisema. "Imekwisha" (Yohana 19:30). Kwa maneno mengine, ile kazi yake ya kutukomboa sisi ilikuwa imekamilika.

Maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa, nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe dhabihu. - (Waebrania 9:26).

Yesu alipokufa, aliziondoa dhambi". Ndiyo maana yasemekana kwamba Muumini aliyeziungama dhambi zake anaweza "Kupumzika" katika kazi ile iliyokamilika ya Kristo. Sisi tunakubalika.

Hatia imejificha katika nyumba ya haraka ya kiwendawazimu tuliyo nayo katika maisha yetu siku hizi. Lakini Yesu alilisuluhisha tatizo hilo la hatia mara moja tu pale msalabani. Kilio cha Yesu, alichosema, "Imekwisha" kilitia muhuri ahadi yake aliyosema "Nitawapumzisha" na kuifanya iwe ni jambo la kweli kabisa. Kristo aliikamilisha kazi yake ya kutukomboa sisi pale Kalvari (Tito 2:14), halafu akapumzika kaburini siku nzima ya Sabato, na kufufuka kaburini siku ya Jumapili asubuhi kama mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Mkristo hawezi kuwa na ahadi kubwa kuliko hiyo ya kupumzika katika kazi ya Kristo ile iliyokwisha.

"Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi. Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu." - Waebrania 10:22,23 kwa kuwa yeye "aliyeahidi ni mwaminifu," basi, sisi tunaweza kuingia katika pumziko la wokovu ambalo Yesu ametuahidi. Uthabiti, amani, na pumziko tunaloliona ndani ya Yesu kila siku ni matokeo, sio ya neno lolote tulifanyalo, bali ya kile alichokifanya pale msalabani.

Tunaweza kupumzika ndani ya Kristo kwa sababu wokovu wetu ni wa hakika. Uhakika huo hututia moyo kutumia wakati wetu pamoja na Kristo kila siku, tukijilisha Neno lake na kuvuta hewa ya mbinguni kwa njia ya maombi yetu. Mahali pale pa kukutana na Yesu hutusaidia sisi kuyageuza maisha yetu yaliyojaa mahangaiko na kuyafanya yawe ya amani na yenye lengo maalum.

3. Kuungana Na Yesu Kila Juma

Baada ya Kristo kuiumba dunia hii kwa siku sita (Wakolosai 1:16-17), alitoa pumziko la Sabato. Ni nafasi ya kila juma tuliyopewa ili kuuendeleza mwungano wetu huo pamoja naye.

"Mungu akaona kila kitu alichofanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni ikawa asubuhi; siku ya sita. Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. Siku ya saba Mungu akawa amemaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya. Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba" - (Mwanzo 1:31-2:3).

Kama Muumbaji wao, Yesu "akapumzika" Sabato ile ya kwanza pamoja na Adamu na Hawa, naye "akaibariki" siku ya Sabato na "kuifanya takatifu". Mungu ndiye aliyeuanzisha mzunguko wa juma - la - siku - saba, si kwa faida yake mwenyewe, bali kwa faida ya Adamu na Hawa na kwa faida yetu sisi leo. Kwa kuwa aliwapenda sana watu wale aliokuwa amewaumba, alipanga kwamba kila siku ya saba katika maisha yao yote ingewekwa wakfu kwa ajili ya kutafuta kuwako kwake yeye. Kila Sabato, kama yeye alivyoiita, ilipaswa kuwa siku ya pumziko la kimwili na burudiko la Kiroho. Kuingia kwa dhambi katika ulimwengu wetu kulifanya haja ya pumziko la Sabato iwe kubwa zaidi.

Mwokozi yule aliyemwahidi Adamu na Hawa "pumziko" lile, alimpa Musa, mnamo miaka elfu mbili baadaye, sheria juu ya ule Mlima Sinai (1Wakorintho 10:14) Yesu alichagua kuiweka amri ile ya pumziko-la-Sabato katikati kabisa ya zile amri Kumi. Amri ya nne inasomeka hivi:
"IKUMBUKE SIKU YA SABATO KWA KUITAKASA. Siku sita utafanaya kazi, na tenda mambo yako yote, Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako wala mtumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye nyumbani mwako. Maana, kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na duniai, bahari, na vyote vilivyomo, kisha NIKAPUMZIKA siku ya saba. Kwa hiyo, MIMI MWENYEZI-MUNGU NILIIBARIKI siku ya Sabato na NIKAITAKASA" - (Kutoka 20:8-11).

Mungu aliianzisha Sabato kama siku inayopaswa kum"kumbuk(a)" Bwana aliye "zifanya mbingu na nchi." Pumziko - la-Sabato la kila juma linatuunganisha sisi na Muumbaji wetu aliyeibariki siku hiyo na kuitenga.

Yesu alipoishi hapa duniani, aliitumia vizuri kila nafasi nzuri kwa kudumisha mwungano huo na Baba yake. Alinufaika na pumziko-la-Sabato kwa kuabudu siku ya Sabato, kama Luka anavyotusimulia:
"Akaenda Nazareti, mahali alipolelewa, na SIKU YA SABATO akaingia katika singagogi, KAMA ILIVYOKUWA DESTURI YAKE." - (Luka 4:16).

Ikiwa Yesu aliyekuwa Mungu - Mwanadamu alihitaji kupumzika mbele za Baba yake siku ya Sabato, basi, sisi tulio wanadamu kwa hakika tunalihitaji zaidi hilo pumziko. Yesu alipozifagilia mbali sheria zile zilizoweka vizuizi vingi walivyokuwa wameviweka Wayahudi katika ile Sabato (Mathayo 12:1-12), yeye aliwaonyesha kwamba Mungu alikuwa ameiweka Sabato kwa ajili ya kuwaletea watu manufaa.

"Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia" - (Marko 2:27,28).

Yesu alisisitiza sana umuhimu wa Sabato hata wakati wa kifo chake. Alikufa Ijumaa, "Siku ya Maandalio, na Sabato ikaanza kuingia "(Luka 23:54). Wakati ule alitangaza. Akasema, "Imekwisha," yaani, kazi yake ya kuja hapa duniani na kufa kama badala ya taifa zima la Kibinadamu ilikuwa imekamilika (Yohana 19:30; 4:34; 5:30). Kisha ili kusherehekea utume wake uliokwisha, Yesu alipumzika kaburini Sabato ile nzima.

Kama Kristo alivyomaliza kazi yake ya uumbaji katika siku ile ya sita, kisha akapumzika siku ya Sabato, ndivyo kwa kufa kwake msalabani alivyomaliza kazi yake ya ukombozi katika siku ile ya sita, na halafu akapumzika siku ile ya saba.

Jumapili alfajiri Yesu alitoka kaburini kama Mwokozi Mshindi (Luka 24:1-7), Tayari alikuwa amewataka wanafunzi wake kuendelea kukutana naye siku ya Sabato baada ya ufufuo wake. Akizungumza juu ya kuangamizwa kwa Yerusalemu, ambako kulitokea karibu miaka arobaini hivi baada ya kifo chake, aliwaagiza, alisema.

"Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya Sabato." Mathayo 24:20.

Mwokozi wetu alitaka wanafunzi wake pamoja na waongofu wao waendelee na desturi alizokuwa amewafundisha (Yohana 15:15,6). Aliwataka wayaonje yote mawili, yaani, pumziko - la - Wokovu na pumziko - la -Sabato. Hawakumwangusha. Wanafunzi wake waliendelea kuitunza Sabato baada ya kifo chake Kristo (angalia Luka 23:54-56; Matendo 13:14; 16:13; 17:2:18:1-4).

Yohana yule aliyependwa sana alidumisha mwungano wake wa kila juma na Kristo katika siku ya Sabato. Katika miaka yake ya baadaye aliandika, akisema, "Siku ya Bwana nilikuwa katika roho" (Ufunuo 1:10). Kulingana na msimamo wa Yesu, "Siku ya Bwana" ni Sabato, "Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato "(Mathayo 12:8).

Siku ya Sabato tunaadhimisha mambo makuu kuliko yote mawili aliyoyakamiisha kwa ajili yetu. Yaani, kutuumba sisi na kutuokoa. Uzoefu huo wa kuitunza Sabato utaendelea kule mbinguni:
"Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, anatangaza BWANA,… 'toka Sabato hata Sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema BWANA" - (Isaya 66:22,23).

4. Manufaa Ya Pumziko-la-sabato

Siku hizi watu wanakanyagana ovyo katika maisha yao ya kiwendawazimu. Watu wanateketea mmoja mmoja. Famili zinasambaratika chini ya shinikizo. Lakini Mungu anawapa Sabato yake kama njia bora zaidi ya kuishi yale maisha mema.

Hebu na tuyaangalie baadhi ya manufaa ya pekee ya hilo pumziko-la-Sabato:

i) Sabato ni kumbukumbu ya uumbaji, na kwa kuitakasa, tunamjengea kumbukumbu Muumbaji wetu. Saa zake takatifu zinatupa nafasi nzuri ajabu za kushughulikia na maisha yetu mapya tuliyoyaanza katika dunia hii iliyoumbwa na Mungu. Je! ni lini kwa mara ya mwisho wewe au familia yako mlitumia muda wenu kwa kuzama kabisa katika kutafakari ule uzuri mtulivu wa njia ile ya msituni au kijito kile kinachotiririka kupitia katika miamba ile? Sabato inatupa muda wa kutumia pamoja na Yesu na kuona kidogo tu maajabu yake aliyoyafanya kwa ajili yetu.

ii) Siku ya Sabato tunaionja furaha ya kumwabudu na kushirikiana na Wakristo wengine. Kuna faida katika kumsifu Mungu tukiwa pamoja na wengine kama kundi la watu waabuduo pamoja. Sabato inatupa sisi muda wa pekee wa kukusanyika pamoja kama kundi la kanisa na kuzichaji upya betri zetu za kiroho.

iii) Sabato inatupa sisi fursa ya kutenda matendo ya wema kwa kuwafikiria wengine. Je! jirani yako amekuwa mgonjwa katika juma hili ulipokuwa huna nafasi ya kumtembelea? Rafiki yako alipotaka umsikilize kwa kusikitika pamoja naye kwa kufiwa na mumewe, je! shinikizo la maisha yako ya kila siku lilimnyima mama huyo upendo wako wa kwenda kumtazama? Yesu alitoa shauri hili: "Ni vyema kutenda mema siku ya Sabato" (Mathayo 12:12).

iv) Sabato ni Siku ya kuviimarisha vifungo vya Familia. Yesu alipoamuru hivi, "Siku hiyo (ya Sabato) usifanye kazi yoyote" (Kutoka 20:10). Asingekuwa ametoa dawa nzuri zaidi kwa mababu walio walevi wa kazi na kwa akina mama wanaosumbuka sana. Sabato ni ishara kubwa sana isemayo SIMAMA kwa familia nyingi. Simama na kuacha kuyaruhusu mambo yale ya muhimu zaidi kwako mambo yale yaliyo ya maana sana. Sabato ni siku moja ambayo katika hiyo tunaweza kuondoa shinikizo na mahali pake kuweka maombi, kuondoa kazi ngumu na kuweka kicheko badala yake, kuziondoa ratiba zenye shughuli nyingi na mahali pake kuweka tafakuri ya kimya kimya. Pumziko -la-Sabato huipa familia nzima muda wa kuungana na Kristo na kuchota nguvu za Kiroho kutoka kwake (kwa matumizi yetu).

v) Sabato ndio wakati ambapo Yesu anakuja karibu nasi zaidi kwa njia ya pekee. Kila uhusiano uliopo unahitaji muda unaofaa uwepo, na uhusiano wetu na Kristo hauna tofauti. Kuitumia siku nzima kwa ajili yake Kristo kila juma ndiyo njia kuu ya kuufanya urafiki wetu naye uwe safi na wa kufurahisha sana. Sabato inatupa muda wa ziada kwa ajili ya kujifunza Biblia na maombi, muda wa ziada wa kuwa peke yetu pamoja na Kristo mahali pa kimya na kusikiliza.

Yesu "akaibariki siku ya saba na kuifanya takatifu" kwa ahadi ya kuwako kwake (Mwanzo 2:3). Unaweza kuelewa kwa nini ni jambo la maana kuitunza Jumamosi, siku ya saba ya juma, kama Kristo aliitenga wakati ule wa uumbaji ili apate kuitumia kwa kuwasiliana nasi kwa njia ya pekee.

Yesu alipoifanya Sabato yaonekana kabisa kwamba alikuwa anakifikiria kizazi chetu mawazoni mwake. Ndiyo tunayoihitaji hasa katika mazingira yetu ya maisha yaliyojaa shinikizo. Ni siku ambayo inatutenga kweli mbali kabisa na mambo mengine yote. Ni siku ya kumwabudu Mungu, kuwasiliana tena na uumbaji wake, na kuuimarisha uhusiano wetu badala ya kuvishuhulikia vitu.

5. Ni Kilionja Mapema Pumziko La Mbinguni

Tunaweza kufanya muhtasari wa manufaa tunayoweza kupata kwa kujiunganisha na Kristo kwa njia ya kukutana naye KILA SIKU na KILA JUMA kwa kutumia neno moja tu - pumziko. Neno hili "Sabato" linatoka katika neno la Kiebrania limaanishalo pumziko, basi, si jambo laajabu ya kwamba Maandiko yanaiita hiyo siku ya saba kuwa ni "Sabato ya kupumzika kabisa" (Mambo ya Walawi 23:3).

"(Mungu) amesema juu ya siku ya saba kwa maneno haya: Siku ya saba Mungu alipumzika na kuacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya…. BASI LIMESALIA PUMZIKO-LA-SABATO KWA WATU WA MUNGU…. Basi, na tufanye bidii kuingia katika pumziko lile"- ( Waebrania 4:4-11).

Kulionja hili "Pumziko-la-Sabato" kila juma hutuwezesha sisi kuionja mapema ile furaha tutakayoipata katika lile pumziko kamilifu kule mbinguni. Pumziko lile sikukaa tu kivivu, linamaanisha kujisikia u salama moyoni, una hali ya amani na hali njema ya maisha iliyo katika shina lile la maisha tele ya kweli. Aina hiyo ya pumziko la kiroho inaweza kuthaminiwa tu kwa kulionja. Ushuhuda wa wale walioonja pumziko-la-wokovu pamoja na hilo pumziko-la-Sabato unajulikana kote. "Kama wewe umeingia katika pumziko la Yesu kwa njia ya kuungana naye kila siku na kila juma, basi, utaigundua furaha kuu kuliko zote katika maisha yako."

Je! ungependa kumshukuru Yesu kwa zawadi yake hiyo ya pumziko? Je, ungependa kumshukuru kwa ahadi yake ya pumziko-la-wokovu analokupa kila siku ili kukabiliana na changamoto za maisha, na kwa ahadi yake ya kukupa pumziko-la-Sabato kila juma ili kuufanya imara uhusiano wako pamoja naye? Endapo wewe hujapata kamwe kufanya hivyo, Je! ungependa kuupokea wokovu anaokupa? Je, ungependa kumwambia kwamba unatamani kuitunza Sabato yake kila juma? Je! ungependa kumwambia, "Ndiyo, Bwana! Natamani kuipata furaha yangu katika siku ile uliyoiweka? Kwa nini usitoe ahadi yako kwake sasa?

(Huenda wewe unashangaa: Ni nani aliyeibadili Sabato kutoka Jumamosi kwenda Jumapili, siku ya kwanza ya juma? Badiliko hilo lilifanyika lini? Je! hivi Mungu alitoa idhini yake kwa badiliko hilo? Maswali haya yatajibiwa katika Mwongozo 21.)

bottom of page